Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, ametoa wito kwa watu wenye ulemavu kuhamasisha maridhiano ya kisiasa na ya kijamii, ili kujenga amani ya kweli katika nchi.
Othman ameeleza hayo
leo ofisini kwake Migombani Mjini Unguja, alipokutana na Ujumbe wa Shirikisho
la Jumuiya za Watu wenye Ulemavu Zanzibar (SHIJUWAZA) uliofika kujitambulisha
na kujadili changamoto zinazowakabili.
Amesema kuwa maridhiano
ni mtaji na raslimali muhimu inayopelekea kupatikana kwa amani, na endapo
yakitoweka nchi haiwezi kuimarika, na hatimaye huleta machafuko yanayoweza
kuongeza kasi ya mahitaji maalum na hata ongezeko la watu wenye ulemavu.
“Hapa ninapenda niwape
changamoto kidogo kama ilivyo kwa jumuiya nyingine, mkahamasishe maridhiano
yatakayopelekea ujenzi wa amani ya kweli kama ajenda muhimu, kwani yakija
machafuko siyo tu yatawaathiri watu wenye ulemavu, bali yataongeza hata huo
ulemavu wenyewe”, amesisitiza Mhe. Othman.
Othman amebainisha
zaidi mambo yanayochangia wimbi la ulemavu, ambayo ni pamoja na ongezeko la
maradhi yasiyoambukiza, dawa za kulevya, na makosa ya uzembe wa usalama
barabarani.
Kwa upande wao viongozi
wa SHIJUWAZA, Makamu Mwenyekiti na Mratib, Bw. Ali Omar Makame na Bakar Omar
Othman, wameeleza kuwa, uwepo wa Shirikisho hilo ni juhudi za makusudi za
kupigania haki, fursa na kuwajengea uwezo watu wenye ulemavu, ili kuimarisha
ustawi bora wa jamii katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Viongozi hao
wamezishukuru Serikali zote mbili, ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na ya
Zanzibar, kutokana na kuungamkono juhudi za kuwakomboa watu wenye ulemavu
nchini, licha ya changamoto nyingi zinazowakabili zikiwemo za udhalilishaji na
ugumu wa maisha.
Kikao hicho
kiliwajumuisha viongozi mbali mbali pamoja na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa
Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Dkt Omar Dadi Shajak, ambaye amebainisha juhudi
zinazochukuliwa na Wizara husika za pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, katika kutekeleza azma ya ushiriki unaostahiki wa mikutano ya kitaifa
na kimataifa, inayowajumuisha watu wenye ulemavu.
Wakati huo huo, Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe Othman Masoud Othman, amekutana na Uongozi
wa Taasisi ya Kuwasaidia Vijana kupata Fursa za Masomo Nje ya Nchi (STUDY-
ABROAD) na kushukuru juhudi muhimu wanazozichukua katika uwezeshaji wa
kitaalamu kwa vijana, na kwa maslahi ya maendeleo ya nchi.
Mhe, Othman amesema kuwa
ubunifu uliotekelezwa na taasisi hiyo ni hatua muhimu ya kupongezwa, hasa
kutokana na uwezo mdogo wa serikali, wa kumhudumia kila kijana anayehitaji
udhamini wa masomo, ndani na nje ya nchi.
“Nataka nieleze
shukrani zangu za dhati kwa ‘initiative’ hizi mlizoanzisha, tukizingatia kuwa
hali ya maisha inabadilika hasa kutokana na ushindani wa soko la ajira katika
ngazi za kitaifa na ulimwenguni kote, naamini ‘the more we get quality
education, the more we set to win the global competitive employment market”,
alisema Mhe Othman.
Naye, Meneja wa ‘STUDY
ABROAD’ Bw Yussuf Mohamed Suleiman, ameiomba Serikali kuzidisha mashirikiano na
taasisi yake, ili kuweza kukabiliana na changamoto zinazowakabili ambazo ni
pamoja na uelewa mdogo wa jamii katika upatikanaji wa fursa za masomo nje ya
Nchi, upotoshaji wa taarifa, na gharama kubwa za tozo katika huduma za
usahihishaji wa vyeti na pia za vipimo vya Maradhi ya Corona (COVID-19).
Meneja huyo aliambatana
na viongozi mbali mbali pamoja na Mlezi wa Taasisi hiyo, Dkt Sira Ubwa
Mwamboya, ambaye alipongeza fursa muhimu pamoja na zile zinazotolewa na
Serikali, za kuwawezesha vijana kujiendeleza kielimu, kwaajili ya maendeleo ya
Nchi na taifa kwa ujumla.
MWISHO.


0 Comments:
Post a Comment