| Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Othman Masoud Othman |
MAKAMU wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Othman Masoud
Othman, amesema ni muhimu Zanzibar kuwa na Chombo rasmi chenye
uwezo na mamlaka ya kisheria kusimamia masuala yanayohusu
majaa na taka za aina mbali mbali zinazozalishwa kwenye maeneo tofauti nchini
yakiwemo mahospitali.
Mhe. Makamu ameyasema hayo leo Ofisini kwake Migombani Mjini
Zanzibar, katika kikao maalum cha muendelezo wa tathmini ya ziara yake ya
Kimazingira ya hivi karibuni, kilichowashirikisha watendaji wa Jiji la
Zanzibar, Manispaa , Mmalaka ya Usimamizi Mazingira na wa Wizara ya Nchi
Afisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ.
Makamu amesema pamoja na serikali kutumia zaidi ya
shilingi 21 bilioni, kufanya uwekezaji mkubwa wa ujenzi wa miundombinu ya
jaa la Kisasa huko Kibele, kutupa taka na kulinda mazingira, lakini jaa hilo
halitumiki ipasavyo kutokana na kuwepo changamoto ya rasilimali watu na bajeti
ya uendeshaji na hivyo kuelekea kutofikiwa matarajio ya jaa hilo.
Amefahamisha kwamba hatua ya kuwa na chombo cha aina hiyo
ni muhimu kwa kusaidia Zanzibar kuweka mfumo bora na sahihi zaidi katika hatua
za ukusanyaji wa taka, usafirishaji na usimamizi utakaokidhi haja na matarajio
kwa hali ya sasa na ya baadae katika utunzaji wa mazingira.
Amesema jaa la kibele lina mfumo bora wa kitaalamu katika
kusimiamia na kutenganisha taka za aina mbali mbali pamoja na uwezo wa
kuzalisha bidhaa kama vile mbolea, lakini baadhi ya vifaa vilivyopo ambavyo ni
vya gharama kubwa havitumiki kwa sababu mbali mbali jambo linalotishia
kutofikiwa matarajio ya kujengwa jaa hilo.
Aidha amesema jaa la kibele ni miongoni mwa majaa ya
kisasa na limeigharimu serikali kiasi kubwa cha fedha, lakini iwapo hakutakuwa
na chombo chenye jukumu rasmi la usimamizi wa taka, ujezi huo hautakuwa na
maana yoyote katika kuweka usafi na utunzaji wa mazingira nchini.
Othman pia katika kikao hicho aliagiza mamlaka zinazohusika na usimamizi wa jaaa hilo kuhakikisha wanaweka mipango bora na kutatua kwa haraka baadhi ya changamoto zilizopo ikiwemo uhaba raslimali watu na mafuta ya kuendeshea baadhi ya mitambo ya jaa hilo.
Naye meneja wa jaa la Kibele ndugu Hassan Mohammed Ali,
amesema, Kibele ni miongoni mwa majaa bora Afrika, lakini linakabiliwa na
changamoto nyingi ikiwemo baadhi ya vifaa kutotumika hadi sasa, kutupwa baadhi
ya taka hatarishi zikiwemo za hospitali licha kwamba kitaalam hazipaswii
kutupwa katika eneo hilo kwa vile zinaweza kuleta madhara makubwa
kwa binaadamu.
Aidha alisema kwamba pia Zanzibar inakabiliwa na tatizo la
ukosefu wa taarifa rasmi za taka , ambapo hadi sasa hakuna taarifa za
uhakika zinazochambua na kuainisha takwimu na kiwango halisi cha taka
kinachozalishwa kila siku nchini.
Kaimu Waziri wa Nchi, Afisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais
Dk. Khalid Salum Mohammed, amesema kwamba kuna haja ya kufikiria zaidi
matumizi sahihi ya jaa hilo hasa kwa kuwa limeigharimu serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kiwango kikubwa cha fedha.
Amesema kunahitajika muongozo rasmi wa kisera na kiseheria
utakaosaidia kuchambua na kuainisha taka zinazotoka katika maeneo mbali mbali
ikiwa ni pamoja na kuwepo mkakati bora wa usimamizi wa taka hizo hapa Zanzibar.
Naye Meya wa Jiji la Zanzibar Mstahiki Mahmoud Mohammed Mussa,
amekiri kwamba taka za hospitali pamoja na kwamba ni hatarishi, lakini
zinaendelea kutupwa katika eneo hilo kutokana na vifaa vya kuchomea taka za
aina hiyo katika Hosptali ya Mnazi mmoja kuharibika mara kwa mara.
Amesema kutokana na changamoto mbali mbali za usimamizi wa
masuala ya taka katika jaa hilo la Kibele, Baraza la Jiji linaendelea na
mazungumzo na muekezaji atakayepewa dhamana ya kusimamia masuala ya taka
ili kupata suluhu ya tatizo hilo hapa Zanzibar.
0 Comments:
Post a Comment