Katibu Mkuu OMKR Dkt Omar D. Shajak akimkabidhi vifaa
vinavyotumika kwa ajili ya kuendeshea kiti kisaidizi Bi Zahra Wazir Said
ambae ana ulemavu wa viungo. |
Raya Hamad - OMKR
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais Dkt Omar
D Shajak amemkabidhi kiti cha magurudumu mawili chenye kutumia chaji(motor
wheel chair) Bi Zahra Waziri Said wa Skuli ya Sayansi na Tiba Mbweni Chuo kikuu cha
Suza anaechukuwa Stashahada ya Famasia mwaka wa pili.
Akimkabidhi kiti kisaidizi hicho Dkt Shajak amesema kuwa
kitamsaidia Zahra katika shughuli zake za masomo na kurahisisha majukumu yake
mengine kiutendaji pamoja harakati zake za kwenda na kurudi chuoni na
kwengineko.
Dkt Shajak amefarijika na uwezo wa Zahra na kusema
kuwa ni mfano mzuri wa kuigwa kwani kila binaadamu anauwezo wake hivyo Ulemavu
wake sio sababu ya kumfanya mtu kukosa fursa muhimu za amali
“huu ni mfano mwema na kigezo kizuri cha wengine
waweze kuiga mfano wako na kujuwa kuwa Mwenyezi Mungu akikupa ulemavu wowote
sio kama umekosa fursa nyengine kwani Watu wenye ulemavu wakirahisishiwa
mazingira yao wanafanya vizuri zaidi”
Katibu Shajak amesema Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa
Rais kupitia Baraza la Watu wenye Ulemavu itaendelea kuratibu na kusaidia Watu
wenye Ulemavu waweze kusoma katika mazingiramepesi na wale wanaofanya kazi pia
na wao wafanye kazi zao katika mazingira rafiki
Nae Zahra Waziri Saidi ameishukuru Ofisi ya Makamu wa
Kwanza wa Rais kupitia Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu kwa kumpatia kiti
kisaidizi hicho “MotorWheelchair” ambachoaliihitaji kwa muda mrefu sana na
kuahidi atakitunza vyema.
Aidha amewashukuru wale wote waliojitahidi na
kuhakikisha anapata kiti kisaidizi kwa ili kurahisisha majukumu yake ya masomo
na harakati za kujiendeleza
Mkurugenzi Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu Inginia
Ussy Khamis Debe kupitia Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais amesema Barazalitahakikisha
kwamba Watu wenye Ulemavu wanapata fursa sawa za elimu, afya na Mambo mengine
ya kijamii hasa ya kujiendesha kimaisha.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inadhamira njema kwa
wananchi wake wote na imeweka mazingatio kwa Watu wenye Ulemavu kuona wanapata
fursa sawa ya kielimu na fursa nyengine za kijamii ukiwemo uwezeshaji na Miundo
mbinu Rafiki ili waweze kujimarisha
kiuchumi.
Kiti kisaidizi kimetolewa na Baraza la Taifa la Watu
wenye Ulemavu kina thamani ya shilingi za Kitanzania Milion tatu ambapo
makabidhiano hayo yamefanyika kwenye viwanja vya Ofisi ya Makamu wa Rais
Migombani, Mjini Zanzibar
0 Comments:
Post a Comment