![]() |
| Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaaliwa |
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewapa muda wa mwezi mmoja viongozi wa mikoa na
halmashauri wawe wamekutana na wafanyabiashara wadogo wadogo maarufu kama
Wamachinga na kupanga namna bora ya usimamizi wa shughuli za biashara ikiwemo
kutenga maeneo ya kufanyia biashara zao.
Hatua hiyo ni
utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamuhuri ya Mungano wa Tanzania Samia
Suluhu Hassan aliyoyatoa wakati akizindua mpango wa uelimishaji na uhamasishaji
wa sensa ya watu na makazi wa 2022, ambapo aliwataka Wakuu wa Mikoa wawe makini katika zoezi
la kuwapanga Wamachinga nchini na kuepuka vurugu, fujo na uonevu.
Ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza kwa njia ya video na Waziri,
Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Waziri wa
Viwanda na Biashara, Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Uongozi wa Wamachinga.
Waziri
Mkuu amewaelekeza viongozi wa Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na wilaya
waone namna ya kutumia baadhi ya barabara za katikati ya majiji na miji
kufungwa muda wa alasiri ili kuruhusu Wamachinga kufanya biashara zao katika
barabara hizo.. “Hii ni fursa nzuri kwa wajasiriamali wetu kufanya shughuli
zao.”
Amesema
viongozi hao wa mikoa kwa kushirikiana na viongozi wa machinga na machinga
wanaweza kutenga maeneo maalumu na kuanzisha magulio ya mwishoni mwa wiki,
utaratibu huo utawezesha wajasiriamali wengine kufanya shughuli zao za kiuchumi
kama madereva wa bodaboda, machinga na taksi watakaokuwa wakisafirisha abiria.
Kadhalika,
Waziri Mkuu amewataka viongozi hao wahakikishe maeneo watakayoyatenga kwa ajili
ya wamachinga kufanya biashara zao yanatambulika na yanakuwa na miundombinu
muhimu kama vyoo, maji ili kuyaboresha.
Waziri
Mkuu amesema Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara ina mkakati wa
kutoa elimu kwa wajasiriamali wadogo kwa lengo la kuwapa uelewa mpana wa
biashara wanazofanya.
Naye,
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Ummy Mwalimu amesema wamepokea maelekezo
hayo na kwamba tayari wameshaanza kuandaa muongozo wa kuratibu shughuli za
Wamachinga ambao utawawezesha viongozi wa mikoa kuweza kuwasimamia
wafanyabiashara hao.
Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara ametumia
fursa hiyo kuwahakikishia Wamachinga pamoja na wafanyabiashara wadogo nchi
kwamba kwa sasa rasmi Serikali katika sera ya Biashara Ndogo ndogo (SME) nchini
imewatambua Wamachinga.
Awali, Mwenyekiti wa Shirikisho la Wamachinga
Tanzania, Ernest Matondo Masanja pamoja na mambo mengine ameishukuru Serikali
kwa hatua inazochukua kuhusu Machinga na kwamba ameahidi kuendelea kushirikiana
nayo.

0 Comments:
Post a Comment