Mwandishi wetu,Arusha
Watu watano wamefariki dunia huku mmoja akijeruhiwa katika ajali iliyotokea baada ya magari mawili kugongana uso kwa uso katika Barabara Kuu ya Arusha-Moshi, eneo la King'ori wilayani Arumeru,mkoa wa Arusha.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha,ACP Justine Masejo,imesema ajali hiyo imetokea Jana majira ya saa 10 alfajiri katika barabara Kuu ya Arusha-Moshi,eneo la Konoike,Kijiji cha Kolila kilichopo Tarafa ya King'ori.
Taarifa hiyo imesema ajali hiyo ilitokea baada ya magari mawili kugongana uso kwa uso ambapo gari lililokuwa na namba za usajili T 111 CUU aina ya Mitsubish Fuso lililokuwa linaendeshwa na Heriel Lyimo(42)mkazi wa Holili,Kilimanjaro liligongana uso kwa uso na gari lenye namba za usajili T 612 BNN aina ya Mitsubish Canter iliyokuwa ikiendeshwa na Peter Mmasi.
Waliofariki katika ajali hiyo ni Mmasi aliyekuwa dereva wa Mitsubishi Canter,Victor Kileo,Vivian Urio na Isack Temba,ambao walikuwa abiria wa gari hilo na wakazi wa Baraa jijini Arusha na utingo wa gari aina ya Mitsubishi Fuso ambaye amefahamika kwa jina moja la Idd ambaye pia ni mkazi wa Himo,Kilimanjaro.
"Uchunguzi wa awali umebaini kwamba, chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa gari aina ya Mitsubishi Fuso iliyokuwa inatokea Moshi kuelekea Arusha ambapo ilihama upande wa pili wa barabara na kugongana na gari aina ya Mitsubishi Canter lililokuwa linatokea Arusha kuelekea Moshi,"
"Baada ya magari hayo kugongana gari aina Mitsubish Fuso lilipitiliza na kuanguka kwenye mtaro uliopo pembezoni mwa barabara,"Iliongeza
Majeruhi katika ajali hiyo ni Lyimo ambaye amepelekwa katika hospitali ya KCMC mkoani Kilimanjaro kwa matibabu zaidi na miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya Rufaa ya Mt.Meru,Arusha.

0 Comments:
Post a Comment