MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman ameshukuru juhudi zinazochukuliwa na jamii ya kimataifa katika ujenzi wa amani ya nchi na uhamasishaji wa maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo katika mazungumzo yake na Ujumbe kutoka Shirika la Kimataifa la Kuhamasisha Amani na Utatuzi wa Migogoro (Search for Common Ground) uliomtembelea Ofisini kwake Migombani, Jijini hapa.
Amesema suala la ujenzi wa amani ya nchi ni muhimu sana, hasa linapozingatia utoaji wa haki kwa jamii (social justice) kwa umakini, ili kutoa fursa ya kukuza mshikamano wa kweli na hatimaye kupelekea taifa lenye maelewano.
Mheshimiwa Othman ameeleza kuwa hayo yatawezekana kwa kuendeleza utamaduni wa uwajibikaji wa kila mmoja katika ngazi zote za umma, kupitia misingi muhimu ya utawala bora, kwa kutarajia jamii iliyofungamana.
“Pamoja na kwamba Zanzibar inatokana na watu wa asili tofauti ‘cosmopolitan’ bali fungamano la Wazanzibari wenyewe limejengeka kwa utamaduni bora uliotokana na misingi ya ustaarabu ambao unahitaji kuendelezwa, na wala siyo kuutelekeza kwa thamani ya siku moja tu ya uchaguzi kama ambavyo inashuhudiwa kila baada ya muda”, amesema Mheshimiwa Othman.
Aidha Mheshimiwa Othman ameeleza utayari wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kushirikiana na Mashirika ya Kimataifa, akisema kuwa milango ipo wazi katika kuhamasisha na kusaidia maendeleo, amani ya nchi, maridhiano, na kujenga heshima ya watu wa visiwa vya Unguja na Pemba na Tanzania kwa ujumla.
Naye Mkurugenzi wa Shirika hilo wa Kanda ya Afrika Mashariki na Kati, Bi Rebecca Besant ameeleza azma ya shirika lake katika kuungamkono kasi ya maendeleo ya Serikali ya Awamu ya Nane ya Zanzibar, pamoja na kuhamasisha amani ya nchi inayolenga kunusuru migogoro ya mara kwa mara.
Bibi Besant amesema yeye na shirika lake wanahisi ni vyema pia kwa Zanzibar kufikiria namna ya kuleta mageuzi ya taasisi na mfumo wa utoaji haki, utakaozingatia mazingira bora ya kutekeleza ndoto ya maendeleo.
Ujumbe huo umewajumuisha pia Meneja wa ‘Search for Common Ground’ Tanzania, Bw. Hussein Faraji Sengu, Mkuu wa Mradi wa Shirika hilo Zanzibar, Bw. Ali Chikira Stanley, na Afisa wake wa Mawasiliano anayehusika na Vyombo vya Habari, Bw. Khelef Nassor Rashid.
0 Comments:
Post a Comment