Mke wa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar akimkabidhi mwanafunzi wa Madrasatul swabrul-imaan ya mtoni Kidatu wilaya ya magharibi A Unguja ambaye aliibuka mshindi katika mashindano ya kuhifadhi Qur an Juzuu tatu.
MKE wa Makamu wa kwanza
wa Rais wa Zanzibar, Mama Zainab Kombo Shaib, amewataka wazazi kujikita katika
kuwapatia watoto wao elimu ya dini ili kuwajengea mustakbali mwema wa maisha
yao duniani na akhera.
Mama Zainab ameyasema
hayo leo katika mashindano ya kuhifadhi Qurani, yaliyoandaliwa na Madrasat
Swabrul-Imaan ya Mtoni Kidatu wilaya ya Magharib 'A' Unguja na kuzishirikisha
madrasa sita.
Amesema vijana
watakapojengwa katika imani ya dini na kuhifadhi Qurani katika nyoyo zao, dunia
itakuwa sehemu salama kwani watakuwa ni vijana wema wenye kuepuka vitendo viovu
katika jamii.
"Wazazi tuendelee
kushirikiana vyema na walimu wetu ili kuendelea kuuimarisha mustakbali mwema wa
watoto wetu" amenasihi Mke huyo wa Makamu wa Kwanza wa Rais.
Sambamba na hayo
amewataka wazazi kuhakikisha wanatoa vipaombele kwa watoto katika elimu zote na
badala yake sio kuipa nguvu elimu ya dunia wakasahau ile ya kiimani ya akhera.
Amekumbushia pia uwepo
wa vijana wenye elimu ya dini na imani kutapelekea kuzalisha viongozi bora
katika familia na Taifa kwa ujumla, kwakusema " Hata kiongozi wa dini yetu
ya kiislamu Mtume Muhammad (S.A.W) alitakiwa na Mola wetu kusoma jambo
lililomfanya aweze kuitangaza dini ya kiislamu hali ya kuwa ana elimu
nayo".
Aidha amewataka waalimu
kuendelea kuchukua jitihada zaidi ili watoto hao waweze wakuingia katika
mashindano makubwa ikiwemo kuiwakilisha Nchi katika ngazi ya kimataifa.
Naye mlezi wa madrasa
hio Dokta Abubakar Makame Hafidh, akimkaribisha mgeni rasmi amesema,
maendeleo makubwa ya wanafunzi na
madrasa hio yatapatikana kutokana na jitihada na mashirikiano ya wazazi na
waalimu.
Akisoma risala ya
madrasa hio yenye wanafunzi takriban 250, mwanafunzi Salama Bakari Ali, amesema
moja ya malengo ya madrasa hio ni kuzalisha viongozi bora katika jamii, pamoja
na kueleza changamoto zao.
Miongoni mwa
changamoto zilizoainishwa ni pamoja na
kukosa tenki la maji ambalo linatoa huduma kwa jamii, ufadhili wa kuwasaidia
watoto yatima waliopo katika madrasa hio, kukamilisha matengenezo ya jengo lao
la madrasa kwa hatua ya plasta, mazulia kwaajili ya vikalio pamoja na
kukosekana kwa zawadi za kuwazawadia washindi yanapotokea mashindano kama haya
ya kuhifadhisha Quran, pamoja na kumtaka Mama Zainab kuwasaidia kuwatafutia
misaada.
0 Comments:
Post a Comment