Wazazi na walezi wa watoto wanaosoma katika Shule ya Msingi
Chunya mjini, mkoani Mbeya wamefanikiwa kudhibiti ukatili dhidi ya watoto na
kupelekea utoro kupungua shuleni na kupanda kwa ufaulu.
Hayo yamebainika wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mwanaidi Ali Khamis alipotembelea Shule
ya Msingi Chunya kukagua utendaji wa klabu ya TUSEME iliyoundwa kwa lengo
la kutoa elimu kwa watoto kukabiliana na ukatili wa kimwili, kiakili, kingono
na kisaikolojia kwa watoto.
Akiwasilisha taarifa kwa niaba ya wanachama wa klabu hiyo, mbele
ya Naibu Waziri Mwanaidi Mlezi wa Klabu hiyo mwl. Eliud Dickson amesema Klabu
hiyo imewasaidia wazazi na wanafunzi kupungua kwa vitendo vya ukatili kwa kiasi
kikubwa ikiwemo mimba, vipigo, ubakaji na hakuna wazazi wanaolalamika watoto
wao kufanyiwa ukatili kama ilivyokuwa awali kutokana na elimu inayotolewa.
Ameongeza kuwa Klabu hiyo yenye wanafunzi 100 inahakikisha
mtoto anakua na uwezo wa kusema pale anapofanyiwa vitendo vya ukatili na
wazazi, walezi, walimu na jamii na kupata malezi bora.
Akizungumza na Wanachama wa klabu hiyo, Naibu Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis
ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Chunya kwa kushirikiana na Shirika la
UNICEF kuanzisha klabu hiyo iliyochangia kupungua kwa vitendo vya ukatili
shuleni hapo na jamii nzima ya Chunya.
"Siku zote tunaambiwa malezi siyo baba na mama tu, mtoto
analelewa popote kwenye usalama, hivyo wazazi tuendelee kushirikiana na
Serikali kupitia Wizara ya Afya tutaendelea kushirikiana na Wadau
wanaoshughulika na masuala ya watoto kuhakikisha ulinzi kwa watoto"
amesema Mhe. Mwanaidi.
Akiwa Wilayani Chunya Mwanaidi ametembelea kikundi cha
wanawake wa nguvu waliochangia nguvu zao katika ujenzi wa Kituo cha Afya katika
mji mdogo wa Makongolosi ili kuondoka na changamoto za upatikanaji wa huduma
hiyo.
Aidha, amezungumza na Kamati za ulinzi na usalama wa mama na
mtoto katika kata ya Chalangwa na kuwataka kuzidi kuwaelimisha wananchi
kuripoti vitendo vya ukatili kwa watoto ili Sheria ichukue mkondo wake
kutokomeza vitendo vya ukatili.
Naibu Waziri Mwanaidi anaendelea na ziara yake Mkoani Mbeya kwa
lengo la kukagua shughuli za Maendeleo na kuamsha Ari kwa wananchi kuchangia
nguvu zao katika Maendeleo.
0 Comments:
Post a Comment