Othman awataka mabalozi kutumia taasisi za kimataifa kuleta maendeleo

Makamu wa kwanza wa rais wa Zanzibar  Othman Masoud Othman akizungumza na Mabalozi wa Tanzania walioteuliwa hivi karibuni. Kulia kwa Mhe. Makamu ni Balozi wa Tanzania nchi Itali Mhe. Mahmoud Thabiti Kombo na Balozi wa Tanzania nchini Uturuki  Luteni Genrali Y. H. Mohammed. Mabalozi hao walifika ofisini kwa makamu Migombani kubadilishana mawazo pamoja na kumuaga kuelekea kwenye vituo vyao vya kazi. ( Mpiga Picha Maalum)



MAKAMU  wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, amesema changamoto inayoikabili Tanzania, kama ilivyo kwa nchi nyingine za Afrika, ni kuchelewa kutumia fursa kupitia Jumuiya na Taasisi za Kimataifa katika kujiletea maendeleo.

 

 Othman aliyasema hayo leo Ofisini kwake Migombani Jijini hapa, alipokutana na Mabalozi sita waliofika kujitambulisha na kumuaga kabla ya kuelekea vituo vyao vya kazi, katika Mataifa mbali mbali, ndani na nje ya Afrika.

 

Alisema zipo fursa nyingi muhimu kupitia jumuiya na taasisi mbali mbali za kimataifa, zikiwemo za kujiletea maendeleo na kujikwamua, bali ushiriki wa Tanzania na Afrika kwa ujumla ni mchache, au hakuna kabisa, na inabaki kuwa changamoto.

 

Othman ambaye aliwahi kuwa Mwakilishi wa Afrika katika Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusiana na Haki Miliki (‘World Intellectual Property Organization’ (WIPO), amebainisha fursa hizo kuwa ni pamoja na maendeleo ya teknolojia, ushindani wa kibiashara na uwekezaji.

 

“Naelewa changamoto kubwa iliyopo, lakini ni vyema tukaelewa kuwa kwa sasa ulimwengu hauelekezi nguvu zake zaidi upande wa mapambano ya kijeshi, bali vita kubwa iliyopo ni ya teknolojia katika kuhamasisha maendeleo ya kiuchumi”, alisema  Othman.

 

Makamu huyo aliwanasihi Mabalozi hao kuzidi kujitolea na kutumia kila juhudi katika kujenga mahusiano mema yatakayowezesha kuibua fursa ambazo kwa kiasi kikubwa zinahitajika katika jamii pamoja na serikali za mitaa, na wala siyo katika kujikita kujenga mahusiano na Serikali Kuu pekee.

 

“licha ya kuwatakia kila la heri katika utekelezaji wao wa majukumu, ameeleza imani yake kwa Mabalozi hao akiamini kuwa mafanikio yao ndiyo heshima ya nchi, na pia kufanikiwa kwa Taifa hili na watu wake” alieleza Othman.

 

Naye Kiongozi wa Kundi la Mabalozi hao, Mahmoud Thabit Kombo, aliyeteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Italy, ameeleza changamoto ya vikwazo vya mawasiliano katika uzoefu wa kidiplomasia, hali inayokwaza azma ya miradi ya maendeleo na inayowakatisha tamaa baadhi ya wawekezaji.

 

Balozi Mahmoud ameahidi kuwa yeye na wenzake watajitahidi kwa hali na mali kuzikabili changamoto hizo, na hawatosita kuomba msaada kupata busara kutoka kwa Othman kila inapobidi, ili kuzichuma fursa katika Mataifa wanayokwenda kuiwakilisha Tanzania, kwaajili ya maendeleo ya nchi na Taifa kwa ujumla.

 

Wengine katika kundi la Mabalozi hao na vituo vyao vya kazi ni pamoja na Meja Jenerali Richard Makanzo (Rwanda), Hoyce Anderson Temu (Switzerland), Grace Alfred Olotu (Sweden), Elsie Sia Kanza (Marekani) na Luteni Jenerali Mohamed Yussuf (Uturuki).

 

Waliojumuika na ujumbe huo ni pamoja Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa Zanzibar, Balozi Masoud Abdalla Balozi.

 

About mmedia

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment