Mkurugenzi mtendaji Tume ya kitaifa ya kuratibu na udhibiti wa dawa zakulevya Kanal Burhani Z. Nassor akimkaribisha katibu mkuu omkr Dkt Omar D. Shajak kuzungumza na wafanya kazi wa tume hio ofini kwao migombani
Na Raya Hamad – OMKR
Watendaji na wafanyakazi wa Tume ya Kitaifa Kuratibu na Udhibiti
wa Dawa za Kulevya wametakiwa kudumisha nidhamu katika maeneo yao ya kazi na
kuhakikisha wanatimiza majukumu yao kwa ufanisi.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dkt Omar D. Shajak
ameyasema hayo kwenye kikao cha watendaji na wafanyakazi wa Tume hio ikiwa ni
mfululizo wa ziara zake katika kutembelea taasisi zinazosimamiwa na Ofisi ya
Makamu wa Kwanza wa Rais.
Amewakumbusha watendaji na wafanyakazi hao kusimamia vyema
majukumu yao kama yalivyoelekezwa kwenye mpango wa majukumu ya kazi waliopewa
na kuacha kufanya kazi kwa mazoea ikiwemo uingiaji kazini na utokaji wa kazini.
Dkt Shajak amesema mapambano ya Dawa za kulevya yanaanzia
ofisini hivyo wanawajibu wa kutunza siri, kuwa waadilifu, watiifu na wazalendo
katika kuitumikia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambayo imewaamini na kuwaweka
walipo.
Amesema mapambano ya dawa za kulevya hayatakwisha iwapo
hakutakuwa na mashirikiano yanayoanzia ndani ya taasisi yenyewe hivyo ni wajibu
wa kila mmoja kuchukuwa tahadhari katika mapambano haya kwani ni vita ya wenye
fedha wanaongalia maslahi yao pekee.
“isije kufika mahali ukajiona wewe ndio mtoa habari za ndani
hatutamuonea mtu muhali na iwapo mtu anaona hawezi kutunza siri haendani na
sheria na taratibu za Tume hii ambayo inaelekea kuwa Mamlaka kamili basi mapema
ajisalimishe milango iko wazi mapambano ya dawa za kulevya ni yetu sote hakuna
aliyekuwa hajaguswa kuanzia mtumiaji mwenyewe, si wazazi, walezi , familia na
hata majirani wote tunaathirika wizi umekithiri na mambo mengine yasiyo na
maadili” Dk. Shajak.
Katibu Dkt amewaahidi wafanyakazi hao kuwa Serikali inatambua
changamoto zao na zinafanyiwa kazi kwa hatua ikiwemo ufinyu wa ofisi na uhaba wa
wafanyakazi kwani ni masuala ya kiutawala.
Mkurugenzi Mkuu Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa
za Kulevya Kanal Burhani Z. Nassor amesema Serikali ya Mapinduzi Zanziba kwa
kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais tayari imeshaandaa mswaada wa
sheria na unasubiri Baraka za Serikali ili Tume hio iwe na hadhi ya kuwa
Mamlaka kamili.
Mamlaka ambayo itakuwa na uwezo wa Kisheria wa kuchunguza,
kukamata, kupeleleza na kupeleka kesi Mahakamani ambapo sasa Tume inafanya kazi
za Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na vyombo vingine
vya Ulinzi na Usalama.
Aidha Kanal Burhan amesema Tume imejipanga vyema kulishughulikia
na kudhibiti uingizwaji wa dawa za kulevya na ameiomba jamii kutoa
mashirikiano kwa kuwafichuwa wanaojihusisha na dawa za kulevya ambapo ameahidi
Tume kutoa ushirikiano kwa kudhibiti siri za mtoa habari.
“Jamii ikithubutu kushirikiana na kubadilisha mifumo ya maisha
ambayo tunaishi ya usasa ni wazi suala la matumizi ya madawa ya kulevya hapa
kwetu litakuwa ni historia, nawaomba wazazi na walezi pia muwe wadadisi wa
watoto wenu na kufatilia mwenendo wao, mtoto anakuja na vespa au pikipiki mzazi
huulizi anarudi usiku huulizi anavitoa wapi vitu vya thamani hizi ni dalili
mbaya na turudi kwenye malezi ya asili”alisisitiza Kanal Burhani.
Ziara na ya Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ni
muendelezo na utaratibu uliopangwa ili kuona utekelezaji kwa vitendo wa
majukumu ya taasisi zinazosimamiwa na Ofisi hio zikiwemo Baraza la Taifa la
Watu wenye Ulemavu, Tume ya UKIMWI, Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira na Idara
ya Mazingira na Afisi kuu Pemba.
0 Comments:
Post a Comment