| Mkurugenzi wa TAMWA-ZNZ Dkt,Mzuri Issa,Picha kutoka Maktaba. |
Chama cha Waandishi wa Wahabari Wanawake Tanzania, Zanzibar, (TAMWA ZNZ) kinawapongeza Bi Salma Ali Hassan Khamis na Bi Mwanamkaa Abdulrahman Mohammed kwa kuteuliwa kuiongoza Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar.
Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar ina
majukumu mengi yakiwemo ya kupokea na kukagua faili zote zinazotoka Polisi,
kuchambua ushahidi wa upelelezi uliotoka polisi, kupeleka faili za kesi
mahakamani, kuendesha kesi Mahakamani kwa kuuwakilisha upande wa Serikali na
kukata rufaa iwapo haitaridhika na maamuzi ya Mahakama kuhusiana na shauri
lolote
Kupitia uteuzi huo uiliofanywa na Mheshimiwa Rais
wa Zanzibar,Dkt Hussein Ali Mwinyi hivi
karibuni, Bi Salma Ali Hassan Khamis ameteuliwa kuwa
Mkurugenzi Mkuu wa Afisi hiyo na Bi Mwanamkaa Abdulrahman Mohammed kuwa Naibu
Mkurugenzi wa Mashtaka katika Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar.
Hawa ni viongozi wa kwanza wanawake kuongoza
Afisi hiyo katika nafasi hizo kuu kabisa na hivyo kuongeza uwepo wa wanawake
katika nafasi za uongozi kwa jumla, hali ambayo inahimizwa kwa maendeleo ya
mwanamke na nchi kwa jumla.
TAMWA - ZNZ inaamini kuwa kuwepo kwa viongozi
hao, kesi za udhalilishaji na ukatili wa wanawake na watoto zitapata msukumo
mpya katika ufuatiliaji na uchunguzi na kwa muda mfupi ili kukomesha kabisa vitendo
hivyo vilivyokithiri nchini na ambavyo vinawaathiri zaidi wanawake na watoto.
Kwa mujibu wa takwimu kutoka Afisi ya Mtakwimu
Mkuu wa Serikali, jumla ya kesi 838 za udhalilishaji
ziliripotiwa kuanzia mwezi wa Januari hadi Agosti, 2021 ambapo wanawake walioathirika
ni 679 sawa na asilimia 81 na wanaume ni
166 sawa na asilimia 19.8.
Ukatili mwingine ni wanawake na watoto kupigwa
kwa mapanga kutokana na sababu zisizokuwa za msingi na kwamba wengi wa wahalifu
bado hawajakamatwa. Hivyo, tunashauri Wakurugenzi
wa Mashtaka kuandaa utaratibu maalum wa kushirikiana na Jeshi la Polisi ili
kurahisisha uchunguzi katika matukio ya aina hii.
TAMWA - ZNZ inawatakia kila la kheri Wakurugenzi
hao katika majukumu yao mapya na muhimu
na Mwenyezi Mungu awaongeze hekima, busara, ushirikishaji na uadilifu zaidi.
Dk. Mzuri Issa
Mkurugenzi
TAMWA, ZNZ
0 Comments:
Post a Comment