Tuwashajiishe watoto wa kike walioacha masomo kurudi skuli

 


Na Salum Vuai

TAARIFA ya wafadhili wa  mradi unaolenga kuwarudisha skuli watoto wa Zanzibar walioacha masomo kwa sababu mbalimbali kwamba bado idadi ya wanawake ni ndogo, inahitaji kukaliwa kitako na kufanyiwa kazi.

Wakati Zanzibar chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ikiwa katika hekaheka za maadhimisho ya Elimu bila Malipo, ni jambo la faraja kuwa shughuli hiyo inakwenda sambamba na mradi wa kuwarudisha skuli watoto walioko nje ya madarasa.  

Kwa namna ya pekee, kupitia tafakuri hii Muhenga analipongeza Shirika la UNICEF pamoja na taasisi inayoshughulikia masuala la elimu kwa wote, EAC kutoka nchini Qatar kwa kuleta mradi huo wa miaka mitatu hapa Zanzibar.

Sio siri kuwa tunao vijana wengi waliolazimika kukatisha masomo kwa sababu mbalimbali na wazazi au walezi wao kushindwa kuwahimiza, lakini sasa wanajuta na kutamani kuipata tena nafasi waliyokuwa wameipoteza.

Hata hivyo,  pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Wizara kuhakikisha mradi huo unafanikiwa kikamilifu, iko haja kwa jamii, wazazi na walezi wa  watoto husika kuona umuhimu wa fursa hiyo na kuitumia ipasavyo.

Mradi huo unaolenga kuwafikia wanafunzi 35,732 katika wilaya zote Unguja na Pemba, ni fursa adhimu inayopasa kupokelewa kwa mikono miwili na wazazi pamoja na vijana wenyewe kujikubalisha kurudi skuli ingawa wengine wameshakuwa wakubwa.

Taarifa za Wizara ya Elimu zinaeleza kuwa zaidi ya wanawake 16,000 kati ya idadi iliyotajwa, ni miongoni mwao, lakini kasi yao ya kurudi hadi sasa imekuwa ya kusuasua.

Ni kweli kwamba kwa maumbile yake, mtoto wa kike akikatisha masomo na kupita muda mrefu akiwa nje, pengine wazazi wamempa mume na Mungu akamjaalia mtoto/watoto, suala la kurudi skuli kwake linakuwa gumu.

Akirudi darasani ambako kuna mchanganyiko wa wanafunzi wa umri tafauti wanaoangaliwa uwezo wao kabla kutawanywa kwenye madarasa mengine mbalimbali kulingana na umri na ufahamu wao, mwanamke anaweza kuona aibu hasa akiwa amezungukwa na watoto wadogo.

Tuwaambie umri usiwe kikwazo, kwani hata wazee wetu waliokosa elimu kabla ya Mapinduzi, baadae  walikuwa wakisoma madarasa ya jioni yaliyokuwa yakiendeshwa katika matawi ya Chama cha Afro Shirazi (ASP) kabla ya kuungana na TANU cha Tanzania Bara Febuari 1977 kuunda CCM.

Elimu hiyo ya watu wazima, angalau wajue kusoma, kuandika na kuhesabu.

Aidha, katika kuwatengenezea fursa za kujiendeleza vijana walioacha masomo kabla kuhitimu elimu ya lazima, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeunda Idara ya Elimu Mbadala ili kuwapa taaluma na stadi mbalimbali za maisha inayoweza kuwasaidia kuajirika au kujiajiri wanapohitimu.

Jamii yote inapaswa kuunganisha nguvu ili kuhakikisha kati ya vijana wote 35,732 waliolengwa na mradi huu, hakuna anayeachwa nyuma awe mwanamme au mwanamke.

Na inapohusu wanawake, hata taasisi za kiraia na wanaharakati wanaoshughulikia ustawi wa vijana na wanawake, waangalie namna wanavyoweza kutoa mchango wao katika kuwasukuma wanawake wasione aibu kurudi skuli.

Taasisi kama TAMWA, BIWO, ZAFELA na  jumuiya zote za vijana, ziungane kuisaidia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuwahamasisha watoto wetu kurudi masomoni.

Katika hili, ninawapongeza wafadhili wa mradi huu pamoja na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, kwa ubunifu wao wa kuwapatia nyenzo na vifaa vyote vinavyohitajika vijana wanaorudi skuli ili kuwaongezea hamu ya kubaki madarasani na kusoma.

Inafurahisha kuwa, mbali na vifaa  vya kujifundishia darasani, pia wanapewa vifaa vya michezo kwa kadiri wanavyohitaji ili kuwazoesha mazingira ya kurudi kuwa wanafunzi, ambayo walikwisha kuyasahau.

Kwa namna hii, ninaamini lengo litafikiwa na mradi utakapomalizika mwaka 2023, sote tutajumuika kufurahia matunda yake.


Kwa maoni na ushauri 

0777 865050/0714 425556

mbumbwinihalisi@gmail.com

 

About mmedia

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment