Mganga wa Kinyeji afungwa miaka 30 kwa makosa ya Ubakaji

 


NA WAANDISHI WETU, PEMBA

MAHAKAMA ya Mkoa B Chake Chake imemuhukumu mganga wa kienyeji kwenda kutumikia chuo cha mafunzo kwa muda wa miaka 30 na kumlipa muathiriwa fidia ya shilingi milioni moja, baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mke wa rafiki yake.

Mganga huyo aliejulikana kwa jina Issa Abdalla Haji mwenye umri wa miaka 41 mkaazi wa Wawi Chake Chake, amehukumiwa kifungo hicho mara tu baada ya kukubali kosa hilo.

Akisomewa shitaka lake na wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa mashitaka Ali Amour Makame, mshitakiwa huyo alikubali kutenda kosa hilo na kuiomba mahakama impunguzie adhabu.

“Mshitakiwa  ulimbaka mwanamke baada ya kumuaminisha kwamba wewe ni mganga wa kienyeji utakaemfanyia dawa ya kumtoa mume wako ambae yupo rumande anaeshitakiwa katika kesi ya jinai namba 140/2021,  kosa la wizi wa kutumia silaha, jambo ambalo ni kosa kisheria”, alidai mwendesha mashitaka.

Hakimu wa Mahakama hiyo Luciano Makoye Nyengo, baada ya mshitakiwa kukubali kosa lake, alimuamuru kwenda chuo cha mafunzo kwa muda wa miaka 30 na kumlipa muathiriwa fidia ya shilingi milioni moja.

Kwa mujibu wa maelezo ya hakimu huyo, mshitakiwa alikuwa rumande na rafiki yake, ikiwa yeye anakabiliwa na tuhuma za wizi huku rafiki yake akikabiliwa na tuhuma za wizi wa kutumia silaha.

“Walipokuwa rumande rafiki yake alimwambia kwamba, amwambie mke wake akamchukulie dhamana ili na yeye akitoka akamwambie mke wake akamchukulie dhamana”, alisema hakimu huyo.

Alisema kuwa, baada ya mganga huyo kupata dhamana, alikwenda moja kwa moja kwa mke wa rafiki yake na kumwambia akamchukulie mumewe dhamana huku akimpa masharti ya uganga.

“Alimwambia ili mume wako apewe dhamana, lete nywele za sehemu za siri za mbele pamoja na mbegu za kiume, akimaanisha wafanye mapenzi ili wapate hizo mbegu za kiume”, alisema Hakimu.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka ya mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo Oktoba 11 mwaka  huu saa 12:00 jioni Wawi Chake Chake, bila ya halali alimbaka mwanamke baada ya kumuaminisha kwamba atamfanyia dawa ya kumtoa mume wake ambae yupo rumande.

Kufanya hivyo ni kosa kinyume na kifungu cha 108(1), (3),(d), na 109(1) sheria ya adhabu, sheria nambari 6 ya mwaka 2018, sheria ya Zanzibar.

                                                           

About mmedia

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment