NA ZUHURA JUMA, PEMBA
WAFANYABIASHARA
kisiwani Pemba wamemshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi kwa
kauli yake aliyoitoa ya kujengwa bandari ya kisasa Mkoani Pemba, ambayo
itasaidia meli za mizigo kufika moja kwa moja.
Hivi karibuni Dk:
Mwinyi alikuwa na ziara ya siku nne kisiwani Pemba, ambapo alitembelea miradi
mbali mbali pamoja kuzungumza na wananchi wa mikoa wilaya nne kusikiliza kero
zao.
Katika ziara yake hiyo
Dk Mwinyi aliwashukuru wananchi kwa kumchagua kuiongoza Zanzibar ambapo aliwaahidi
wananchi kuwatekelezea mambo mbali mbali, ili kuhakikisha nchi inapata
maendeleo endelevu.
Wakizungumza na
waandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti wafanyabiashara hao walisema kuwa,
wamefarijika sana kusikia kauli hiyo ya raisi kutaka kujenga bandari, kwani
wanaamini gharama za bidhaa zitapungua kwa kiasi kikubwa.
Walisema kuwa, bidhaa
zinapofika kisiwani Pemba zinakuwa ghali sana hali ambayo inasababisha wananchi
kushindwa kununua na hatimae kukaa muda mrefu bila kupata wateja.
Walisema kuwa, ikiwa itajengwa
bandari ya kisasa, itasaidia meli za mizigo kuja moja kwa moja kisiwani Pemba,
hivyo wanaamini kwamba bei ya bidhaa itashuka na kuwapa wafanyabiashara na
wananchi ahuweni.
“Bidhaa tunachukua
Dar-es-Salaam au Unguja, kwa hiyo tunapofika Pemba bei lazima iwe kubwa kwa
sababu kila tunapopita tunalipia mzigo na ukiangalia pia tunatakiwa tulipe
kodi, hivyo lazima tuongeze bei ili na sisi tujilipe gharama zetu”, walisema
wafanyabiashara hao.
Mfanyabiashara wa kanga
na madira Chake Chake Mbarouk Mohamed Zahor alisema, kauli ya dk: Mwinyi kutaka
kujenga bandari Mkoani Pemba ni nzuri na anaifagilia sana, kwani anaamini
watapata maendeleo mazuri kwao na wananchi kama walivyo wenzao wa nje ya kisiwa
hiki.
Alisema kuwa, wanaiunga
mkono kauli hiyo kwa asilimia mia kutokana na kuwa itawasaidia sana kupungua
kwa gharama za usafirishaji na wananchi watafaidi kwa bei kupungua.
“Biashara kwa Pemba
muda mwingi ni ngumu, lakini hii inasababishwa na kuwa bei ni kubwa na pia
mizigo huchelewa kupatikana, hivyo ikiwa itajengwa bandari ya kisasa na mizigo
kuja Pemba itakuwa ni chachu ya maendeleo yetu kwa kweli”, alisema baba huyo.
Kwa upande wake
mfanyabiasha wa nguo za watoto Maulid Ali Kassim alisema, wamefarajika sana
walipomsika rais kuhusu kutaka kuijenga bandari, kwani ushuru utapungua kwa
kiasi fulani ukilinganisha na wanapochukua nje ya Pemba.
“Ushuru ukipungua na
bei zitapungua, hivyo itakuwa ni rahisi kwa wananchi kununua bidhaa zetu, kwa
sababu tukinunua kitu shilingi elfu 15,000 huku kinaweza kufika hata shilingi
20,000, hivyo tunawaumiza wananchi hasa wa
kipato cha chini”, alisema.
Maulid alieleza kuwa,
kwa sasa biashara ipo vizuri kiasi kutokana na kuwa ni msimu wa karafu, hivyo
angalau watu wanapata pesa za kujikimu, lakini utakapomalizika msimu tu biashara
huwa ni ngumu sana kwa sababu bei ni ghali sana.
Nae mfanyabiashara wa
vitambaa Yussuf Abrahman Mohamed alieleza kuwa, kauli ya dk Mwinyi ni nzuri
sana na wanaiunga mkono na kuiomba Serikali kuharakisha kuijenga bandari hiyo, ili
kuwasaidia katika shughuli zao za kibiashara.
“Tutapata mafanikio
makubwa ikiwa bandari itajengwa ya kisasa na itakuwa ni jambo la busara sana,
kwa sababu kila tunapopita lazima tulipie mzigo, hivyo inatugharimu sana na
ndio maana bei zinakuwa kubwa”, alisema.
Alimshukuru dk Mwinyi
kwa kauli yake hiyo, kwani ni kilio chao cha muda mrefu, hivyo ipo haja ya
kuharakishwa jambo hilo, ili kuleta manufaa kwa wafanyabiashara na wananchi kwa
ujumla.
Mfanyabiashara ambae
hakutaka jina lake litajwe alisema kuwa, wanataka wauze bidhaa kwa bei ndogo kama
wenzao wa Unguja na Dar-es-Salaam, lakini wanashindwa kutokana na kuwa
wanatumia gharama nyingi kusafirisha hadi kufikia Pemba.
“Wananchi hawatuamini
kama tunatumia gharama kubwa mno kuleta bidhaa Pemba na ndio maana wanapokuja
madukani wanalalamikia bei kubwa, ila naamini kutokana na kauli ya Dk Mwinyi
watafaidika hivi karibuni, kwani bidhaa zitakuwa bei rahisi”, alisema dada
huyo.
Mfanabishara Ali Omar
Juma amesema kauli iliyotolea na rais kuhusu kujengwa badari itakayoweza
kuegesha meli za mizigo kutoka moja kwa moja nchi za nje ni zuri kwao kwani
itaweza kuwapunguzia gharama za bidhaa.
“Iwapo bidhaa zitakuja
moja kwa moja gharama zitakuwa nafuu, meli zote huishia Unguja ambapo hupata
gharama kubwa za usafirishaji na kuweza kusababisha kupata gharama kubwa mteja
wa mwisho”, alisema.
Alieleza kuwa, anazidi
kumuombea rais azidi kuwa na moyo wa kuwasaidia ili waweze kundokana na
changamoto zinazowakabili kwenye biashara zao.

0 Comments:
Post a Comment