![]() |
| Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba akuzungumzia juu ya mgawanyo wa fedha zilizotolewa na IMF katika Hafla iliyofanyika Dodoma |
Na Ramadhani Kissimba, WFM, Dodoma
Waziri wa Fedha na
Mipango Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amewahakikishia Watanzania kuwa Mkopo
wenye masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 567.3 sawa na shilingi
trilioni 1.3 uliotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa ajili ya
kukabiliana na athari za Uviko-19 zitasimamiwa kikamilifu ili kuleta tija
iliyokusudiwa.
Akizungumza na vyombo
vya habari vya ndani na nje ya nchi Jijini Dodoma, Dkt. Nchemba alisema kuwa
kati ya fedha hizo, dola za Marekani milioni 189.1 ni mkopo nafuu usio na riba
ambao umetolewa kupitia dirisha la Rapid credit Facility (RCF), na
dola za Marekani milioni 378.2 ni mkopo nafuu wenye riba ndogo kupitia dirisha
la Rapid Financing Instrument (RFI),” alisema Dk. Nchemba.
Aliongeza kuwa fedha
hizo tayari zimepokelewa nchini na zitatumika ndani ya mwaka wa fedha 2021/21
katika sekta zilizoathiriwa na UVIKO – 19 ambazo ni afya, elimu, utalii,
maji, pamoja na kusaidia kaya masikini kupitia mfuko wa Maendeleo ya Jamii
(TASAF).
Aidha Dk. Nchemba
alisema kuwa ili kupambana na ugonjwa huu ambao umeathiri kwa kiasi kikubwa
uchumi Serikali itahakikisha fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa
hasa katika kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani, wagonjwa hospitalini na
kuongeza upatikanaji wa vifaa tiba katika hospitali hapa nchini.
‘’Fedha hizi
zitatumika katika kujenga madarasa au kujenga shule mpya ili kupunguza
mlundikano wa wanafunzi darasani na kuwaepusha na maambukizi ya ugonjwa wa
UVIKO -19, aidha pesa hizi zitatumika katika kuongeza upatikanaji wa mitungi ya
hewa ya oksijeni hasa katika hospitali zilizo pembezoni mwa mji ili kuweza
kuokoa maisha ya Watanzania’’, alisema Dk.Nchemba.
Pia Dk. Nchemba
amezitaka sekta zote zitakazopata fedha hizo kuhakikisha kuwa zinatumika kwa
kuzingatia makubaliano kati ya Serikali na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF)
na kulingana na mpango uliondaliwa kwa pamoja na sekta husika wa kukabiliana na
athari za UVIKO-19.
Kwa upande wake Waziri
wa nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Jamal
Kassim Ali, alilishukuru Shirika la Fedha Duniani (IMF) kwa kuipatia Tanzania
mkopo huo ambapo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imepatiwa dola milioni 100
ambazo zimeelekezwa kutumika katika sekta mtambuka zilizoathirika na UVIKO -19
hasa katika sekta ya Utalii.
Ali alisema kuwa
pamoja na sekta zingine kuathirika na janga la UVIKO – 19, Zanzibar imeathirika
zaidi katika sekta ya Utalii ikizingatiwa kuwa utalii ndio kitovu cha uchumi wa
visiwa hivyo.
“Zanzibar ilikuwa
inapokea watalii takribani 567,000, lakini kutokana na janga la UVIKO – 19, kwa
mwaka jana pekee imepokea watalii chini la 100,000, hivyo upatikanaji wa fedha
hizo utasaidia sekta hizo ili kuweza kukuza uchumi wa Zanzibar na Tanzania kwa
ujumla,” alisema Mhe. Ali.
Naye Mwakilishi Mkazi
wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) Bw. Jens Reinke alisema shirika hilo
lipo tayari kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo nchini
ili kupambana na maambukizi ya UVIKO -19 na kusaidia kukuza uchumi wa nchi.
Bw. Reinke aliongeza
kuwa ofisi yake ipo tayari kufanya kazi na wadau wote wakiwemo waandishi wa
habari kwa ajili ya utoaji wa taarifa zitakazo saidia kutatua changamoto
mbalimbali za kiuchumi na kijamii ukiwemo UVIKO-19 pamoja na kupambana na
umasikini.
Aliahidi kuwa Taasisi
yake inaendelea na majadiliano mengine na Tanzania kwa ajuili ya kuiwezesha
Zaidi kifedha kwa ajili ya kujenga uchumi wake pamoja na kuendeleza mapambano
dhidi ya UVIKO-19 ambao umeathirini uchumi wa nchi mbalimbali duniani ikiwemo
Tanzania.

0 Comments:
Post a Comment