![]() |
| Katibu Mkuu Afisi ya makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar Dk. Omar Dad Shajak |
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa
Kwanza wa Rais Dkt Omar D. Shajak ameitaka Tume ya UKIMWI Zanzibar kukabiliana
vyema na mazingira ya sasa kwa kutumia mbinu na kuibua mawazo mapya ambayo
yatazidisha mapambano dhidi ya maambukizi ya UKIMWI.
Dkt Shajak ameyasema hayo alipofanya
mazungumzo na viongozi pamoja na watendaji wa Tume ya UKIMWI ambapo amesisitiza
kuwa jitihada zinazofanyika sasa katika kukabiliana na maambukizi ya UKIMWI
yaende mbali zaidi kwa vile dunia hivi sasa nguvu kubwa imewekezwa kwenye
kupambana na virusi vya Korona.
Amesema ugonjwa wa Korona
umeipelekea jamii kujisahau kama ugonjwa wa UKIMWI bado upo hivyo Tume ya
UKIMWI iendelee kuchukuwa nafasi yake katika kuelimisha jamii na kuhakikisha
hakuna maambukizi mapya ya VIRUSI vya UKIMWI ifikapo 2025.
“juhudi zetu zilenge mafanikio na
kufikiria njia mbadala za kutatua matatizo yaliyopo, mpango mkakati wa nne ni
vyema sasa ukaangalia mawazo mapya yatakayotuvusha hapa tulipo ili tuondokane
na maradhi ya UKIMWI” alisisitiza.
Nakueleza kuwa lengo la kupunguza na
kuondokana na idadi ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka kawa mama kwenda
kwa mtoto linafikiwa, Vijana na makundi maalum kufikiwa katika kupewa elimu,
wenye mahitaji kupatiwa dawa na tiba sahihi.
Nae Mkurugenzi mtendaji Tume ya
UKIMWI Dkt Ahmeid M. Khatib amemuelezea Katibu Mkuu kuwa katika kufikia malengo
ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Tume inawajibu wa kutayarisha mkakati maalum
na wadau wote wanajukumu la kuufuata mkakati huo.
Tume ya UKIMWI inaendelea na
matayarisho ya Mkakati wa nne wa UKIMWI utaogusa sekta zote kama taasisi za
Serikali ama binafsi pamoja na jamii kwa vile wadau wote ni wa mapambano ya
UKIMWI na hivyo ni wajibu wa kila anaeguzwa kuhakikisha malengo ya nchi na
dunia yanafikiwa.
Amesema mafanikio yaliyopatikana
katika kudhibiti maradhi ya UKIMWI yamepelekea Zanzibar kufikia chini ya
asilimia moja ya kiwango cha maambukizi ambapo nchi chache zimeweza kufikia
malengo haya na kuifanya Zanzibar iwe ni moja kati ya nchi zenye mafaniko.
Dkt Ahmeid amesema hadi kufikia
mwaka 2020 malengo na shabaha za dunia ni kuhakikisha kuna 90 tatu ambazo
zinafikiwa, na Zanzibar imefanikiwa kufikia asilimia 90 na amehakikisha
asilimia 90 ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI wanaojitambuwa ni asilimia
94, wanaojitambua na wanaotumia dawa za kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI
ni asilimia 98 na wanaotumia dawa ambao wameweza kuvishusha virusi ndani ya
mwili ni asilimia 93.
Wakitoa maoni yao wafanyakazi wa
Tume ya UKIMWI wameiomba Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kutoa msukumo
kwa Serikali kwa baadhi ya taasisi kuendelea kuunga mkono juhudi za mapambano
ya maradhi ya UKIMWI kwani hakuna taasisi ambayo haijaguswa na changamoto ya
maradhi ya UKIMWI.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa
Kwanza wa Rais alieongozana na Mkurugenzi Mtendaji Tume ya UKUMWI na kufanya
mazungumzo na Mwenyekiti wa ZAYEDESA Mama Shadya Karume kisha kutembelea kituo
rafiki wa vijana na huduma za afya kilichopo Miembeni pamoja na kutembela Kituo
cha Programu ya shirikishi ya UKIMWI, homa ya ini, kifua kikuu na ukoma.
Aidha Dkt Shajak amezishukuru taasisi
zinazojishughulisha na mapambano dhidi ya UKIMWI na kuahidi Ofisi ya Makamu wa
Kwanza wa Rais kupitia ZAC itaendelea kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja
na wadau wote wa mapambano ya UKIMWI ili lengo lililowekwa na Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar liweze kufikiwa.
Lengo la ziara hio ni kuona
yanayoendelea kwenye vituo hivyo, changamoto wanazokabiliana nazo na namna ya
kuzitatua ikiwa ZAC ndio mratibu wa masuala ya UKIMWI ili kujenga ufanisi
katika kutoa huduma bora dhidi ya mapambano ya UKIMWI.

0 Comments:
Post a Comment