Wenye tatizo la afya ya akili ni wenzetu, tusiwanyanyapae


Picha sio halisia


Salum Vuai

 

HUKU tukiwa katika wiki ya maadhimisho ya afya ya akili duniani, jamii inapaswa kutafakari ili kujua kwa kiasi gani inatimiza wajibu wake katika kuwatunza ndugu zetu wanaokabiliwa na tatizo hilo.

 

Kwanza ni lazima tufahamu kwamba maadhimisho hayo yanayofikia kilele Oktoba 10, hayakuanzishwa kuwa ni sherehe ya kujifurahisha, kama inavyofanyika kwenye mambo mengine mathalan siku ya uhuru au ile inayoitwa ya wapendanao (Valentine Day).

 

Bila shaka hii ni siku maalum kwetu kufanya tathmini ya pamoja juu ya changamoto zinazowakabili wenzetu wanaopatwa na fadhaa ya kurukwa na akili hata mara nyengine wakafanya mambo yasiyostahili kutendwa na mtu mwenye akili timamu na tena kadamnasi.

 

Ni vyema jamii ifahamu kwamba kamwe hakuna mtu anayependa kuwa mgonjwa wa afya ya akili, bali yote yanayomkuta ni kwa kudra na mipango ya Mwenyezi Mungu.

 

Katika miaka ya nyuma, watu wengi walijenga tabia mbaya ya kuwachokoza ndugu zetu wenye maradhi hayo huku wakiwapachika majina mengi mabaya.

 

Majina kama vile chizi, kichaa, mwehu, punguwani, mwendawazimu na mfano wa hayo, yalikuwa ndiyo wapewayo jambo ambalo ni unyanyapaa uliokithiri.

 

Kwa kuwa wenzetu hawa ni binadamu, tabaan wanapochokozwa huchokozeka na wengine hawahimili na hivyo huonesha hasira zao kwa kuokota mawe na kuwarushia hao wasiokuwa na utu, imani wala kuthamini haki ya wagonjwa hao.  

 

Lakini ni jambo zuri kwamba kitengo cha afya ya akili katika hospitali ya Kidongochekundu, kimefanya kazi nzuri kutoa elimu kwa jamii ili itambue kuwa hao ni wagonjwa wanaohitaji mapenzi na kutunzwa badala ya kugeuzwa karagosi mitaani.

 

Lolote utakalolifanya dhidi ya mtu mwenye tatizo la afya ya akili ambalo lina namna nyingi tofauti, ni vyema ukumbuke usemi, “Hujafa hujaumbika”.

 

Kwa kuwa hakuna aijuaye kesho yake, ili mradi yuko hai basi lolote linaweza kutokea, na si ajabu kupata maradhi yoyote ikiwemo ya akili kwa namna moja au nyengine ile ijapo isiwe kiasi cha kupiga au kugombana na watu ovyo.

 

Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na hospitali ya Kidongochekundu na Wizara yote ya Afya, bado wapo baadhi ya watu wanaendeleza vitendo vya unyanyapaa kwa wagonjwa wa afya ya akili.

 

Katika tafakuri ya leo, Muhenga ameamua kuwapa elimu watu wanaopenda kuwakebehi ndugu zetu wenye mtindio wa ubongo maarufu sura mfanano kila wanapowakuta mitaani.

 

Yumkini huko ndiko kuonesha mapenzi kwao kwa kuwashirikisha katika baraza na michezo yao, lakini mara nyengine huwageuza watu wa kufurahisha jamii katika njia ya uchale.

 

Inashangaza mara kadhaa utakutana nao mitaani wakiwaimbisha nyimbo na kuwataka wanengue, huku wao wakifurahia kwa kupiga kofi na kuangusha vicheko.

 

Baya zaidi, wanapofanya hayo, huwa wameshughulika kurekodi kwa simu zao kisha kusambaza video hizo katika makundi ya ‘Whatssap’ na marafiki zao mbalimbali.

 

Je, wafanyao haya kwa watoto wa wenzao, wana uhakika gani kwamba nao au jamaa zao hawatakuja kuzaa watoto wenye kasoro za maumbile mbalimbali ikiwemo ya aina hiyo?

 

Hatuombi yatokee, lakini hata wao wenyewe, wanadhani hawawezi kutokezewa na mabadiliko ya kiakili kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuchanganyikiwa kimaisha?

 

Tuelewe kwamba Mwenyezi Mungu ndie muweza wa yote, hivyo kila analolifanya kwa binadamu ni miongoni mwa mitihani yake kwetu ambayo inahitaji subira, imani na mafunzo kwa wengine.

 

Wakati tukiungana na nchi nyengine duniani kuadhimisha siku ya afya ya akili, tukumbuke kwamba sote ni wagonjwa watarajiwa wa maradhi yoyote yale, hivyo tusikufuru kwa kuyaona matatizo ya wenzetu wengine kuwa ni komedi ya kufurahisha nyoyo zetu kwani kwa Mungu hakuna kubwa.

 

Mwisho lakini si kwa umuhimu, Muhenga anachukua fursa hii kuwapongeza madaktari, wauguzi na wataalamu wote katika vitengo vya afya ya akili Unguja na Pemba kwa juhudi zao za kuwashughulikia ndugu zetu wanaopata matatizo hayo.

 

Aidha, kazi kubwa wanayofanya kutoa elimu ili kubadilisha mitazamo hasi iliyomo katika jamii zetu, na kuwezesha kupungua sana vitendo vya kuwanyanyapaa ndugu zetu hao.

 

Kama bado wapo wanaoendeleza unyanyapaa watu wenye tatizo la afya ya akili, ninaamini kwa tafakuri hii watakuwa wamejifunza na nitarajie kutoka sasa nao watakuwa walimu wazuri kwa wengine.

 

SIMU: 0777865050/0714 425556

Baruapepe: salumss@yahoo.co.uk

About mmedia

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment