Kwa tamaa zetu tunatengeneza taifa ‘mbumbumbu’

 

Salum Vuai,mwandishi wa ukurasa huu wa Tafakuri ya Muhenga ambayo inakujia hapa kila siku ya Alhamis

 

KUKOSEKANA kwa dhamira ya dhati miongoni mwa Wazanzibari hasa walioko kwenye uongozi, kumekuwa kukiigharimu sana Zanzibar na kukwamisha juhudi zake za kujiletea maendeleo.

Watu wengi wamejenga dhana potofu kwamba mtu kuteuliwa kushika nafasi ya uongozi, au kupata kazi katika taasisi kubwa na nyeti hasa za kifedha, ni njia ya ‘kuukata’ kimaisha kama vijana wanavyosema.

Na kwa sababu hiyo, watu wako tayari kuuza utu wao kwa kufanya mambo yanayoweza kudhoofisha mustakbali wa taifa, ili mradi wao wanatia ndani fedha kwa manufaa yao binafsi.

Watu kama hao hawajali kabisa kama utashi wao unaweza kuliingiza taifa katika maafa makubwa ya maradhi yasiyoponeka, uchumi duni, vizazi vyetu kudumaa kiakili na kukosa maarifa ya kujiendesha wao na nchi yao na mengi kama hayo.

Hivi karibuni, Mkoa wa Mjini Magharibi ulitikishwa na taarifa za kushikwa kwa vijana wanaotengeneza vyeti na nyaraka bandia za aina mbalimbali.

Shukurani na pongezi nyingi ziende kwa viongozi wakuu wa Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) kwa kuwagundua mapema wahalifu hao na kuliarifu Jeshi la Polisi na Mkuu wa Mkoa kwa  hatua zaidi.

Wahalifu wao walibainika baada ya Jeshi la Polisi Tanzania kutangaza nafasi za ajira, ambapo walifumwa wakitengeneza vyeti vya kuhitimu elimu ya sekondari na mafunzo ya JKU ili kuwawezesha waomba kazi kupitishwa.

Katika tafakuri yake, Muhenga anaona kuwa mtandao huu wa wahalifu wa kughushi nyaraka ni mkubwa na haukuanza leo wala jana.

Hivyo ni dhahiri mtandao huu umeshawanufaisha watu wengi hasa vijana kwa kuajiriwa katika taasisi mbalimbali za serikali na binafsi bila kushtukiwa, au pengine wanafumbiwa macho tu kwa kuwa ni miongoni mwa ‘Ibn Vinana’.

Kwa namna hii, kuwepo maeneo ambako watu wameweka vifaa vya kuchapisha vyeti feki na nyaraka nyengine muhimu, kunatoa indhari kwamba nchi hii imejaa ghishi katika kila ofisi na sekta.

Kilio cha kuzorota utendaji kazi maofisini na wananchi kutokuona matokeo chanya, huenda ni zao la ajira zinazotolewa kwa wenye vyeti bandia vya elimu ambao hawana chochote wajuacho kuhusiana na kazi wanazoziomba au kuajiriwa kwazo.

Kwa watu wanaotazama kwa jicho la tatu wakiwemo wanahabari, ni wazi wanaona mambo yanakwenda shaghala baghala tu, na hilo linajibainisha wazi katika nyuso zao zilizopoteza matumaini.

Kila siku kumekuwa kukiongezeka manung’uniko ya wananchi wanaotarajia makubwa kutoka kwa watoa huduma na viongozi wa kisekta, kwa kuwa hawaoni matunda wanayoyatarajia, kumbe vyeti feki ndio sababu ya yote hayo.

Muhenga hana maana kwamba watendaji wote wanahodhi vyeti vya kughushi, lakini ni lazima turudi katika msemo wa Kiswahili, “Nazi mbovu harabu ya nzima”.

Yumkini walio na vyeti halali wanajitahidi kufanya kazi vizuri kwa mujibu wa taaluma zao, lakini jitihada zao zinakumbana na vikwazo kutoka kwa walioingia makazini kwa njia haramu zilizoambatana na ghishi, hivyo wote kuonekana ni jora moja.

Kwa utendaji wa aina hii, ndipo tunaposikia katika hospitali za nchi nyengine (Kwa kutolea mfano), mgonjwa wa kupasuliwa mguu anafanyiwa upasuaji wa kichwa na kinyume chake.

Na kwa kuwa mtu huvuna alichopanda, kama hakujatumika nguvu za ziada kukomesha ghilba hizi, tujiandae kushuhudia taifa lililojaa kizazi ‘mbumbumbu huko tuendako.

 

Simu: 0777 865050/0714 425556

Baruapepe: mbumbwinihalisi@gmail.com  

About mmedia

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

3 Comments: