Peter
Haule na Josephine Majura, WFM
Kamishna wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha
nchini, Dk. Charles Mwamwaja amesema kuwa watanzania chini ya asilimia 50 ndio
waliofikiwa na huduma za fedha jambo ambalo limeifanya Serikali kuwa na Wiki ya
Huduma za Fedha Kitaifa ili kuongeza uelewa kwa wananchi kwa lengo la kuchochea
ustawi wa jamii.
Hayo ameyabainisha wakati akitembelea mabanda
katika maonesho ya Wiki ya Fedha yanayoendelea katika viwanja vya Mnazi Mmoja
Jijini Dar es Salaam ikiwa ni siku ya kwanza ya maonesho hayo.
DK. Mwamwaja alisema huduma za fedha zinarahisisha
utaratibu wa kubadilishana bidhaa na huduma jambo ambalo ni muhimu katika
maendeleo ya uchumi kwa nchi yeyote Duniani ikiwemo Tanzania hivyo ni lazima
kuwa na mkakati wa kutoa elimu kwa umma kuhusu uelewa wa huduma hiyo.
“Watu wanadhulumiwa na hawajui waende wapi,
nani ni mtoaji wa huduma hiyo rasmi, mteja akidhulumiwa aende wapi na
hawajui kuwa mteja wa huduma za fedha analindwa, hivyo Serikali imeamua kutoa
elimu kwa umma ili kuondoa sintofahamu hiyo”. alieleza.
Dk. Mwamwaja alisema kuwa Sekta ya Fedha
inarahisisha upatikanaji wa mitaji na uwekezaji ndio maana vikundi vidogo vya
kuweka na kukopa kama Vikoba, vinasaidia kukuza mitaji ambayo inaweza kutumika
kuwekeza kwenye miradi ya ufugaji na mingine ambayo inamanufaa si tu kwa mtu mmoja
mmoja bali kwa Taifa kwa ujumla.
Aidha alisema matokeo chanya ya Sekta ya Fedha
hayawezi kufikiwa bila kuwekeza katika elimu ili wananchi waweze kutumia fursa
zilizopo kwa maendeleo yao na nchi kwa ujumla.
Alisema umbo la Sekta ya Fedha limegawanyika katika
maeneo matano ambayo ni masuala yanayohusiana na huduma za Benki, Bima,
Masoko ya Mitaji na Dhamana, Mifuko ya Jamii na Huduma ndogo ya Fedha.
Maonesho ya Huduma za Fedha Kitaifa yameanza
Novemba 8 na kutarajiwa kuhitimishwa Novemba 14 mwaka huu katika Viwanja vya
Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.

0 Comments:
Post a Comment