WIZARA YA AFYA, USTAWI
WA JAMII, WAZEE,
JINSIA NA WATOTO
HOTUBA YA MHESHIMIWA
MHE. NASSOR AHMED MAZRUI WAZIRI WA AFYA USTAWI WA JAMII, WAZEE, JINSIA NA
WATOTO ALIYOITOA KUZUNGUMZIA MIRADI YA MAENDELEO INAYOTEKELEZWA KWA FEDHA ZA
IMF
HOTEL VERDE 12
NOVEMBER, 2021
Ndugu Waandishi wa
Habari
Assalaamu
alaykum,
Nianze kwa kumshukuru
Mwenyezi Mungu, aliyetupa uhai na nguvu ya kutuwezesha kukutana hapa leo,
katika shughuli hii adhimu tukiwa katika hali ya afya njema.
Leo hii tumepata fursa
tena ya kuzungumza na Wananchi kupitia waandishi wa Habari.
Ndugu Waandishi wa
Habari, Wizara hii ina majukumu ya msingi yafuatayo: -
Kuhakikisha kwamba
wananchi wote wa Zanzibar bila ya ubaguzi wa aina yoyote wanakuwa na afya njema
pamoja kuwapatia huduma bora za kinga na tiba;
Kuratibu na kusimamia
upatikanaji wa haki kwa makundi yenye mazingira magumu kwa kuimarisha mifumo ya
hifadhi ya jamii na huduma kwa Wazee, Watoto na wanaoishi katika mazingira
magumu zaidi; na
Kuratibu na kusimamia
utekelezaji wa haki za wanawake na watoto katika kukabiliana na vitendo vyote
vya udhalilishaji ikiwa ni pamoja na kusimamia utekelezaji wa sera, sheria
zinazohusu maendeleo ya wanawake na watoto pamoja na kuwaendeleza wanawake kwa
kuzingatia mipango ya Kitaifa, Mikataba ya Kimataifa na Kikanda.
Ndugu Waandishi wa
Habari, Itakumbukwa kwamba, hivi karibuni Serikali ya awamu ya nane (8)
inayoongozwa na Mhe Rais Mwinyi imeadhimisha mwaka mmoja tokea kuingia
madarakani. Katika maadhimishisho hayo ambayo yaliadhimishwa kwa shughuli
mbali mbali, kilele chake kilifanyika tarehe 6 November, 2021 katika hoteli ya
Golden Tulip, Kisauni mjini Unguja ambapo Mheshimiwa Rais alihutubia
Taifa.
Katika hotuba yake
alieleza kwa kina Mpango wa Utekelezaji wa Serikali katika kipindi cha mwaka
mmoja ujao na kuelekea miaka minne iliyo kwenye awamu hii. Maadhimisho hayo
yalihudhuriwa na Viongozi mbali mbali wa chama na serikali. Aidha katika hotuba
yake aliahidi Serikali yake imepanga kutumia fedha katika kuimarisha miradi
iliyopo na kuanzisha miradi kadhaa ya maendeleo. Serikali ya Awamu ya 8 katika
kutekeleza hilo imetenga kiasi kikubwa cha fedha ambazo zitatumika kupitia
sekta mbali mbali. Hii ni Pamoja na sekta ya inayojumuisha maendeleo na ustawi
wa Jamii wa Wazee, Jinsia na Watoto.
Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar katika kuufufua Uchumi kutokana na janga la UVIKO-19 imechukua
mkopo wa fedha kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) jumla ya shilingi Billion
230 utakaoharakisha maendeleo hayo. Kutoka na Umuhimu wa Sekta ya Afya katika
utoaji uduma kwa Jamii Wizara yangu imepatiwa kiasi cha shilingi bilioni
69.
Ndugu Waandishi wa
Habari,
Hili la matumizi ya
Mkopo wa IMF ndio leo ambalo nataka kulifanyia ufafanuzi ili muweze kujua
zitatumika vipi na kwa maeneo yepi, kwenye Sekta ya Afya.
Ndugu Waandishi wa
Habari, Sekta yangu imepanga kutekeleza Miradi mbali mbali ya kuimarisha
miundombinu ya afya na upatikanaji wa vifaa tiba
Kwanza, nianze na
miradi ya kuimarisha miundombinu ya Afya ikiwemo ujenzi wa hospitali mpya ngazi
ya Mkoa wa Mjini Magharibi, eneo la Lumumba itakayokuwa na uwezo wa kulaza
wagonjwa 200 kwa wakati mmoja. Hospitali ya Mkoa itakuwa na ghorofa tano,
itakuwa na huduma za wagonjwa kwa nje (OPD) na waliolazwa (IPD). Hospitali
itakua na huduma za kisasa za MRI, CT scan na kutoa huduma zote za kitaalamu
zikiwemo huduma za Sikio, Pua na Koo (ENT), Aidha kutakua na huduma za macho,
meno, kliniki na wodi za kulaza wagonjwa mbali mbali. Ujenzi huu una nia ya
kuongeza wigo wa huduma na kupunguza idadi ya watu wanaokwenda hospitali ya
Mnazi Mmoja ambayo itaendelea uboreshwa ili ikidhi hadhi yake yakuwa hospitali
ya rufaa.
Kuhusu miundombinu ya
Hospital ya Mkoa ya Abdalla Mzee tutajenga chumba cha Wagonjwa mahututi ICU,
Chumba cha Kuhifadhia maiti na kuweka vifaa vya kisasa vya uchunguzi kama
“Digital X ray”, huduma za figo “Dialysis”, vifaa vya chumba cha upasuaji na
kuweka mtambo wa gesi tiba “Oxygen Plant” ambao utasambaza moja kwa moja kwenye
kitanda cha mgonjwa.
Sambamba na ujenzi huo,
Serikali itajenga hospitali 10 katika ngazi ya Wilaya zinazotegemewa kwa kila
moja kulaza wagonjwa 100 kwa wakati Mmoja, pamoja na nyumba za wafanyakazi kwa
baadhi ya hospitali zitakazotosha familia 16. Hospitali hizo zitajengwa
katika maeneo ya Unguja na Pemba
Kwa Unguja ujenzi huo
utakua kwenye maeneo yafuatayo:
Chumbuni
Magogoni,
Kivunge
Pangatupu
Dunga,
Makunduchi,
Pemba
Micheweni,
Vitongoji Chakechake
na
Kinyasini Wete Pemba.
Ndugu Waandishi wa
Habari,
Michoro ya Hospitali
zote hizi imekamilika na taratibu za manunuzi ili kuwapata wakandarasi wa
ujenzi zitatangazwa rasmi kwa kutumia njia ya haraka ili kazi iliyokusudiwa
ifanyike kwa muda uliopangwa. Kazi za ujenzi zinaanza mwezi wa Disemba, 2021 na
kukamilika Juni, 2022.
Hospitali hizi zitatoa
huduma za wagojwa wa nje (OPD) na waliolazwa, uchunguzi kwa kutumia vifaa vya
kisasa (X-ray ya kijiditali, Ultrasound, upimaji wa damu kujuwa kiwango cha
damu, uwepo wa magojwa ya sukari, mafuta kwenye damu, mabadiliko ya damu
yanayohusiana na figo na kadhalika). Huduma nyengine ni Pamoja na huduma za
ICU, magojwa ya wanawake, Kliniki za waja wazito, huduma za uzazi wa kawaida na
wa operesheni, upasuaji mdogo (wanaume na wanawake), huduma za watoto ikiwemo
sehemu ya kuwaweka “watoto njiti”. Hospitali zote zitakuwa na sehemu ya kutoa
huduma kamilifu kwa wahanga wa Unyanyasaji wa Kijinsia (One stop centres).
Ndugu Waandishi wa
Habari,
Serikali itanunua
magari 12 ya kubebea wagonjwa (ambulances). Gari hizo zitakuwa za aina ya
Toyota Land cruiser zitakazonunuliwa moja kwa moja kutoka kiwandani
zitasambazwa katika hospitali zote za Wilaya na mbili katika hospitali za
Mikoa; vile vile, Serikali itanunua magari matano (5) ya kusambazia dawa katika
hospitali na vituo vya afya Unguja na Pemba. Huduma hii itaondosha gharama
zinazotumika hivi sasa za kukodi gari za kampuni binafsi kwa kufanya kazi hiyo
na pia kuhakikisha usalama wa dawa na vifaa tiba vinavyosafirishwa
Ndugu Waandishi wa
Habari,
Kila hospitali ya wilaya
itakuwa na Mtambo wa kuchomea taka hatarishi kwa lengo la kudhibiti mazingira.
Aidha kati ya mitambo hiyo, miwili itakuwa ni yenye uwezo mkubwa wa kuchoma
taka hatarishi nyingi kwa wakati mmoja na itafungwa katika hospitali ya Mkoa
ili iweze kutoa huduma kwa hospitali za karibu za Serikali na pia Sekta
binafsi
Ndugu Waandishi wa
Habari, Huduma za Damu Salama zitaimarishwa kwa kupatiwa vitendea kazi muhimu
vinavyoendana na mahitaji husika ili kuweza kutoa huduma muda wote, hali ambayo
kwa sasa kitengo hakina vifaa hivyo. Uwepo wa vifaa hivyo kutaongeza damu
iliyopimwa na kuwa tayari kupewa mgonjwa anaehitaji
Ndugu Waandishi wa
Habari,
Serikali itaweka
mitambo 2- katika Hopsitali za Pangatupu na Abdalla Mzee ya kuzalisha gesi tiba
(oxygen) kila mmoja ikiwa na uwezo wa kuzalisha mitungi 400 kwa siku,
itakayotumika kwenye hospitali nyengine Pemba na Unguja zitakazohitaji huduma
hii.
Ndugu Waandishi wa
Habari,
Serikali inahakikisha
kwamba Hospitali zote tunazozijenga zitakuwa na vifaa tiba vya kisasa katika
utoaji wa huduma za uchunguzi za mionzi (X ray, CT-scan na Ultrasound) na za
maabara ili kutambua maradhi mbali mbali ikiwemo figo, saratani
nakadhalika,
Ndugu Waandishi wa
Habari,
Matarajio/faida
zitakazopatikana baada ya kukamilika mradi ni kupeleka huduma za Afya zilizo
bora karibu na wananchi, pia itapunguza idadi ya wagonjwa wanaosafirishwa nje
ya Zanzibar.
Ndugu waandishi wa
Habari,
Hizi huduma za afya
ambazo Serikali yetu inaziimarisha hazitokuwa na maana kama hatutozitumia,
naomba niwaambie wananchi wote, kike kwa kiume kuanza kuhudhuria kliniki
mapema, hii ni Pamoja na wajawazito kujifungulia Hospitali. Aidha tujitahidi
kupeleka watoto wote kupimwa ili kujua maendeleo yao ya afya na ukuaji wao, hii
ni pamoja na kupata chanjo zote stahiki ili kuwakinga na maradhi.
Ndugu waandishi wa
Habari
Hitimisho
Nachukua fursa hii
kuishukuru Serikali ya awamu ya 8 chini ya Uongozi mahiri wa Dr Mwinyi, juhudi
za kuwaletea maendeleo wananchi zimeanza kuonekana ikiwa pamoja na uimarishwaji
wa Sekta ninayoiongoza. Ambapo zinaimarisha kwa juhudi kubwa ili kuwafikishia
wananchi huduma safi kwa wananchi wote wa Zanzibar. Huduma ambazo zinapatikana
karibu na ulipo na bila ubaguzi wowote.
Mwisho
Nachukua nafasi hii
vile vile kuwakumbusha Wazanzibari wote kupata Chanjo dhidi ya UVIKO 19. Idadi
ya waliopata chanjo inaendelea kuongezeka. Napenda mufahamu hadi tarehe
10 Novemba 2021 jumla ya watu 70,000 tayari wameshapatiwa chanjo hizo hapa
Zanzibar. Hivyo nawasihi wananchi wote wenye umri kuazia miaka 18 na kuendelea
wajihimu kuchanja. Kwani ukichanja utakua umetengeneza kinga ya kupambana na
ugonjwa huu thakili, si hivyo tu bali utakua pia unawakinga wengine na
maambukizo. Inatakiwa tufahamu pia kuwa Kinga ni bora kuliko tiba na wageni
wote wanakaribishwa Zanzibar ipo Salama
Ndugu waandishi wa
habari
Ahsanteni sana kwa
kunisikiliza.
0 Comments:
Post a Comment