Ili kuepuka maafa, tusitoe zabuni kwa upendeleo na ‘Ten Parcent’

 

Salum Vuai

Salum Vuai


“Kwa pamoja tunaweza kuikoa dunia dhidi ya maafa”. Hii ni kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Maafa Kimataifa ambayo iliadhimishwa jana Oktoba 13, duniani kote.

Maadhimisho ya siku hii ni utekelezaji wa Azimio Na. 64/200 lililopitishwa na Baraza la Umoja wa Mataifa tarehe 21 Disemba, 2009.

Siku hii inalenga kukuza utamaduni wa usimamizi wa maafa kimataifa, ikiwa ni pamoja na kuzuia, kupunguza madhara, kujiandaa, kukabili na kurejesha hali katika ubora zaidi pale maafa yanapotokea.

Katika kuadhimisha siku hii, Sekretarieti ya Upunguzaji wa Madhara ya Maafa ya Umoja wa Mataifa (United Nation Strategy for Disaster Reduction–UNISDR) hutoa kaulimbiu ya mwaka husika.

Katika tafakuri yake wiki hii, Muhenga anauliza je, ni wangapi wako tayari kushirikiana na wengine kwa kutoa mchango wa dhati katika kuhakikisha dunia inakuwa mbali na maafa?

Yumkini wanaotaka mafanikiio katika hili ni watu wote katika kila nchi, lakini wasiwasi wa Muhenga ni kwamba miongoni mwao wapo wasiokuwa na dhamira ya kweli katika kuifanya  dunia iwe pahala salama pa kuishi.

Bila shaka wapo wanaoangalia zaidi masahi yao binafsi kwa tamaa ya kujitengenezea fedha ili kujijengea utajiri.

Watu kama hao wako tayari kuisaliti nchi kwa kufanya vitendo vinavyoangamiza rasilimali za taifa ili mradi wanajaza fedha katika makasha yao.

Wapo ambao kukitungwa sheria za kulinda na kutuza mazingira wao hupiga kofi na kushangiria mchana, lakini usiku hugeuka wachawi wa kuyaharibu.

Pengine miongoni mwa waharibifu wakubwa wa mazingira na rasilimali nyengine za nchi kama vile misitu, bahari na mchanga, ni watendaji wanaopewa dhamana kwa kuaminiwa kuyalinda ili kuiepusha nchi na janga.     

 

Na haoa ndipo Muhenga anapoona iko haja kwanza kupambana na TABIA WATU na baadae tugeukie kulaumu tabianchi, kwa sababu maafa mengi yanayitijkea nchini chanzo chake ni mikono ya binadamu inayoambatana na utashi wa kujikumbia kila kitu hata kwa kuwadhuru wengine.

Mathalan, ujenzi wa miundombinu  isiyokuwa na viwango stahili ambayo baaade kuleta maafa na majanga, chanzo chake ni kugawa zabuni kwa upendeleo na kujuana.

Katika miaka hii kampuni nyingi za ujenzi pamoja na mafundi binafsi, wanaibuka na kujitangaza kuwa wao ni mahiri katika kazi hizo na kuomba zabuni mbalimbali.

Kwa bahati mbaya, mara kadhaa imewahi kuripotiwa wakandarasi kupokonywa kazi walizopewa kwa mikataba kabla kuzikamilisha baada ya kubainika hazina viwango.

Lakini baya zaidi, ni pale mkandarasi anapomaliza kazi na kuikabidhi kwa mteja (Hapa nazungumzia zaidi serikali), lakini baada ya muda mfupi ikadhihirisha ubovu, huku akiwa ameshatia hasara ya mamilioni kama si mabilioni ya fedha. 

Aidha, mara nyengine miundombinu isiyokuwa imara hutokana na ujanja wa baadhi ya watendaji wanaoongozwa zaidi na tamaa binafsi, kwa kuwapa kazi waomba zabuni wasiokuwa na sifa ili mradi wameahidiwa asilimia kadhaa ya fedha.

Ni ukweli usio shaka kwamba rushwa imekuwa chanzo kikubwa cha matatizo mengi yanayotokea kwenye miundombinu, na kwa bahati mbaya hata inapobainika hakusikiki hatua madhubuti zinazochukuliwa ili hali kama hiyo isijitokeze tena.    

Kwa mfano, ujenzi wa barabara, madaraja, majengo ya taasisi kama vile skuli, hospitali na ofisi nyengine mbalimbali, umekuwa ukikwangua mno hazina ya serikali huku thamani ya fedha zilizotumika ikiwa haionekani.   

Kupitia tafakuri hii, Mujega anashauri, ili tuwe na miundombinu imara itakayodumu kwa miaka mingi na kukomesha maafa yanayoweza kuepukika, ni lazima serikali inoe meno yake maradufu ili kuwafanya wasimamizi wa shughuli za ujenzi wa majengo na miundombinu yetu wawajibike ipasavyo.

Aidha mtindo wa kuchagua washindi wa zabuni za serikali kwa misingi ya usahibu na udugu nao usipewe nafasi kwani ndio unaosababisha maafa yasiyotarajiwa. 

Kwa upande wa wananchi ambao ndio waathirika wakubwa wa majanga yakiwemo ya kimaumbile, nao hawana budi kuzingatia maeneo salama ya kujenga nyumba za makaazi na wasiwe watumwa wa shida walizonazo kwa kujenga popote hata kwenye njia za maji au mabondeni.

Kwa hakika ujenzi holela na katika maeneo hatarishi, umekuwa chanzo cha nyumba na majengo ya taasisi kujaa maji na kuwafanya wakaazi wawe watu wa kuhama na kurudi kila msimu wa mvua unapofika na kumalizika. 

Lakini hili la ujenzi wa nyumba za makaazi, serikali na Idara zake zisingoje mpaka watu wamejenga katika maeneo hatarishi kisha kuwabomolea wakati walifuata taratibu zote za kupata viwanja na vibali vinavyowaruhusu kujenga.

Iwapo inaamua kuwahamisha watu waliojenga mabondeni au kwengineko kusikoruhusiwa, basi pia iwawajibishe maofisa wanaobariki ujenzi huo kwa kuwachukulia hatua stahiki.

Halikadhalika, shughuli za ujenzi zifanyike kwa kutumia wataalamu waliosajiliwa na Bodi ya Usajili wa Wabunifu na Wakadiriaji wa Majengo badala ya kuachia kila anayeweza kushika kijiko ajenge. 

Ni dhahiri kwamba kuchukua hatua katika suala hili kutaonesha kwamba kuna mikakati katika ngazi ya taifa, mkoa, wilaya na shehia inayolenga usimamizi wa kudhibiti maafa hapa nchini.

Jambo hili ni changamoto kubwa ambayo inaweza kutatuka endapo kutakuwa na ushirikiano na uratibu mzuri baina ya wadau mbalimbali. 

Simu: 0777865050/0714425556

Baruapepe:salumss@yahoo.co.uk

About mmedia

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment