Sheha mteule Mwanamke ashidwa kuapa akihofia ushirikina Pemba

Muonekano wa mandhari ya mji wa Chakecheke Mkoa wa kusini Pemba.


Na Haji Nassor 

MWANAMKE mmoja mkaazi wa shehia ya Ngwachani wilaya ya Mkoani Pemba, aliyeteuliwa kushika nafasi ya usheha Augosti 20 mwaka huu, ameachia ngazi siku nne kabla ya kula kiapo, akihofia vitendo vya ushirikina.

Mwanamke huyo Kaije Faki Mjaka, alisema kuachia kwake ngazi nafasi hiyo, hakutokani na amri ya mume wake, kama baadhi ya watu wanavyodai, bali ni hofu ya kufanyiwa vitendo vya ushirikiana.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mwanamke huyo alisema, amekuwa akiwindwa windwa kwa muda mrefu na badhi ya wanaume, hasa katika siku za hivi karibuni, baada ya kuwepo taarifa kuwa, huwenda akateuliwa nafasi hiyo.

Alisema, amekuwa akiona mambo ya maajabu kwenye nyumba yake, ikiwemo mayai yalioandakiwa maandishi ya lugha ya kiarabu.

Alieleza kuwa, hata anapokuwa katika hali ya kawaida, wapo wanomtahadharisha kuwa asijaribu kuikubali nafasi hiyo, jambo ambalo linamkosesha amani katika shughuli zake za kila siku.

Mwanamke huyo alisema hata, usiku wa Augsti 20, mwaka huu baada ya kuteuliwa, alifikiwa na mwanamke mmoja asiyemfahamu, akiomba hifadhi, jambo ambalo lilimtia wasi wasi.

“Nilishangaa alikuja mwanamke kwangu majira ya saa 5:00 usiku, eti mimi ni sheha anataka hifadhi alikosa gari, na alipofikia nilipata wasi wasi wa wa roho, maana hata maelezo yake hakuyanyaoosha,”alieleza.

Aidha alisema kuwa, hapo aliamua kuwaamsha baadhi ya watu na kisha kwa vile hakuwa na lugha yenye kufahamika mwanamke huyo, alimuacha na kuchukuliwa na watu wengine.

“Wapo walioniambia kuwa nimshukuru Mwenyezi Muungu kwa yule mtu aliyejifanya amepotea, kutomkaribisha ndani mwangu, maana engefanya jambo kubwa,’’alieleza.

Aidha mwanamke huyo alisema, jengine ambalo limemtia hofu kushika nafasi hiyo, ni kuwepo wale watu wake wa karibu aliyotarajia kumsaidia, kuanza kumpa maneno yasiyo ya kawaida.

“Mmoja ameninuna bila ya sababu, mmoja kanikatia jicho, wengine wananipa maneno ya yasioashiria amani juu yangu, ndio maana nilikakataa kula kiapo,’’alieleza.

Hata hivyo alisema, ataendelea kutoa ushirikiano wa karibu na sheha mpya aliyekwishateuliwa, ili kufikia maendeleo kamili ya shehi yao na serikali kwa ujumla.

Baadhi majirani wanaomfahamu mwanamke huyo na kukataa kutaja majina yao, walisema amekuwa akiingia kwenye majaribio mengi na ya hatari juu ya vitendo vya ushirikiana.

“Hata kwenye harakati za uchaguzi uliomalizika, mwanamke huyo kwa vile ni mpigania demokrasia, alionekana kama adui ingawa alikuwa anatimiza wajibu wake,’’alisema.

Walisema, ni kweli kuachia kwake ushehe huo hakutokani na sababu yoyote, bali ni hofu ya kufanyiwa vitendo vya ushirikiana, ambao kwake amekuwa wakiingizwa kwenye majaribu kila baada ya muda.

Katibu tawala wilaya ya Mkoani Miza Hassan Faki, alikiri kutokea kwa kadhia hiyo, na kusema hakuachia kwa sababu za kisasa wala amri ya muume, bali ni hofu yake binafsi.

“Mimi baada ya kuskia kwa huwenda asishiriki kwenye kula kiapo siku moja kabla, nilimfuata na wakati namuhoji, inaonesha ana jambo, linalomkwaza na sio agizo la muume,’’alifafanua.

Hata hivyo alisema, kumteua mwanamke huyo, ilikuwa ni miongoni mwa azma ya kuhakikisha wanawake wanakuwemo kwenye vyombo vya maamuzi.

Sheha mpya wa shehia Ngwachani Issa Is-mail Juma, alisema anajua kuwa, aliipata nafasi hiyo, baada ya aliyeteuliwa awali kuicha kwa sababu zake binfasi.

“Mimi kwa kweli sijui sababu zipi mwenzangu zilizompelekea kuaichia nafasi hiyo, maana mimi baada ya kuteuliwa niliapishwa na sasa ndio naongoza shehia hii,’’alieleza.

Mratibu wa Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA-Zanzibar kisiwani Pemba, Fat-hya Mussa Said, amesikitishwa na taarifa hiyo.

Alisema, ndio maana TAMWA –Zanzibar imekuwa ikitafuta miradi kadhaa ya kuwajengea uwezo wanawake kashiriki katika uongozi, ingawa sasa kumeibuka aina mpya ya vikawazo vya ushirikiana.

“Huyu ni mmoja, lakini hata kwenye changuzi zetu za vyama vingi, kwenye kuomba nafasi ndani ya vyama wanawake wanazungukwa na tishio la ushirikiana, ‘’alieleza.

Mwanaharakati wa haki wanawake na watoto Pemba Tatu Abdalla Msellem, alisema hilo ni jambo zito na linalowezekana kutokea, na ndio maana mwanamke huyo aliamua kusalimu amri.

Augosti 20, mwaka huu Mkuu wa Mkoa wa kusini Pemba Mattar Zahor Massoud alifanya uteuzi wa masheha 15 katika shehia mbali mbali wakiwemo wanawake wawili mmoja huyo aliyeachia ngazi na mwengine ni sheha wa shehia ya Tibirini.

About mmedia

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment