
Na Haji Nassor,Pemba
KATIBU tawala wilaya ya Mkoani Miza Hassan Faki, amewataka wanawake wasiziogope nafasi mbali mbali ikiwemo za usheha, na pale wanaposhauriwa kutaka kuteuliwa, kwani kiongozi kama akifuata misingi ya sheria na kanuni hakuna kitu kigumu.
Alisema, huu sio wakati kwa wanawake kuendelea kuziogopa nafasi, kwani kila kitu kipo kwa mujibu wa sheria na kanuni, na pindi kiongozi akizifuata hizo ataongoza pasi na kuvunja maadili.
Katibu huyo tawala aliyasema hayo, wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi, juu sababu za wanawake kutoonekana kwenya nafasi mbali mbali za uongozi.
Alisema kuwa, wapo baadhi ya wanawake na inawezekana kwa kule kutopata elimu ya ujasiri, wamekuwa wakiziogpa baadhi na fasi kama vile za usheha, na ndio sababu ya kutoonekana wengi kwenye nafasi hizo.
Akito mfano Katibu tawala huyo alieleza, ipo moja ya shehia ndani ya wilaya ya Mkoani walitamani kumteua mwanamke, ingawa pamoja na ujasiri wake, alikataa nafasi ya usheha.
“Sisi ipo shehia ndani ya wilaya ya hii, tulimuona mwanamke anaweza kuendesha nafasi hiyo, lakini tulipomshauri ashike nafasi hiyo, aliogopa,’’alieleza.
Katika hatua nyingine Katibu tawala huyo, amesema lazima wanawake wakumbuke kuwa katiba na sheria zinawapa uhuru wa kuwa viongozi.
“Wanawake ni jeshi kubwa katika taifa hili, sasa lazima waelewa kuwa pia wanapaswa kuonekana kwenye nafasi mbali mbali za uongozi iwe usheha, ukuu wa wilaya na nyinginenezo,’’alifafanua.
Mratibu wa TAMWA –Pemba Fat-hya Mussa Said, alisema wamekuwa na mradi maalum wa kuwawezesha wanawake kudai haki zao za kisiasa, kiuchumi na uongozi ‘SWIL’ ili kuna wanawake hawachwi nyuma.
Kwa upande wake Mratibu wa mradi huo Salma Amir Lusangi, alisema kundi la wanaume ambalo ndio linalosimamia sheria, hawajaona umuhimu wa kuwapa nafasi wanawake.
“Hata ikitokezea mwanamke anagombea, basi figisu figisu huanzia kwa wanaume na kisha kutumwa wanawake, ili kuona mwanamke hasimami, hili sio sahihi,’’alieleza.
Mkuu wa Mkoa wa kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib, alisema sheria zisizo rafiki leo hii ambazo zinawanyima haki wanawake zilipitishwa kwa miaka kadhaa na wanaume.
“Ukiona leo hii nafasi za kitaifa kama za Mwenyekiti na Katibu kwenye vyama vya siasa zinaendelea kushikwa na wanaume, inatokana na kuwepo sheria na kanuni zinazowakosesha haki wanaume,’’alieleza.
Sheha wa shehia ya Chole wilaya ya Mkoani Batini Sharif Nassor, alisema changmoto nyingine kubwa ni baadhi ya wanaume kutowaamini wake zao katika nafasi za uongozi.
“Inawezekana mwanamke anataka kupewa nafasi, lakini kwa vile yuko kwenye ndoa basi mwanamme bila ya sababu za msingi anamzuia mke wake au kumtishia talaka na kushindwa kupata nafasi husika,’’alifafanua.
Kisiwa cha Pemba chenye masheha 101, kwa wilaya zote nne za Micheweni, Wete, Mkoani na Chake chake wanawake ni 28 pekee, ikilinganishwa na masheha wanaume 73.
0 Comments:
Post a Comment