Wafanyabiashara Pemba watakiwa kuacha Magendo

 

Bandari Bubu 

WAFANYABIASHARA kisiwani Pemba wametakiwa kuacha tabia ya kuingiza bidhaa kwa njia ya magendo kwani wanaikosesha Serikali mapato yake ambayo husaidia kutumika kwenye miradi ya maendeeo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Mdhamini wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa upande wa Pemba Habib Saleh Sultan alisema, wafanyabiashara waelewe kwamba fedha zinazokusanywa ndizo zinazojengewa vituo vya afya, skuli, kuwafikishia wananchi huduma za umeme, maji safi na salama na huduma nyengine.

Alisema kuwa, kuna baadhi ya wafanyabiashara hutumia bandari bubu kuingiza bidhaa kwa lengo la kukwepa kodi, jambo ambalo sio sahihi, kwani mapato yanayokusanywa na Mamlaka ndio yanayowanufaisha wananchi kutokana na huduma za kijamii wanazofikishiwa.

Alieleza kuwa, pamoja na vikosi vya ulinzi na usalama vinavyofanya doria katika maeneo ya bahari, lakini wafanyabiashara wamekuwa wakitumia njia mbali mbali ambazo huingiza bidhaa bila kuonekana, hali ambayo inawapa wakati mgumu katika kutekeleza majukumu yao ya kukusanya Kodi.

“Kuna vikosi vya ulinzi na usalama lakini binadamu hawezekani, na wala hawaogopi kwa sababu akikamatwa tunataifisha bidhaa na chombo kilichobeba hatimae kupata wao hasara kwani ni lazima walipe faini, ila hawajali”, alisema Mdhamini huyo.

Alisema kuwa, wamekuwa wakifanya jitihada mbali mbali kuhakikisha wanaondosha kadhia hiyo ili Serikali ipate mapato yake, ingawa sio kitu rahsi, hivyo wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi, jambo ambalo wanaamini litawasaidia kutataua changamoto mbali mbali katika ukusanyaji wa mapato.

“Tumekuwa tukitoa elimu kwa wananchi, wafanyabiasha wadogo na wakubwa pamoja na wanafunzi wa skuli za Chasasa Wete, Madungu na Fidel Castro Chake Chake na Uweleni Mkoani ambazo zimo kwenye mradi maalumu”, alisema.

Alifahamisha kuwa, Serikali ya awamu ya nane kupitia Dk, Mwinyi inawajali wananchi wake katika mambo mbali mbali, ambapo kupitia kodi inajaribu kufanya kila hali kuona kwamba wanaweza kulipa kodi.

Alieleza kuwa, pamoja na kwamba Serikali inahitaji fedha kwa ajili ya kufanya shughuli zake za kimaendeleo, lakini kuna vitu ambavyo imeona kuwa, ipo haja ya kuhakikisha viwango vya kodi vinamsababishia mfanyabiashara kumrahisishia kulipa kodi yake.

“Kuna bidhaa mbali mbali ambazo kwa sasa zimeondolewa ushuru na zile ambazo ni za wafanyabiashara wadogo wadogo ambao wanaonekana kwamba kipato chao ni kidogo, hivyo tuone umuhimu huu wa Serikali kutujali”, alifafanua.

Akizungumzia changamoto nyengine zinazowakabili katika ukusanyaji wa mapato alisema, ni wafanyabiashara kutokuweka kumbu kumbu katika mauzo yao, jambo ambalo linaifanya Mamlaka ikadirie.

“Ikiwa wanaweka kumbu kumbu zao vizuri inakuwa rahisi kujua mauzo ya mfanyabiashara, lakini kama hana risiti ni lazima tumkadirie na hapo ndipo kunatokea malalamiko ya wafanyabiashara”, alisema Mdhamini huyo.

Aidha aliwataka wafanyabiashara hao kushirikiana pamoja na TRA ili kujua utaratibu mzima wa kulipa kodi, sambamba na kuijua sheria ya kodi, kwani itawasaidia kufahamu kitu ambacho anastahiki kulipa.

Kwa upande wao wafanyabiashara wamesema kuwa wamekuwa wakiweka kumbu kumbu wanapouza bidhaa zao, ingawa kwa Pemba hakuna mzunguko wa biashara kutokana na kuwa bei za bidhaa ni kubwa.

“Bidhaa inapofika Pemba huwa tushalipia kodi sehemu nyingi, hivyo hatuwezi kuuza bidhaa kwa bei ndogo jambo ambalo linasababisha wateja kufika kwa uchache”, walieleza.

Walisema kuwa, wafanyabiashara wanaweza kukaa dukani kuanzia asubuhi hadi anapoondoka hajauza chochote na ndio maana wakati mwengine wanashindwa kulipa kodi, kwani kipato chao kinakuwa kidogo.

Ili Serikali ipate mapato yake na kufanya miradi mbali mbali ya kimaendeleo ambayo huwanufaisha wananchi, ipo haja kwa wafanyabiashara kulipa kodi kwa wakati sambamba na wananchi kudai risiti wakati wanaponunua bidhaa.

About mmedia

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment