RC,kaskazini Pemba akunwa na kilimo cha Green House



Na Zuhura Juma,Pemba 

MKUU wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib amesema, Green House zinaweza kuwainua vijana kiuchumi ikiwa watachukua juhudi ya kuzalisha bidhaa nyingi na zenye ubora.

Alisema kuwa, ipo haja kwa Wizara husika kuhakikisha kwamba Green House zilizopo zinatumika kama ilivyokusudiwa katika kuzalisha bidhaa nyingi na bora, ili kusaidia kuinua kipato cha vijana.

Akizungumza katika ziara ya kukagua mradi wa Green House uliopo Shumba Vyamboni Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba Mkuu huyo alisema kuwa, kuna baadhi ya Green House haziko vizuri, hivyo uzalishaji unakuwa mdogo, jambo ambalo sio lengo la kuanzishwa kwake.

“Tunatakiwa tuhakikishe katika vikundi vyetu tunazalisha bidhaa bora na nyingi na pia tujigawe watano watano, ili tusiwape wavivu fursa ya kujipweteka, hii itasaidia kuzalisha zaidi na kupata kipato kitakachowakwamua na maisha duni”, alisema.

Mkuu huyo aliitaka Wizara inayoshughulika na Vijana ifuatilie kwa ukaribu na kuwaweka vijana pamoja, ili wajiajiri katika kuzalisha bidhaa mbali mbali sambamba na kulidhibiti soko la ndani.

“Ikiwa mutawasimamia vizuri vijana hawa wataweza kuzalisha zaidi na tutalidhibiti soko la ndani kwa sababu itakuwa tuna bidhaa nyingi na zenye ubora”, alisema Mkuu huyo.

Aidha aliwaahidi vijana hao kuwa nao bega kwa bega, kuwahamasisha na kuhakikisha wanafanikiwa katika miradi mbali mbali wanayoianzisha.

“Mdhamini ahakikishe anatatua changamoto za vijana ili wapate maendeleo katika shughuli zao, wapewe elimu ili wawe wabunifu kwani zipo fursa mbali mbali ambazo wakizifanya wanaweza kusonga mbele”, alieleza.

Mapema Ofisa Mdhamini Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Salum Ubwa Nassor alisema, kuna changamoto zinazowakabili vijana waliojikita na ujasiriamali ambazo zinawarudisha nyuma kila siku zinaposonga mbele.

Alisema kuwa, wamekuwa wakifanyakazi kubwa katika kuzalisha bidhaa, ingawa wanapata kipato kidogo ambacho hakikidhi haja, hasa ukizingatia wamekuwa na familia ambazo zinawategemea. 

“Serikali katika kuwajali wananchi wake imejenga Green House nne na visima sita kwa ajili ya kuwasaidia vijana kujiajiri katika shughuli za kilimo, ambapo kila Green House moja imegharimu shilingi milioni 21,191,000/=”, alifahamisha Mdhamini huyo.

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Wilaya ya Micheweni Is-haka Khamis Shaame alisema, wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya maji katika Green House yao ya Shumba Vyamboni, ambapo hutumia kisima cha wanajamii kushota maji, jambo ambalo linasababisha mfarakano.

“Tunahitaji angalau tupate hodhi kwa hatua ya mwanzo kwani tunapata tabu sana, tulikaa pamoja kuzaa wazo hilo lakini tumeshindwa, hivyo tunaomba tusaidiwe saruji”, alisema Mwenyekiti huyo.

Alifahamisha kuwa, iwapo watatatuliwa changamoto zao kwenye miradi waliyoianzisha, watajiajiri wenyewe na wataweza kujikwamua kiuchumi, kwani kilimo kina tija kubwa.

Mkuu wa Mkoa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib alikuwa na ziara ya kukagua miradi ya kimaendeleo katika Mkoa huo kwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo pamoja na Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale.

                                  MWISHO.  

About mmedia

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment