WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Ofisi ya Rais-TAMISEMI
ihakikishe inasimamia ujenzi wa majengo ya ofisi za halmashauri ya wilaya ya
Kigoma unafanyika kwenye Kata ya Mahembe kama ilivyopendekezwa katika vikao vya
Baraza la Madiwani si katika Kata ya Kamala linalopendekezwa na watalamu.
Ametoa agizo hilo leo (Ijimaa, Septemba 17, 2021) mara
baada ya kusimamishwa na wakazi wa kata hiyo ambao wamedai maamuzi
ya madiwani yamebadilishwa na kusisitiza kuwa kama sababu ni eneo kutofaa kwa
ujenzi wa majengo ya ghorofa wabadilishe ramani Ili yajengwe majengo ya
kawaida.
Wananchi hao ambao waliwasilisha malalamiko yao kupitia mabango
walimueleza Waziri Mkuu kwamba hawaridhishwi na maamuzi ya Serikali ya
kuhamishia ujenzi wa ofisi za halmashauri katika Kata ya Kamala wakati Baraza
la Madiwani lilishatoa maamuzi kupitia vikao rasmi.
Baada ya kusikiliza malalamiko hayo, Waziri Mkuu alimtaka Katibu
Tawala wa Mkoa wa Kigoma Rashid Mchata atoe ufafanuzi juu la suala hilo ambapo
kiongozi huyo amekiri kuwa ni kweli ujenzi ulipendekezwa ufanyike katika eneo
hilo ila uamuzi wa kubadilisha ulitokana na ushauri wa wataalamu ambao walisema
eneo hilo halifai kujengwa majengo ya ghorofa kama ramani inavyoonesha.
Waziri Mkuu amesema kwamba “Kama eneo hili halifai kujengwa
ghorofa ni lazima mjenge majengo ya ghorofa? Wananchi wanahitaji majengo ya
kutolea huduma. Unajua maamuzi ya eneo la ujenzi yameamuliwa na wananchi
kupitia Baraza la Madiwani, hivyo yazingatiwe huko msiende kujenga.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema “Serikali ya Awamu ya Sita
inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ipo makini na haiwezi
kuwaangusha, halmashauri itajengwa katika eneo lililochaguliwa na vikao vya
Baraza la Madiwani na kama wataalamu watasema eneo hilo halifai kujengwa
majengo ya chini waende kuhamisha kijiji maana patakuwa hapafai kwa makazi.”
Naye, Mbunge wa jimbo
la Kigoma Kaskazini Assa Makanika amesema Baraza la Madiwani lilipendekeza kuwa
ujenzi wa jengi la halmashauti ijengwe katika eneo hilo na alishangaa kusikia
ujenzi huo ukihamishiwa katika eneo linguine, ameomba maombi ya wananchi
yasikilizwe.
Pia, Diwani wa Kata ya
Mahembe, Mamisho Seif alisema Baraza la Madiwani lilifanya vikao na kupiga kura
kuamua eneo ambalo zitajengwa ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma ambapo
kata ya Mahembe ilichaguliwa kati ya kata sita zilizopendekezwa.
“Jambo la kusikitisha ni kitendo cha wataalamu kufanya
mabadiliko ya eneo la ujenzi na kuhamishia katika Kata ya Kamala. Mheshimiwa
Waziri Mkuu tunaomba maamuzi ya Baraza la Madiwani yafuatwe.”
Awali, Mwenyekiti wa
Kijiji cha Mahembe alisema baada ya kupekea taarifa kwamba eneo lao
limechaguliwa kujengwa ofisi za halmashauri walitoa bure eneo la ukubwa wa
ekari 25 kwa Serikali ili liweze kutumia kwa ajili ya ujenzi huo.
Aliongeza kuwa wakati wakisubiri ofisi hizo zijengwe walitoa
majengo ya shule ya msingi yatumike kama ofisi na wao kuamua kujenga shule
nyingine, hivyo wanashangazwa na taarifa za kuhamishwa kwa makao makuu ya
halmashauri yao, ambapo waliiomba Serikali iingilie kati suala hilo.
Kwa upande wake, Naibu wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, David Silinde
amemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba wamepokea maelekezo na watasimamia
utekelezaji wa mapendekezo ya Baraza la Madiwani na Ofisi za Halmashauri ya
Wilaya ya Kigoma zitajengwa katika eneo hilo na si lazima yajengwe maghorofa.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo
kuzungumzia juhudi zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita za kuendeleza zao
la mchikichi nchini na kuwataka wakazi wa mkoa huo kuachana na kilimo cha
mazoea na badala yake wasikilize ushauri wa unaotolewa na wataalamu ili
kujiongea tija.
Akiwa katika Gereza la Kwitanga ambalo ni miongoni mwa maeneo
maalumu kwa ajili ya kilimo cha mchikichi, Mheshimiwa Majaliwa amesema
muitikio wa taasisi na wakazi katika kilimo hicho umetafsiri wazi mafanikio
katika safari ya kuifanya Tanzania kujitolesha kwa mafuta ya kula na kuwa
kitovu cha zao hilo katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki.
Amesema miche ya michikichi kwa sasa inatolewa bure, hivyo
wsananchi wachangamkie fursa hiyo kwa kuongeza ukubwa wa mashamba na hatimaye
kuipunguzia Serikali matumizi ya fedha nyingi za kigeni zinazotumika katika
kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi.
Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameisisitiza Serikali
iwasaidie wananchi wanaotaka kulima zao la michikichi kwa kuwapa elimu kuanzia
hatua za awali za utayarishaji wa mashamba, upatikanaji wa mbegu, pembejeo hadi
upatikanaji wa masoko. “Suala la masoko la zao hili msiwe na shaka soko la
uhakika lipo hapa hapa nchini.”
0 Comments:
Post a Comment