Na Salum Vuai
KATIKA uzinduzi wa ‘Wiki ya Dk. Hussein Mwinyi’
Jumatatu Novemba mosi ikiwa sehemu ya maadhimisho ya kutimiza mwaka mmoja wa
uongozi wake, wananchi sote tulihamasika kusafisha miji na mitaa yetu ili
ipendeze.
Ukiachia Mkoa wa Kusini Unguja na Kaskazini Pemba
ambako zoezi hilo la usafi lilifanyika kitaifa, wananchi katika shehia
mbalimbali walionesha mshikamano mkubwa kuhakikisha nchi inakuwa safi.
Aidha, kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kamati ya
maadhimisho hayo Idrissa Kitwana Mustafa ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini
Magharibi, wito wa kufanya usafi ni utekelezaji wa kauli ya mara kwa mara ya
Rais Dk. Mwinyi kutaka tuipendezeshe nchi yetu kwa kuisafisha.
Kwa hakika uchafu una madhara makubwa kiafya na pia
unatoa taswira mbaya kwa watalii na wageni wengine wanaotutembelea, wakati
Zanzibar ni miongoni mwa visiwa vinavyovutia utalii ambao kwa sasa ndio chanzo
kikuu cha kuiingizia nchi mapato.
Kama ilivyo desturi na utamaduni wa Wazanzibari
unapofika msimu wa sikukuu kusafisha na kupamba nyumba zao kwa samani mpya,
mapazia na mavazi, ndivyo inavyopasa kufanya hivyo kwa nchi.
Wazanzibari wa itikadi zote za dini wamejenga
utamaduni huu wa kujipamba siku za sikukuu lakini Muhenga katika tafakuri yake
anauona ni mzuri.
Hata hivyo, utamaduni huu unafaa kuendelezwa hata
kusipokuwa na sherehe au maadhimisho ya tukio lolote kubwa la kijamii au
kitaifa.
Itakuwa aibu kama baada ya kuhitimisha sherehe za
kumpongeza Rais, kuona taka na uchafu wa karo zinazofurika unarudi tena
mitaani.
Nimelazimika kutoa tanbihi hii kwani imekuwa mazoea
miongoni mwa wananchi, kuwa wazuri wa kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya
wakati wa dharura tu mathalan kunapokuwa na maradhi ya mripuko.
Mara tu baada ya kudhibitiwa kwa maradhi ya kuambukiza
ikiwemo kipindupindu, watu hupuuza kuchukua tahadhari na kurudi katika mazoea
ya kula na kunywa bila kufuata masharti ya kiafya ikiwemo kuchemsha maji.
Katika jambo hili, kwanza kila siku tuhakikishe
mazingira ya ndani na nje kwa kila kaya yanasafishwa vizuri, takataka
zinachomwa moto na zile zisizochomeka zikusanywe ili wenye dhamana wapite
kuzichukua.
Aidha chini ya usimamizi wa masheha na kamati zao,
kuwekwe utaratibu kwa wakaazi wa mitaa kushirikiana kusafisha maeneo yao
angalau kila siku moja ya mwisho wa wiki.
Utaratibu huu uwe mbali na ule usafi wa kitaifa kila
mwisho au mwanzo wa mwezi ambao huko nyuma ulikuwa ukitekelezwa kila wilaya.
Kamwe Muhenga hatarajii zoezi la usafi lililofanyika
mwanzoni mwa wiki iwe njia ya kujikweza tu kwa mkuu wa nchi kisha watu warudi
katika tabia mbaya ya kutupa taka kila pahala.
Aidha, jamii ihamasishwe kutumia karo kwa ajili ya
kuhifadhi maji machafu yatokayo majumbani mwao, badala ya kuyamwaga mitaani
kupitia tobo wanazotoboa kwa kisingizio cha kuepuka karo zao kujaa.
Haipendezi kuwa katika mitaa kuna masheha na madiwani,
lakini wanaona muhali kuwachukulia hatua watu wanaotiririsha maji machafu nje
ya nyumba zao, jambo linalosababisha tope na harufu mbaya kuhanikiza.
Kwa hivyo, tunapomaliza kuadhimisha mwaka mmoja wa
uongozi wa Rais Dk. Hussein Mwinyi, tuhakikishe usafi hauondoki na sherehe hizo
kwa watu kuendelea kupuuza umuhimu wa kuyatunza maeneo yao.
Kufanya hivyo itakuwa istihizai ambayo itatusuta
wenyewe kwa kauli zetu kwamba tunampenda sana Mheshimiwa Rais na kuikubali kasi
ya utendaji wake katika kuiletea nchi yetu maendeleo.
Simu: 0777 865050/0714 425556
Baruapepe: mbumbwinihalisi@gmail.com
0 Comments:
Post a Comment