Washauriwa kutoa kipaombele kwa Watu wenye mazingira maalum

 

Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Sada Mkuya Salum

Na Raya Hamad - OMKR                                                                                                  

Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe Dkt Saada Mkuya Salum amezishauri taasisi za Serikali na binafsi zinazotoa huduma kwa jamii kutoa kipaumbele kwa Watu wenye mazingira maalum wakiwemo  wenye Ulemavu wa Uziwi.

 

Dkt Saada ameyasema hayo wakati akiyafungua mafunzo maalum ya lugha ya alama kwa watendaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ZSSF yaliyoaandaliwa na Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu katika ukumbi wa ZSSF Kariakoo.

 

Ameipongeza ZSSF kwa kuwa mfano bora kwa mashirika ya serikali kuonesha kwa vitendo na dhamira njema ya kuwahudumia wananchi wa makundi yote kwa kuanza na lugha ya alama ambayo itawasaidia viziwi kupata huduma wanazozitoa kwa uhakika bila ya gharama ya kutafuta mkalimali.

 

Aidha Dkt Saada ameiomba ZSSF wasiishie hapo bali kutafuta na njia nyengine ya kuwasaidia Watu wenye Ulemavu wa Uoni kwa kuangalia uwezekano wa kutengeneza kadi za ZSSF zenye alama ya nukta nundu.

 

“Naziomba na taasisi za Serikali ili tuwe na jamii shirikishi basi sasa hata vitabu vya sera na sheria na vyenginevyo tuhakikishe tunaandika kwa nukta nundu ili wenzetu wenye Ulemavu wa Uoni nao waweze kusoma maendeleo ya nchi yetu mfano nzuri tulivyoanza Ofisi ya Mkamu wa Kwanza wa Rais Bajeti ya Serikali tuliwazingatia kwa kutoa vitabu vilivyoandikwa kwa kutumia nukta nundu”

 

Kufanya hivyo kutahusisha huduma wanazozitoa kuwa bora zaidi na zinazokwenda na wakati huu wa ukuwaji wa teknologia pamoja na kuziomba taasisi nyengine kujipanga ili ziweze kutoa huduma kwa ufanisi bila ya kuwaacha wengine kama Watu wenye Ulemavu .

 

Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kupitia Baraza la Watu wenye Ulemavu linatambua kuwa fursa mpya ya uchumi wa buluu ni kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wote wa Zanzibar hivyo imejipanga kuandaa mpango mkakati wa kuona lugha ya alama inapewa kipaumbele kufundishwa kwenye taasisi zote zinazotoa huduma kwa jamii.

 

Nae Mkurugenzi wa Baraza la Watu wenye Ulemavu Mhandisi Ussy Khamis Debe amesema mafunzo ya lugha ya alama yameanzishwa baada ya kuonekana kuna upungufu kwa taarifa kwa Watu wenye Ulemavu wa Uziwi.

 

Mhandisi Ussy amesema kati ya changamoto wanazozipata Watu wenye Ulemavu wa uziwi kutopata taarifa sahihi kwa wakati muafaka na ndio maana Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu likaamua kuendelea kutoa elimu hii ya lugha ya alama kwa taasisi tofauti.

 

Mafunzo kama hayo pia hutolewa na Jumuiya ya wakalimani wa lugha ya alama JUWALAZA, Chama cha Viziwi Zanzibar CHAVIZA na chuo cha SUZA, hii ni awamu ya pili ya muendelezo wa mafunzo ya lugha ya alama kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar.

About mmedia

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment