Polisi Kaskazini Pemba yaapa kupambana na udhalilishaji

 


NA ZUHURA JUMA, PEMBA

JESHI la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba limesema, litaendelea kupambana na udhalilishaji, ili kuhakikisha vitendo hivyo vya kikatili vinaondoka katika Mkoa wao.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Ofisini kwake Wete, Kamanda wa Polisi Mkoa huo RPC Juma Sadi Khamis alisema, hawatokuwa tayari kuona watoto wanadhalilishwa huku watendaji wa makosa hayo wakidunda mitaani.

Alisema kuwa, Jeshi la Polisi litaendelea kuchukua juhudi mbali mbali za kupambana na vitendo vya udhalilishaji, kwa kuwachukulia hatua stahiki watendaji wa makosa hayo, ili kuhakikisha kila mmoja anaogopa.

“Ni vyema kabisa wananchi kuacha tabia hizi za udhalilishaji ambazo zinakwenda kinyume na sheria na yeyote atakaefanya hivyo tutaendelea kupambana nae kwa lengo la kuondosha kabisa vitendo hivyo”, alisema.

Alieleza kuwa, wanawake na watoto wanahitaji kuheshimiwa, kuthaminiwa na kutunzwa, jambo ambalo litasaidia kupata vizazi vilivyo bora na vyenye kufuata maadili mema.

Kamanda Sadi alieleza kuwa, wamejipanga ipasavyo kuona jamii inaishi kwa salama, kwani wananchi tayari wameshapata elimu ya kutosha juu ya mambo ya udhalilishaji, hivyo yamepungua kwa kiasi fulani.

“Tunashukuru wananchi wameelewa kutokana na elimu wanayopewa, matukio yamepungua kiasi, tunatumai kumaliza kabisa”, alisema Kamanda huyo.

Hata hivyo aliwataka wananchi kuacha tabia ambazo ziko nje ya maadili, kwani Zanzibar inafuata maadili mema ambayo husaidia kuipeleka jamii pahala pazuri.

About mmedia

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment