Zuhura Yunus : wanawake wa Zanzibar sio legelege

 


 

Picha na Mtandao

Na Salum Vuai


MWANDISHI wa habari wa Idhaa ya Kiswahili katika Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC Zuhura Yunus, amezindua kitabu alichoandika kutambua mchango wa wanawake katika kufanikisha Mapinduzi ya Januari 12, 1964 visiwani Zanzibar.

 

Katika uzinduzi wa kitabu hicho uliofanyika Novemba 6, 2021 kwenye hoteli ya Golden Tulip iliyoko karibu na uwanja wa ndege Zanzibar, mwanahabari huyo Mtanzania mwenye asili ya Zanzibar, alitaja mambo kadhaa yaliyomtia shauku ya kuandika riwaya hiyo adimu.

 

Alisema kitabu hicho alichokipa jina la ‘Biubwa Amour Zahor: Mwanamapinduzi mwanamke’, kimelenga kuonesha ushiriki wa wanawake ambao kwa bahati mbaya hautajwi inavyostahiki katika kuwakumbuka watu waliofanikisha Mapinduzi yaliyoung’oa utawala wa kigeni hapa Zanzibar na kuwapa wazalendo uhuru wa kujitawala.

 

Alisema maudhui ya riwaya hiyo yalikusanywa kutoka kwa watu mbalimbali ndani na nje ya Tanzania wanaomjua Biubwa Amour Zahor ambaye ndie muhusika mkuu.

 

“Azma yangu ni kutaka kufuta dhana iliyoganda katika akili za watu wengi  kwamba wanawake wa Kizanzibari eti ni legelege’, na kuonesha namna Biubwa alivyoendesha harakati na kuwa kiungo muhimu kwa waasisi wa Mapinduzi hayo,” alisema mtangazaji huyo maarufu wa BBC Swahili.

 

Alieleza kuwa inasikitisha kwamba wakati Mapinduzi hayo yakikaribia miaka 58 sasa, mchango wa wanawake umekuwa ukisahaulika, na pale unapokumbukwa hautajwi kwa ukubwa wake halisi.

 

“Tukio hili muhimu katika historia ya Zanzibar limekuwa likionekana kama ni la wanaume tu, wanawake waliokuwa mstari wa mbele katika mapambano  ya kuuangusha utawala wa kigeni wanapewa nafasi ndogo sana kwenye maandishi ya historia ya tukio hilo au hawapewi kabisa,” alibainisha.

 

Zuhura aliishauri Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuzijumuisha kumbukumbu zinazowaelezea akinamama majasiri walioshiriki kwa namna tofauti harakati za siasa hadi kufanyika Mapinduzi, na kuziweka katika makumbusho ya ‘Mapinduzi Square’ Michezani na  majengo mengine ya kihistoria ili nao wafahamike.

 

Mgeni rasmi katika uzinduzi huo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dk. Saada Mkuya Salum, aliusifu ujasiri wa muhusika mkuu Biubwa, kwa kuridhia  kuelezea namna alivyozijua na kushiriki harakati za Mapinduzi akitoa kila aina ya msaada kwa washiriki wanaume hadi yakafanikiwa.

 

Aidha, alimpongeza Zuhura Yunus, kwa jitihada zake ambazo alisema zimeinua hadhi ya mwanamke wa Kizanzibari na kuiongezea thamani historia ya visiwa hivi kwa kuonesha ukweli uliokosa sauti.

 

“Hii simulizi ya mwanamke aliyesimamia kile alichokiamini, iwe chachu ya kuamsha ari kwa wengine kufanya tafiti na kuandika vitabu vingi zaidi kuhusu utajiri mkubwa wa historia na maudhui mengine kuhusu Zanzibar ambavyo vinaweza kutumika kufundishia katika skuli zetu,” alieleza Waziri Mkuya.

 

“Sehemu ambayo ilinigusa sana na kunitoa machozi niliposoma kitabu hiki, ni suala la unyanyasaji wa kijinsia. Kumbe mambo haya yalikuwepo tokea zamani. Ila ujasiri wa Biubwa kumsimulia Zuhura naye akaweza kuandika si kitu kidogo,” alisema.

 

Kwa upande mwengine, Dk. Mkuya alieleza kuwa kitabu hicho kinaonesha pia umuhimu wa elimu kwa wanawake wa Kizanzibari na nguvu walizonazo iwapo wanapewa nafasi na kuongeza kuwa, kama angelipata fursa ya kukipa jina jengine, angekiita Nguvu ya Mwanamke.

 

Kitabu hicho ambacho Zuhura alianza kukusanya maudhui yake tokea mwaka 2017, kinatarajiwa kuzinduliwa pia jijini Dar es Salaam Novemba 13, 2021, na kinapatikana kwa nakala ngumu na laini.

 

Jumla ya nakala 150 ziliuzwa wakati wa hafla ya kukizindua iliyohudhuriwa pia na mawaziri mbalimbali wastaafu na wa sasa, watendaji wa taasisi za umma na binafsi pamoja na mabalozi kadhaa.

 

Wengine ni wadau wa fasihi na uandishi, familia ya mtunzi na muhusika mkuu Biubwa Amour Zahor, na uhakiki wake ulisomwa na mwanaharakati Salma Maoulid, huku kikundi cha Tausi Women Taarab na Rahat zaman vikitoa burudani mwanana ya taarab asilia.

About mmedia

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment