Na Salum Vuai
svuai@marhabanews.net
WAKATI dunia ikiadhimisha Siku ya Wazee kimataifa leo Oktoba 1, 2021, wazee visiwani Zanzibar wamepaza sauti zao wakidai kusahauliwa katika fedha zinazotolewa na serikali kwa makundi maalum.
Mratibu wa miradi katika Jumuiya ya Wastaafu na Wazee Zanzibar Bi. Ghanima Othman Juma, amesema Wizara ya Nchi (OR) Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, kila robo mwaka hutoa asilimia kumi ya mapato yake kwa makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Akizungumza katika warsha ya siku moja iliyofanyika Kidongo chekundu kuzungumzia changamoto za wazee kuelekea maadhimisho ya siku yao, Ghanima alisema katika mgao huo, makundi ya wanawake na vijana hupewa asilimia nne kila moja, huku watu wenye ulemavu wakipata asilimia mbili ya fedha hizo, lakini wazee hawamo katika wanufaika wa ruzuku hiyo.
Pamoja na kulilia haki ya wazee, Mratibu huyo alieleza kushangazwa kwake na asilimia ndogo wanayopewa watu wenye ulemavu tofauti na vijana ambao alisema, kimsingi wana nguvu na uwezo wa kufanya shughuli mbalimbali za kuwaingizia kipato.
“Tunaelewa kuwa serikali yetu inafanya juhudi kubwa kujenga ustawi wetu ikiwemo kutoa posho ya shilingi 20,000 kila mwezi kwa wazee waliotimiza miaka 70, lakini katika hili la Wizara ya Tawala za Mikoa, tunasikitika kuwekwa kando,” alieleza.
Alifahamisha kuwa, wazee wana changamoto nyingi zinazohitaji kuangaliwa kwa jicho la tatu ili wapate faraja kutokana na kupungukiwa nguvu na uwezo wa kujituma, ikizingatiwa walitumia ujana wao kujenga nchi na kuatika mbegu njema ambapo matunda yake yanakinufaisha kizazi cha sasa.
Aidha, aliiomba serikali kuwahimiza madaktari hospitalini na katika vituo vya afya, kuwapa wazee kipaumbele cha kwanza kwa kuwafanyia uchunguzi wa kina wanapokwenda kufuata matibabu ili kubaini matatizo ya kiafya waliyonayo na kuwapatia tiba sahihi na za uhakika.
“Mara nyengine mzee anakuwa na maradhi ambayo hawezi kuyatambua zaidi ya kujiona anaumwa kichwa na mgongo akidhani ni kawaida na kutaka panadoli tu. Hawa wanapaswa kuangaliwa vizuri kwani huenda kuna mambo yaliyojificha,” alieleza Ghanima.
Mratibu huyo pia alivitaka vyombo vya habari kutoa nafasi kubwa katika vipindi vyao kuwaendea wazee na kutangaza mambo yanayowahusu, badala ya mara nyingi kuweka burudani na vipindi vinavyowahusu vijana pekee.
Aidha alisisitiza umuhimu wa vijana kuwatunza wazee na kutengeneza sheria zinazowahusu kwani watakapoondoka zitawafaa wao kwa kuwa nao wanaelekea huko akisema uzee haukwepeki.
Mapema, akiwasilisha mada katika warsha hiyo, Ofisa kutoka Idara ya Wazee katika Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Dk. Salum Rashid Mohammed, alisema bajeti kubwa ya idara inakwenda katika kuhudumia wazee ili kuimarisha ustawi wao na kuwaondoshea unyonge.
Hata hivyo, alisema upatikanaji wa fedha hizo hutegemea uwezo wa serikali, kwani mara nyengine, kiwango kinachoombwa huwa hakifikii makadirio wanayopendekeza.
Kwa upande mwengine, ofisa huyo alisema umefika wakati serikali ifikirie kuunda sheria ya kutenga nafasi za uwakilishi wa wazee katika vyombo vya maamuzi na mabaraza ya kutunga sheria ili kuwasilisha maoni yao kama ilivyo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
“Yumkini mtu akadai kuwa wapo wawakilishi, wabunge na madiwani waliofikia umri wa uzee, lakini suala la kuangalia hapa ni je, wanamuwakilisha nani? Uwakilishi kama huu hauakisi haja ya kuwepo nafasi maalum za wazee,” alifafanua.
Meneja miradi wa kitengo cha kinga jamii kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wazee (Help age) Jerome Sam Demwaya, alisema lengo la warsha hiyo ni kuwashajiisha waandishi wa habari kufuatilia na kuripoti taarifa na changamoto zinazowakumba wazee.
Alisema waandishi wana mchango mkubwa katika kuinua uelewa wa jamii juu ya mambo mbalimbali ikiwemo namna bora ya kuyapatia ufumbuzi matatizo yanayowakabili watu wa kundi hilo.
Aliahidi kuandaa utaratibu wa kuyafanyia kazi maazimio yaliyofikiwa kwenye warsha hiyo, ikiwemo kuanzisha mtandao utakaowaunganisha waandishi na mamlaka zinazoratibu mambo ya wazee, ili kuhakikisha malengo yao yanafikiwa kikamilifu.
Siku ya wazee duniani huadhimishwa Oktoba mosi ya kila mwaka, ambapo hapa Zanzibar yamepangwa kufanyika katika kijiji cha Kitope Wilaya ya Kaskazini ‘B’, kwa matukio mbalimbali ikiwemo kutolewa chanjo ya kinga ya UVIKO 19 kwa wazee na wananchi wengine.
0 Comments:
Post a Comment