| Salum Vuai,mwandishi wa ukurasa huu wa Tafakuri ya Muhenga ambayo inakujia hapa kila siku ya Alhamis |
KUKOSEKANA kwa dhamira ya dhati miongoni mwa
Wazanzibari hasa walioko kwenye uongozi, kumekuwa kukiigharimu sana Zanzibar na
kukwamisha juhudi zake za kujiletea maendeleo.
Watu wengi
wamejenga dhana potofu kwamba mtu kuteuliwa kushika nafasi ya uongozi, au
kupata kazi katika taasisi kubwa na nyeti hasa za kifedha, ni njia ya ‘kuukata’
kimaisha kama vijana wanavyosema.
Na kwa sababu
hiyo, watu wako tayari kuuza utu wao kwa kufanya mambo yanayoweza kudhoofisha
mustakbali wa taifa, ili mradi wao wanatia ndani fedha kwa manufaa yao binafsi.
Watu kama hao
hawajali kabisa kama utashi wao unaweza kuliingiza taifa katika maafa makubwa
ya maradhi yasiyoponeka, uchumi duni, vizazi vyetu kudumaa kiakili na kukosa
maarifa ya kujiendesha wao na nchi yao na mengi kama hayo.
Hivi karibuni,
Mkoa wa Mjini Magharibi ulitikishwa na taarifa za kushikwa kwa vijana
wanaotengeneza vyeti na nyaraka bandia za aina mbalimbali.
Shukurani na
pongezi nyingi ziende kwa viongozi wakuu wa Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) kwa
kuwagundua mapema wahalifu hao na kuliarifu Jeshi la Polisi na Mkuu wa Mkoa
kwa hatua zaidi.
Wahalifu wao
walibainika baada ya Jeshi la Polisi Tanzania kutangaza nafasi za ajira, ambapo
walifumwa wakitengeneza vyeti vya kuhitimu elimu ya sekondari na mafunzo ya JKU
ili kuwawezesha waomba kazi kupitishwa.
Katika tafakuri yake, Muhenga anaona kuwa mtandao huu wa wahalifu wa kughushi nyaraka ni mkubwa na haukuanza leo wala jana.
Hivyo ni dhahiri mtandao huu umeshawanufaisha watu
wengi hasa vijana kwa kuajiriwa katika taasisi mbalimbali za serikali na
binafsi bila kushtukiwa, au pengine wanafumbiwa macho tu kwa kuwa ni miongoni
mwa ‘Ibn Vinana’.
Kwa namna hii,
kuwepo maeneo ambako watu wameweka vifaa vya kuchapisha vyeti feki na nyaraka
nyengine muhimu, kunatoa indhari kwamba nchi hii imejaa ghishi katika kila
ofisi na sekta.
Kilio cha
kuzorota utendaji kazi maofisini na wananchi kutokuona matokeo chanya, huenda
ni zao la ajira zinazotolewa kwa wenye vyeti bandia vya elimu ambao hawana
chochote wajuacho kuhusiana na kazi wanazoziomba au kuajiriwa kwazo.
Kwa watu
wanaotazama kwa jicho la tatu wakiwemo wanahabari, ni wazi wanaona mambo
yanakwenda shaghala baghala tu, na hilo linajibainisha wazi katika nyuso zao
zilizopoteza matumaini.
Kila siku
kumekuwa kukiongezeka manung’uniko ya wananchi wanaotarajia makubwa kutoka kwa
watoa huduma na viongozi wa kisekta, kwa kuwa hawaoni matunda wanayoyatarajia,
kumbe vyeti feki ndio sababu ya yote hayo.
Muhenga hana
maana kwamba watendaji wote wanahodhi vyeti vya kughushi, lakini ni lazima
turudi katika msemo wa Kiswahili, “Nazi mbovu harabu ya nzima”.
Yumkini walio na
vyeti halali wanajitahidi kufanya kazi vizuri kwa mujibu wa taaluma zao, lakini
jitihada zao zinakumbana na vikwazo kutoka kwa walioingia makazini kwa njia
haramu zilizoambatana na ghishi, hivyo wote kuonekana ni jora moja.
Kwa utendaji wa
aina hii, ndipo tunaposikia katika hospitali za nchi nyengine (Kwa kutolea
mfano), mgonjwa wa kupasuliwa mguu anafanyiwa upasuaji wa kichwa na kinyume
chake.
Na kwa kuwa mtu
huvuna alichopanda, kama hakujatumika nguvu za ziada kukomesha ghilba hizi,
tujiandae kushuhudia taifa lililojaa kizazi ‘mbumbumbu huko tuendako.
Simu: 0777 865050/0714 425556
Baruapepe: mbumbwinihalisi@gmail.com
Hongera mwandishi mbobezi kwa makala nzuri na yenye mashiko, Nimekuelewa
ReplyDeletesawa
ReplyDeleteKaribu sana usiache kusoma kila Alhamis
ReplyDelete