watakiwa kuungana kumnyanyua mwanamke

Baadhi ya wanawake walioshiriki mkutano Tumbe Wilaya Micheweni Pemba  wa kampeni dhidi mwanamke kushiriki katika uongozi 

 



PEMBA

 

WANANCHI wametakiwa kushirikiana katika kuwainua mwanamke, ili kuhakikisha wanakuwa viongozi kuanzia ngazi ya jamii hadi Taifa.

 

Akizungumza na wananchi wa shehia ya Tumbe Magharibi, Mkurugenzi wa Jumuiya ya PEGAO Pemba Hafidh Abdi Said alisema, wanawake wao uwezo wa kuongoza na kuleta mabadiliko ya haraka, hivyo ni vyema jamii ikampa mashirikiano katika kuusaka uongozi.

 

Alisema, katika jamii kuna vikundi na Jumuiya mbali mbali zinazoanzishwa kwa ajili ya kuleta maendeleo, ingawa kinachomshangaza ni kuona kuwa wanawake hunyimwa hata nafasi hizo, jambo ambalo sio sahihi kwani wanawafanya waendelee kubaki nyuma kila siku zinaposonga mbele.

 

"Tumekuwa tukiwanyima wanawake nafasi hata hizi za Jumuiya ndogo ndogo tunazoziunda kwenye jamii, sasa tunataka tumuinue mwanamke ili na yeye awe kiongozi kwani wanaweza na wanaleta mabadiliko makubwa", alisema Mkurugenzi huyo.

 

Aidha aliwataka akinababa kuwaunga mkono akinamama wanaotia nia ya kugombea uongozi, kwani kila mmoja anamtegemea mwenzake katika harakati mbali mbali za kijamii, kisiasa na kiuchumi katika kufikia malengo.

 

"Sote tunategeneana katika mambo yetu, hivyo basi tuache kumdharau mwanamke kwamba hawezi wakati huko nyumbani akiamua baba asifanikiwe basi huwezi kufika pahala, kwa hiyo tujue kwamba na wao wana mchango mkubwa", alisema.

 

Akiwasilisha mada katika mkutano huo Mudathir Sharif Khamis alisema, kuwa kila mmoja yuko sawa mbele ya Sheria, hivyo si vyema kumnyima mwanamke kugombea uongozi kwa kisingizio cha kuwa yeye ni mama wa nyumbani.

 

"Akinababa tusiwabane wanawake, wapo viongozi wanawake ambao wanaongoza na wanaleta mabadiliko makubwa katika jamii yetu", alisema Mudathir.

 

Nae muwasilishaji Hadia Sultan Hamad alieleza, kuna baadhi ya wanajamii humkwamisha mwanamke katika kugombea nafasi hizo kwa kisingizio cha dini, jambo ambalo so sahihi kwani zamani walikuwepo wanawake wa kiislamu ambao walikuwa wakisimamia mambo mbali mbali katika jamii zao.

 

"Tuwaelimishe watoto wetu wa kike tangu wakiwa skuli na kuwaelekeza kwamba na wao wanayo haki ya kugombea uongozi, ili watakapofikia muda wasione ajabu na badala yake wawe mstari wa mbele katika hili", alisema.

 

Kwa upande wake Maryam Hemed Said mkaazi wa Tumbe alieleza kuwa, wanawake ambao ni viongozi wameleta mchango mkubwa katika jamii na juhudi mbali mbali zinaonekana katika kuliletea Taifa maendeleo.

 

"Miaka ya hivi karibuni baada ya wanawake kuanza kuwa viongozi imeonekana wametoa mchango mkubwa na juhudi zao zinaonekana kwani wamefanya mambo mengi ambayo hata hao wanaume hawakuyafanya", alifafanua.

 

Akichangia katika mkutano huo Ali Mohamed Bakar alisema kuwa, wanawake wanashindwa kufikia uongozi kutokana na mifumo ya kiutawala iliyopo katika vyama, kwani huwekewa vizingiti vikubwa.

 

"Wakati mwengine utaona kwamba mwanamke anapata nafasi ya pili katika watu tisa waliogombea na wote aghalabu huwa ni wanaume, kwanini tusimpe kipaombele kwa pale kwa ujasiri wake aliouonesha, vyama vibadili mifumo yao na vimpe nafasi mwanamke", alisema.

 

"Unakitumikia chama usiku mchana baadae siku za kugombea anatokea mwenye pesa anawapa watu, hivyo hapa wanawake wengi hushindwa kwa sababu hawana pesa, jambo ambalo linawasababishia kuvunjika moyo, ila nawashauri wasirudi nyuma", alifahamisha.

 

Kwa upande wao wananchi wengine walisema kuwa, kumekuwa na viongozi kwenye majimbo ambao huwashawishi wapiga kura wasimpe mwanamke na kuwabandikiza chuki zisizo na sababu, jambo ambalo linawaumiza sana wanaogombea.

About mmedia

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment