![]() |
| Aliekua Mwenyekiti wa Tume ya kurekebisha katiba ya Jamuhuri ya Muungano Tanzania Jaji Joseph Warioba.(Picha kwa hisani ya mtandao.) |
| Na Salum Vuai |
Wengi wao wanadai kuwa, katiba mpya ni muhimu ili pamoja na mambo mengine, Tanzania iweze kufanya chaguzi zake kwa misingi ya haki na uadilifu.
Shindikizo limekuwa kubwa hata kuibua maoni tafauti kutoka kwa wanasiasa, wanaharakati na wananchi wengine katika nafasi zao mbalimbali, wakitaka rasimu ya katiba ya tume ya Warioba ipewe thamani inayostahili.
Hata hivyo, mara kadhaa tumekuwa tukisikia majibu yanayotolewa na upande wa serikali, na baadhi ya wakati Chama cha Mapinduzi, ambayo hayaoneshi utashi wa kuwa na katiba hiyo angalau kwa sasa.
Serikali imekuwa ikisisitiza kuwa kipaumbele chake kwa sasa ni kuweka sawa uchumi na mambo mengine yatafuata hatua kwa hatua.
Hata hivyo, katika tafakuri yake, Muhenga anaeleza kuwa kusawazisha uchumi kwanza sio jambo baya, lakini inafikiri pia kuna mambo mengi ya kutafakari kuhusu mchakato mzima wa katiba mpya, mbali na kupatikana kwake ambako wanaharakati wanakupigia chapuo.
Muhenga hana tatizo na mtazamo wa serikali, lakini anaona ni vyema ioneshe utashi wake kwa kuzionea huruma gharama kubwa zilizotumika katika mchakato mzima wa kutafuta katiba mpya.
Nakumbuka mwana CCM mmoja kindakindaki, katika mkutano mmoja uliofanyika hapa Zanzibar, alimuuliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi, kwamba hata kama hana nia ya kufukua makaburi, je, hata gharama za mazishi hataki kuzijua?
Kwa mnasaba huo, Muhenga anauliza kwa nini viongozi wetu hili jambo la mabilioni yaliyotumika katika mchakato mzima wa kutafuta katiba mpya hawalioni kuwa ni kubwa na zito?
Je, lengo la kutoa fedha zote hizo lilikuwa lipi? Kuwapa watu utajiri?
Na jambo la kusikitisha ni kuwa katika Bunge Maalum la Katiba sio wote waliokuwa wakitoa maoni, na hadi Bunge hilo lililoanza Febuari 18, 2014 lilipofikia tamati, wapo miongoni mwa wajumbe ambao hawakufunua mdomo kuchangia japo kidogo.
Wengi walikuwa wakipiga kofi tu na kuwazia namna watakavyozitumia fedha walizovuna ambazo wengine hawakuwahi kuota hata siku moja kuzitia mikononi.
Ikumbukwe kuwa idadi ya wajumbe wa Bunge la Katiba ilikuwa kubwa, ikijumuisha Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar na wajumbe 201 walioorodheshwa kwa mujibu wa Kifungu Na. 22(1c) cha sheria ya mabadiliko ya katiba ambayo ilionesha makundi kumi mbalimbali yaliyohusika. Awali, Bunge la katiba lilipangiwa kukutana kwa siku 70 ambazo baadae ilielezwa zitaongezwa siku 20 zaidi kujadili rasimu ya katiba kama ilivyowasilishwa na Tume ya Warioba. Na katika kuonesha kuwa wengi waliweka mbele maslahi binafsi kuliko kukata kiu ya Watanzania kupata katiba mpya, baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba waliushangaza umma pale walipodai kuwa posho ya shilingi 300,000 waliyokuwa wakilipwa haitoshi na kutaka iongezwe kufikia shilingi 500,000 kwa siku. Kitendo hicho kiliwasikitisha Watanzania wengi na hata mtandao wa Shirika la Kutetea Haki na Usawa wa Kijinsia (TGNP), katika kuhakikisha rasilimali za taifa zinawanufaisha wananchi wote, ulipinga madai hayo ya wajumbe ikizingatiwa wakati huo taifa lilikuwa na uhaba mkubwa wa fedha na deni la taifa likiongezeka kwa kasi kubwa hadi kufikia shilingi trilioni 27. Hicho kiasi ni zaidi ya mshahara wa baadhi ya watumishi serikalini na sekta binafsi ambao wanapambana kulea familia kwa mshahara huo huo na pindi wakidai kuongezewa maslahi yao wabunge wanashindwa kuwatetea,” ilikaririwa TGNP wakati huo. Mchakato mzima wa kutafuta katiba mpya uligharimu mabilioni ya shilingi yatookanayo na jasho la walipa kodi, lakini leo pamoja na suala la katiba kuwekwa kiporo, hakuna anaeonesha kuumwa na gharama hizo wala kuzionea uchungu. Bila shaka, baadhi ya mapendekezo yaliyomo kwenye rasimu ya Tume ya Warioba huenda yakawa hayaendani tena na wakati wa sasa, hivyo kuhitajika mchakato mwengine kwa ajili ya kuifumua, ambao nao utaikamua hazina ya nchi fedha nyengine nyingi. Maoni na usharu mpigie wasiliana na mwandishi. salumss@yahoo.co.uk 0777865050 |

0 Comments:
Post a Comment