Salama Haridhishwi na kiwanja cha Mpira Kishindeni

 

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib akizungumza katika Ziara yakeWizara ya Habari, Vijana, Sanaa na Mchezo na Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale kwa Mkoa wa Kaskazini Pemba

MKUU wa Mkoa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib amesema, hakuridhika na mradi wa kiwanja cha mpira Kishindeni Wilaya ya Micheweni kutokana na matumizi ya fedha iliyotumika kutokuwa  sahihi.

Alisema kuwa, kiwanja hicho kimegharimu fedha taslimu shilingi milioni 236, ingawa haziendani na matumizi hayo, jambo ambalo lilimuhuzunisha sana, kwani fedha zinazotumika kufanyia miradi ya kimaendeleo ni kodi za wananchi.

Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo kwa Wizara ya Habari, Vijana, Sanaa na Mchezo na Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale kwa Mkoa wa Kaskazini Pemba alisema, hatokuwa tayari kuona fedha za miradi hazitumiwi ipasavyo.

Alisema kuwa, fedha ambazo zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikiwa hazikutumika kwa mujibu wa utaratibu huathiri sana, hivyo aliwataka wasimamizi kuwa makini na wawe na tabia ya kuelekezana na kushauriana, ili fedha zitumike kwa usahihi.

“Fedha zilizotumika kujengea uwanja huu haziendani kabisa na hadhi ya kiwanja kilivyo, ipo haja kwa wote wanaohusika kusimamia ipasavyo miradi inayowafikia na fedha zitumike kama ilivyokusudiwa”, alisema Mkuu huyo.

Aidha Mkuu huyo alisema, awali alielekeza kwamba katika kiwanja hicho kujengwe sehemu za kukalia watu wanaokwenda kuangalia michezo  sambamba na kupandwa miti ya kivuli, ingawa yote hayo hayakufanyika.

“Lengo letu ni kuimarisha vijana kwa kuonesha na kukuza vipaji vyao, hii itasaidia kuzalisha ajira miongozi mwa ajira laki tatu zinazotakiwa kutoka katika sekta rasmi na zisizo rasmi”, alieleza.

Alieleza kuwa, kwa sasa ipo haja ya kuandaa makundi madogo madogo ili yaweze kucheza ligi ndogo ndogo sambamba na kuweka kiwango japo kidogo cha fedha ambacho watapewa washindi, jambo ambalo litasaidia kuamsha ari kwa vijana hao katika sekta ya michezo.

“Kiwanja kimetengenezwa kwa fedha nyingi, hivyo tuwaandae vijana wakitumie ili tuone kwamba kinaleta faida kubwa katika mkoa wetu”, alieleza.

Mapema Ofisa Mdhamini Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Salum Ubwa Nassor alisema, Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015/2020 iliahidi kujenga viwanja vya michezo kisiwani Pemba kwa lengo la kuisaidia kuimarisha miundombinu ya viwanja na kupewa fursa ya michezo mbali mbali kuanzia ngazi ya shehia, Wilaya na Mkoa.

Alisema kuwa, taarifa ya utekelezaji katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa viwanja viwili vya Wilaya, ambapo kwa Pemba wamefanikiwa kujenga Kishindeni Wilaya ya Micheweni na Kangani Wilaya ya Mkoani.

“Viwanja hivi vimejengwa na mkandarasi wa ndani na kwa hatua ya awali vimeshakamilika kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba na kukabidhiwa kwa wakuu wa Wilaya husika na viko tayari kutumika kwa wananchi”, alisema Mdhamini huyo.

Akizungumzia changamoto katika uwanja huo alisema, eneo lipo kwenye makaazi ya watu kidogo jambo ambalo linakosa kutumiwa ipasavyo, hivyo ipo haja kwa wakuu wa Wilaya kuwahamasisha vijana kwenda kuutumia sambamba na Wizara kuihamasisha ZFA kuutumia.

“Changamoto nyengine ni kukosekana kwa miundombinu ya kuingilia uwanjani ambayo ipo nje ya uwezo wetu, wakati wa mvua huwa panajaa maji na watu kushindwa kufika”, alieleza.

Nae Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Mgeni Khatib Yahya alisema kuwa watachukua juhudi mbali mbali kuhakikisha vijana wanakitumia kiwanja hicho kwa maslahi yao na Taifa kwa ujumla.

Ziara hiyo ya siku moja ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib walikagua miradi mbali mbali ya kimaendeleo na kuwataka wasimamizi wa miradi hiyo kutumia fedha hizo kama inavyotakiwa.

About mmedia

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment