Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman
Masoud Othman, akizungumza na viongozi wa ngazi za mikoa, wilaya na Idara mbali
mbali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kikao chake cha Tathmini ya
Ziara ya Siku mbili katika maeneo ya kimazingira yaliyoathirika na mabadiliko
ya tabianchi na maeneo ya kiafya, kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Kiwanda
cha Makonyo, Wawi Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba,
Makamu wa Kwanza wa
Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman amesema kunahitajika uelewa
mkubwa wa watu wote katika suala la mazingira ambalo ni uhai na linalogusa
sekta zote za uzalishaji na maendeleo nchini.
Othman ameyasema hayo
leo akiongoza Kikao cha Majumuisho ya Ziara yake ya Siku mbili ya kimazingira
na afya kisiwani hapa, kilichofanyika katika Ukumbi wa Kiwanda cha Makonyo,
Wawi Wilaya ya Chake, Mkoa wa Kusini Pemba.
Amesema hakuna nyanja
yoyote ya maisha, sekta ya maendeleo au wizara ya serikali, ambayo kwa namna
moja au nyingine haitoguswa na suala la mazingira, bali kilichozoeleka katika
jamii ni kulichukulia kwa wepesi na mtazamo wa juujuu.
Othman ametoa wito kwa
wadau wote kujumuika katika kuungamkono juhudi za kukabiliana na athari za
mazingira zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, zikiwemo upandaji wa mikoko
na kuepuka ukataji wa miti ya asili kiholela.
“Katika tishio kubwa
ambalo linalotishia mazingira ni ardhi yetu ambayo ni chache, kuvamiwa na maji
ya bahari bali la msingi kwa sasa ni kuweka mikakati na sisi kuiendea bahari
ingawa kwa kufuata miongozo ya kitaalamu”, amesema Makamu wa kwanza wa Rais.
Othman ametoa wito kwa
mamlaka zinazohusika kuweka miongozo, taratibu, kuzingatia haki za wananchi na
mbinu mbadala za kuepusha uharibifu wa makusudi wa mazingira katika maeneo
mbali mbali yakiwemo machimbo ya mawe na mchanga ya Micheweni, Pujini na Shumba
Viamboni, ili kuyafanyia kazi malalamiko na kuepuka visingizio vikiwemo vya
ukosefu wa ajira.
Kabla ya kikao hicho
Othman ametembelea Hospitali ya Vitongoji ‘Cottage’ sambamba na kukagua Bohari
Kuu ya Dawa kisiwani Pemba, ambapo ameeleza matumaini yaliyopo kutokana na
juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na moyo wa kujitolea wa watumishi
mbali mbali wa Wizara ya Afya wakiwemo madaktari, katika kuwapatia wananchi
huduma bora za afya licha ya changamoto nyingi zinazowakabili.
Othman amesema pamoja
na juhudi zote, maendeleo hayatowezekana katika visiwa vya Unguja na Pemba na Tanzania
kwa ujumla, bila ya kuwepo misingi mikubwa ya kuwavutia wawekezaji, ambayo ni
pamoja na amani, utulivu, umoja na mshikamano, bali amewaasa viongozi na
wananchi wote kuielewa dhima ya kuyalinda maridhiano ya kisiasa, chini ya
Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, kwaajili ya mustakabali mwema wa
nchi.
Naye Waziri wa Afya,
Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Mheshimiwa Nassor Ahmed Mazrui,
ameeleza juhudi za makusudi za Serikali kuwapatia wananchi huduma bora za afya
kwa ufanisi ambazo ni pamoja na ujenzi wa Jengo kubwa linalotarajia kuwahudumia
wagonjwa takriban 200 kwa wakati mmoja, katika Hospitali ya Vitongoji, Wilaya
ya Chake Chake Pemba, ambayo maandalizi yake yamekamilika.
Aidha Daktari dhamana
wa Hospitali hiyo, Dokta Sharif Hamad Khatib, ameeleza changamoto kubwa
zinazowabili katika kuwapatia wananchi huduma bora za afya hospitalini hapo,
zikiwemo uhaba wa eneo la kutosha la kuwahudumia wazazi na wajawazito wanaofika
kwaajili ya kujifungua.
Kikao hicho cha
tathmini kimewajumuisha Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Bi Salama Mbarouk
Khatib, Wakuu wa Wilaya zote nne kisiwani hapa, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa
Kwanza wa Rais, Dokta Omar Dadi Shajak, Wakurungezi, Maafisa Wadhamini, Wakuu
wa Idara Maalum za Serikali, Watendaji, Maafisa na Watumishi wa Wizara mbali
mbali za Serikali, Wabunge, Wawakilishi na Viongozi mbali mbali wa kijamii na
vyama vya siasa.
0 Comments:
Post a Comment