MIGOGORO YA ARDHI BADO NI KITENDAWILI - OTHMAN MASOUD
Makamu wa Kwanza wa
Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, ameeleza ulazima wa
kuwatumia wataalamu wa milki kuu (‘Real Estate Professionals’) kutokana na
ufinyu mkubwa wa ardhi na ili kuleta maendeleo ya kweli ya kiuchumi nchini.
Makamu wa Kwanza
ameitaja Zanzibar kwa ujumla wake kuwa ni eneo la kitalii ambalo linapokea
wageni wengi wa kimataifa tangu asili, na hivyo linahitaji kutoa kipau-mbele
katika matumizi bora ya ardhi yanayoweza kuchangia kupendezesha mitaa na
mandhari ya visiwa vya Unguja na Pemba.
Mheshimiwa Othman
ameyasema hayo leo, wakati akifungua Kongamano na Mkutano Mkuu wa Pili wa Mwaka
wa Taasisi ya Wataalamu wa Milki Kuu Tanzania (AREPTA) unaofanyika katika
Hoteli ya Verde, nje kidogo ya Jiji la Zanzibar.
Akiongelea juu ya tatizo
sugu la biashara holela ya majengo na mizozo katika umiliki wa ardhi,
Mheshimiwa Othman amesema, “binafsi ninaamini kuwa iwapo suluhisho la migogoro
ya ardhi litapatikana, wananchi watatekeleza majukumu yao ya kilimo, ufugaji na
ujenzi kwa tija zaidi kulikoni hali ilivyo sasa”.
Mheshimiwa Othman
ametoa wito kwa waandaaji wa kongamano hilo kutafakari namna bora ya kutumia
akiba kubwa ya wataalamu waliobobea, ili kutafuta muarubaini wa tatizo sugu la
matumizi holela ya ardhi na biashara ya majengo na kusaidia kuikwamua nchi
kiuchumi; huku akieleza utayari wa Serikali katika kuunga mkono juhudi hizo.
Akimkaribisha Mgeni
Rasmi, Rais wa Taasisi ya Milki Kuu Tanzania, Bw. Andrew Katto alibainisha
mahitaji makubwa ya sheria itakayodhibiti wimbi kubwa la biashara holela ya
umiliki wa majengo na ardhi, akisema azma hiyo itawezekana kwa mashirikiano
makubwa ya Serikali.
Mkutano huo wa siku
mbili unawajumuisha wataalamu na wanataaluma wa nyanja mbali mbali za maendeleo
ya ardhi ambao ni pamoja na wathamini, maafisa ardhi, mawakala wa milki,
wasimamizi, na wachambuzi wa biashara za majengo kutoka Tanzania Bara na
Zanzibar.
Dhamira ya kongamano
hilo ni pamoja na kujadili njia muafaka na endelevu ili kuifikisha Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania katika uchumi bora kupitia tasnia ya milki kuu sambamba na
utatuzi wa migogoro ya ardhi inayoendelea kubaki kuwa donda ndugu nchini.



0 Comments:
Post a Comment