Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba na
Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Mheshimiwa Regine Hess, wakisaini
mikataba mitatu ya msaada wenye thamani ya Euro milioni 45, sawa na shilingi za
Tanzania bilioni 119.2 kwa ajili ya kusaidia maendeleo katika sekta za maji,
afya na maliasili na utalii, jijini Dar es salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba na
Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Mheshimiwa Regine Hess,
wakibadilishana mikataba ya msaada wenye thamani ya Euro milioni 45, sawa na
shilingi za Tanzania bilioni 119.2 kwa ajili ya kusaidia maendeleo katika sekta
za maji, afya na maliasili na utalii, jijini Dar es salaam.
NA
BENNY MWAIPAJA, DAR
SERIKALI ya
Ujerumani imeipatia Tanzania msaada mwingine wa Euro milioni 45 sawa na
takribani Sh.Bilioni 119.2 kwa ajili ya kutekeleza miradi mitatu katika sekta
za maji, afya na kuendeleza sekta ya maliasili na utalii.
Msaada huo
umekuja siku mbili tangu nchi hiyo iingie makubaliano mengine ya kutoa msaada
wa kiasi cha Euro milioni 71 sawa na zaidi ya shilingi bilioni 190.5, kwa
ajili ya kutekeleza miradi kadhaa ikiwemo maji, uendelezaji wa maliasili na
utalii, afya ya mama na mtoto pamoja na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Akizungumza
baada ya kusaini mikataba hiyo mipya mitatu kwa niaba ya Serikali, na Balozi wa
Ujerumani nchini Tanzania Regine Hess kwa niaba ya Ujerumani, Katibu Mkuu
Wizara ya Fedha na Mipango Emmanuel Tutuba, alisema kuwa fedha hizo zitaisaidia
nchi kukabiliana na athari za Uviko 19, kuboresha uhifadhi wa mazingira na huduma
za jamii.
Tutuba alisema,
kuwa Mkataba wa kwanza uliosainiwa unahusisha mradi wa kuboresha upatikanaji wa
maji na udhibiti wa mabadiliko ya tabianchi na mradi wa kuboresha huduma za
afya uliiotengewa kiasi cha Euro milioni 16.5 sawa shilingi bilioni 43.73.
“Katika fedha
hizo kiasi cha Euro milioni 6 kitatumika kuboresha huduma ya maji kwenye Miji
ya Mbeya, Songwe na Tunduma ambapo zaidi ya watu 500,000 wanatarajiwa kunufaika
na huduma hiyo pamoja na kutoa ajira ya watu 2,000 katika sekta ya maji kwenye
maeneo hayo”. Alisema.
Alifafanua kuwa
mradi wa uboreshaji wa huduma ya afya umetengewa Euro milioni 10.5 na una lengo
la kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya
Afya (NHIF) katika mikoa ya Tanga na Mbeya.
Katibu Mkuu huyo
alisema, kuwa mradi mwingine unaofadhiliwa na Ujerumani una thamani ya Euro
milioni 8.5 sawa na Sh. Bilioni 22.53 zitakazotumika kwa ajili ya kufunga
mitambo maalumu ya kidigitali itakayosaidia kudhibiti magari ya watalii
yanayoingia kwenye Hifadhi za Taifa yasiharibu mazingira katika Hifadhi nne za
Serengeti, Burigi-Chato, Katavi na Mikumi.
“Mkataba
wa tatu tuliosaini unahusisha msaada wa Euro milioni 20 sawa na shilingi za
Tanzania bilioni 53 zilizotolewa kama fedha za dharura kwa ajili ya kukabiliana
na upungufu wa fedha uliotokana na athari za ugonjwa wa UVIKO 19, katika sekta
ya maliasili na utalii”. Aliongeza.
Alieleza kuwa
kusudi la mradi huo ni kufidia mapato yaliyopotea kwa Shirika la Hifadhi za
Taifa (TANAPA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Misitu Tanzania (TAWA), katika maeneo
tengefu katika Pori la Akiba la Selous na Hifadhi za Taifa za Serengeti na
Nyerere.
Tutuba
aliishukuru Ujerumani kwa kuwa rafiki mkubwa wa Tanzania ambapo mpaka sasa
Serikali imenufaika na miradi mingi ya maendeleo iliyofadhiliwa na nchi hiyo
katika Sekta za maji, afya, nishati, matumizi endelevu ya maliasili na uhifadhi
wa mazingira, usimamizi bora wa fedha za umma na fedha za kuandaa miradi.
Kwa upande wake
Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Regine Hess, alisema nchi yake inajivunia
uhusiano wa kindugu uliopo kati ya nchi yake na Tanzania ulifikisha miaka 60
sasa na kwamba nchi hiyo itaendelea kutoa misaada zaidi kwa nchi.
Alielezea
umuhimu wa hifadhi ya mazingira katika maeneo ya hifadhi za taifa pamoja na
kuboresha huduma za kijamii katika nyanja za maji na afya.
Naye Kiongozi
wa Ujumbe wa Ujerumani uliofanikisha upatikanaji wa Msaada huo Bw. Marcus Von
Essen, alisema Ujerumani imeamua kufufua ushiriki wake katika kujenga maendeleo
ya Tanzania ili kuunga mkono uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita.
Kwa upande wake
Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Dk. Damas Ndumbaro, aliishukuru
Ujerumani kwa kusaidia sekta ya Hifadhi za Taifa nchini baada ya kuathiriwa kwa
kiasi kikubwa na ugonjwa wa UVIKO 19 ambapo katika miaka miwili iliyopita
shughuli za utalii zilikwama.
Alisema katika
kipindi hicho ufanisi wa masuala ya utalii ulishuka kwa asilimia 72 na pia
mapato yanayotokana na utalii yalishuka kutoka wastani wa dola za Marekani
bilioni 2.6 hadi kufikia dola bilioni 0.715.
“Tuliomba
misaada kwa nchi nyingi wahisani ili tuweze kukabiliana na athari hizo lakini
ni Serikali ya Shirikisho la Ujerumani pekee limetupatia msaada ambapo hivi
karibuni imetupatia msaada wa Euro milioni 20 na leo tumepewa fedha za nyongeza
kiasi cha Euro milioni 15” Aliongeza Dk. Ndumbaro.
Hafla ya utiaji
saini wa mikataba hiyo imehudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili
na Utalii Dk. Allan Kijazi, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Amina
Khamis Shaaban na Meneja wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW) anayesimamia
Kanda ya Mashariki na Umoja wa Afrika (AU), Gerald Kuehnemund.
0 Comments:
Post a Comment