Mkurugenzi Taasisi
ya Utafiti wa Afya Zanzibar Dkt. Mayasa Salim Ali akizungumza machache na
kuwakaribisha wajumbe katika uzinduzi wa mradi wa kuongezea thamani tiba asili,
hafla iliyofanyika Ukumbi wa Mkutano Wizara ya Afya Mnazimmoja Zanzibar.
Na Sabiha Khamis Maelezo
Taasisi ya Utafiti wa Afya Zanzibar (ZAHRI) imetakiwa kuendeleza
kufanya utafiti wa dawa za asili ili zitumike kwa usahihi katika kutibu maradhi
yasiyoambukiza.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Uongezaji wa Thamani
Tiba za Mimea ya asili katika kutibu maradhi yasiyoambukiza ofisini kwake
Mnazi Moja, Mkurugenzi Tiba kutoka Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee,
Jinsia na Watoto, Dk. Amour Suleiman Mohamed, amesema tafiti zinazofanywa
zitawasaidia wanajamii kutibu maradhi ya yasioambukiza kwa usahihi na kuepuka
kubahatisha.
Alisema kuwa, idadi kubwa ya wanajamii hutumia dawa za
asili bila kuwa na elimu na kipimo sahihi jambo ambalo husababisha madhara
makubwa kwa afya zao.
Alisema ili kuiepusha jamii na madhara hayo, ipo haja ya kutoa
elimu juu ya viwango na matumizi sahihi ya dawa hizo ili kuleta matoke chanya
ya dawa zinazotumiwa.
“Jamii hutumia dawa asili za mimea bila kiwango, kupitia tafiti
hizi zitasaidia kugundua maradhi na kutumia tiba kwa kiwango kinachotakikana
ili kuwasaidia wazee wetu majumbani kuweza kutumia dawa kwa usahihi
kulingana na majibu sahihi yanayotolewa na tafiti ili kuleta tija” alisema Dk
Amour.
Alifahamisha kuwa, dunia ilipokumbwa na janga la Uviko 19 ambayo
ni maradhi yanayoambukiza, tiba asili zilisaidia katika kupambana na janga
hilo, hivyo ni vyema kuongeza jitihada katika kuzipa thamani dawa hizo za
mimea na kuzitumia kama zinavyotumika katika nchini nyengine.
Kwa upande wake, Mwenyekiti Baraza la Tiba Asili Prof. Hamis
Malebo amesema jamii inapaswa kupewa elimu kuhusiana na kuhifadhi na kutunza
rasilimali ya mimea dawa, kwani inamchango mkubwa katika kuimarisha sekta
ya afya nchini.
Vile vile ameipongeza Taasisi ya Utafiti wa Afya Zanzibar, kwa
kuchukua fursa hii muhimu ya kuanzisha mradi huu utakaosaidia kuonesha thamani
ya dawa asili zinazotokana na mimea.
0 Comments:
Post a Comment