Na Sabiha Khamis Maelezo
Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar (SMZ) imesema itashirikiana na Jumuiya ya Uchunguzi wa Vinasaba vya
Binaadamu ili kugundua maradhi yanayotokana na vinasaba hivyo ili kuyapatia
ufumbuzi.
Aliyasema hayo Waziri
wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui hayo huko
Ofisini kwake Mnazi Mmoja, wakati alipotembelewa na Ujumbe kutoka katika
Jumuiya ya Vinasaba vya Binaadamu Tanzania, amesema maradhi mengi sana
yanasababishwa na vinasaba ikiwemo maradhi ya Urithi.
Alisema maradhi ya
vinasaba huanza kuwapata watoto kutokana na jamii kushindwa kuyagundua mapema
kwa sababu ya ukosefu wa elimu ya kuyajua na kuyapatia ufumbuzi bila ya
kuwaathiri.
Alieleza Jumuiya hiyo
inafanyakazi sehemu mbali mbali ya kuchunguza vinasaba vya binaadamu, hivyo
serikali imejipanga kuimarisha zaidi kitengo cha uchunguzi kilichopo Binguni na
kudumisha ushikiano baina yao ili kupata uzoefu.
“Ipo haja ya
kushirikiana nao kwani kutaleta maendeleo ya nchi kwa haraka kwani kwenye Afya
bora ndio kwenye maendeleo, pia wanauzoefu mkubwa kuhusiana na vinasaba vya
binaadamu hivyo watapata kupeana elimu na ujuzi zaidi watakapofanyakazi
Zanzibar”, alisema Waziri.
Aidha Waziri Mazrui
alisema wamefurahishwa na ujio huo wenye lengo la kuleta mashirikiano na
maendeleo katika sekta ya afya nchini.
Kwa upande wake Rais
wa Jumuiya ya uchunguzi wa Vinasaba vya Binaadamu Dk. Siana Nkea ameipongeza Wizara ya Afya kwa mashirikiano na
mapokezi waliyoyapata na kuonesha utayari wa kufanyakazi ya kuchunguza vinasaba
vya binadamu ili kuyagundua na kuyapatia ufumbuzi maradhi hayo.
Alifahamisha Jumuiya
hiyo imejipanga kufanya uchunguzi ili kugundua maradhi yanatokanayo na vinasaba
vya binaadamu kwa lengo la kuimarisha afya za wananchi pamoja na kutoa elimu
kuhusiana na maradhi yatakayogunduliwa.
Dk. Siana alifahamisha
kuwa Jumuiya hiyo inatarajia kufungua tawi Zanzibar kwa lengo la kusaidia jamii
na kubadilishana ujuzi kuhusiana na maradhi yanayotokana na vinasaba pamoja na
kujikinga na maradhi hayo mapema.
0 Comments:
Post a Comment