Serikali imekabidhi kwa
Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza eneo lenye ukubwa wa Hekta 6,000 lililotolewa
kwa wananchi wa vijiji vya Mpeta na Chakuru ili ligawiwe kwa wananchi hao kwa
ajili ya shughuli za ufugaji baada ya mgogoro wa muda mrefu wa wananchi hao kuvamia
Hifadhi ya Ranchi ya Taifa ya Malai iliyopo Mkoani Kigoma.
Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amekabidhi eneo hilo (23.09.2021), akitekeleza agizo
la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye
ameamua eneo hilo kumegwa kutoka Hifadhi ya Ranchi ya Taifa ya Malai baada ya
kusikia kilio cha wafugaji hao kutoka mikoa ya kanda ya ziwa kutokuwa na maeneo
kwa ajili ya mifugo yao.
Waziri Ndaki amebainisha
kuwa hatua hiyo inakuja kukiwa na mgogoro mkubwa baina ya wananchi hao ambao ni
wafugaji, Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO)
ambapo wananchi zaidi ya 5,900 wamevamia eneo la ranchi hiyo kitongoji cha
Mwanduhu Bantu kijiji cha Mpeta na eneo la Kazaroho Wilaya ya Uvinza na
kuendesha shughuli za ufugaji na kilimo.
Kabla ya hatua ya
kukabidhi eneo hilo serikali kupitia Wizara za Kilimo na Mifugo na Uvuvi,
watendaji wa Halmashauri za Wilaya za Uvinza na Kasulu kutoka Idara za Ardhi,
Kilimo na Mifugo ambao walifanya sensa ya kujua idadi ya wavamizi hao kupima
eneo ambalo litaweza kutumika kwa wananchi, kuchora ramani upya na kugawa eneo
kuondoa mgogoro huo mchakato uliochukua miezi miwili kukamilika.
Waziri Ndaki amesema
awali Rais Samia alishauriwa kutoa Hekta 4,000 lakini baada ya kufanywa kwa
sensa ya watu na mifugo aliamua kutoa Hekta 6,000 ili ziweze kutumiwa na
wananchi hao.
“Baada ya Rais Samia
Suluhu Hassan kutoa eneo hili naomba kutangaza kuwa serikali haitaongeza eneo
lingine na mgawanyo utafanywa kwa watu zaidi ya 5,900 waliokuwa wakihusika na
mgogoro na kwamba watakaovamia eneo la ranchi ambalo siyo eneo lililomegwa na
kugawiwa sheria itachukua mkondo wake.” Amesema Waziri Ndaki
Akitoa taarifa kwa
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa
(NARCO), Prof. Peter Msoffe amesema mchakato umefanyika kwa kuwa na vikao zaidi
ya vitano na viongozi na wananchi waliovamia eneo hilo ambapo changamoto
mbalimbali zilijitokeza.
Prof. Msoffe amesema
licha ya mapendekezo na ushauri uliokuwa ukitolewa na wataalam wananchi hao pia
walikuwa na mapendekezo, ushauri na maamuzi ambayo wakati mwingine yaliegemea
kwenye baadhi ya makundi kuona yananufaika zaidi hivyo maamuzi mengi kuwa na
changamoto ya kufikia mwisho kwa faida ya wote.
“Kwa sasa kumekuwa na
idadi kubwa sana ya watu na mifugo na hiyo inatokana na ongezeko kubwa la
wavamizi hao ambapo baada ya kusikia kumeanza mchakato wa sensa na upimaji
baadhi ya watu waliongezeka ambao hapo awali hawakuwepo kwenye eneo hilo na
wengine wameingia kwenye eneo ambalo hapo awali halikuwa kwenye mgogoro na
kuanza kudai waongezewe eneo.” Alisema Mkurugenzi huyo wa NARCO.
Ameongeza kuwa eneo hilo
la Hekta 6,000 limegawanywa kwa Hekta 2,500 kutoa kitongoji cha Kazaroho kijiji
cha Mpeta na Hekta 3500 kitongoji cha Mwanduhu Bantu kijiji cha Mpeta wilaya ya
Uvinza.
Naye Mkuu wa Wilaya
Uvinza, Mhe. Anafi Msabaha akizungumza katika mkutano huo amesema mgogoro huo
umefikia mwisho kwa maamuzi ya Rais kutoa eneo ambalo litatumiwa na wananchi
waliokuwa kwenye mgororo na kwamba wilaya itasimamia kuona taratibu za ugawaji
zinafanyika kwa uwazi na wananchi ambao ni wafugaji waliohusika wanapatiwa
maeneo kulingana na mgawanyo utakaofanyika.
Baadhi ya wananchi
walioongea baada ya taarifa ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki
kuhusu kutolewa kwa eneo hilo wameishukuru serikali kwa kukubali kuwamegea eneo
hilo, huku wakidai bado eneo walilopewa haliwezi kutosheleza mahitaji na kuomba
waongezewe maeneo zaidi.
Mmoja wa wananchi hao
Bw. Masele Mayenga amesema eneo lililotolewa linaweza kutumika kupatia ufumbuzi
wa mgogoro uliokuwepo ambapo wafugaji walikuwa wakisumbuliwa na kuondolewa eneo
la Ranchi kwa kuvamia eneo hilo ambapo amesema kuwa bado eneo walilopewa
haitoshelezi mahitaji yao.
0 Comments:
Post a Comment