
IMEANDIKA NA ZUHURA JUMA, PEMBA
WANANCHI kisiwani Pemba wamesema, wanasikitishwa na kitendo cha wafanyabiashara kuingiza bidhaa zilizoharibika ama kupitiwa na muda, jambo ambalo linaweza kuwasababishia maradhi mbali mbali.
Wakizungumza wakati wakishuhudia uteketezaji wa mchele aina ya Sauflower tani 36.7 katika Kware ya Pujini Chake Chake wananchi hao walisema, mara kadhaa wamekuwa wakishuhudia Wakala wa Chakula na Dawa kwenda kuteketeza bidhaa mbali mbali zilizoharibika na kupitiwa na muda ikiwemo ya mchele.
Walisema kuwa, ipo haja kwa Serikali kuweka vidhibiti madhubuti katika kuhakikisha bidhaa zinazoingizwa kisiwani Pemba zinakuwa salama kwa mtumiaji, ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.
“Kwa nini huu mchele ufikie kuingia Pemba kama huko Unguja umefanyiwa ukaguzi wa kutosha, kwa sababu ungegundulika kwamba umeshaharibika, tunaiomba Serikali iwe makini juu ya suala hili, kwani jambo bidhaa mbuvu ni kucheza na maisha ya watu”, walisema wananchi hao.
Mwananchi Rajab Juma Mjawiri mkaazi wa Pujini Kumvini alieleza kuwa, ameuona mchele jinsi unavyotoa wadudu kutokana na kuwa umeshaharibika, ambapo aliwapongeza ZFDA Pemba kwa kuokoa maisha ya watu.
“Kwa ulivyo huu mchele kama haukudhibitiwa, tungeumbulika lakini tunashukuru kwa juhudi waliyoichukua katika kuudhibiti na kuteketezwa”, alisema.
Mwananchi Mohamed Ramadhan Khatib alisema kuwa, ni hali ya kusikitisha kuona kwamba bidhaa zilizoharibika zinaingizwa kisiwani Pemba kiasi ambacho hata wao wanaanza kuingiwa na hofu.
“Kwa mchele niliouona leo lazima tuwe na hofu, tunaangamia jamani, tunaomba ukaguzi wa bidhaa ufanywe kabla ya kuingia Pemba, ili kuepuka wananchi kula vyakula vilivyoharibika”, alisema.
Alieleza kuwa, wazee wa zamani walikuwa hawana magonjwa kiholela kutoakana na kwamba walikuwa wanakula vyakula vilivyo salama, lakini sasa kutokana na tamaa waliyonayo wafanyabiashara, hufanya ubadhirifu na hatimae watu kupata magonjwa mbali mbali.
Nae Riziki Uledi Komba mkaazi wa Pujini alieleza kuwa, ikiwa bidhaa zitakaguliwa kabla ya kuingia Pemba, wataepusha kuingizwa bidhaa zilizoharibika.
“Itakuwa ulipotoka Unguja kuja Pemba hakufanyiwa uchunguzi, hivyo tunaomba kabla ya kufika huku wauchunguze kwanza ndipo uletwe, kinyume chake tutaangamia na watoto wetu”, alieleza.
Mapema Mkurugenzi wa Wakala wa Chakula na Dawa (ZFDA) Pemba Nassir Salum Buheti alisema, wameteketeza polo 737 ambazo ni sawa na tani 36.7 za mchele aina ya sunflower baada ya kuonekana kuwa haufai kwa matumizi.
Alisema kuwa, hatua hiyo imekuja baada ya kukamata mchele katika bandari ya Wete polo 400 zenye ujazo wa kilogramu 50 kwa kila moja, ambapo baada ya kupelekwa maabara uligundulika kwamba haufai kwa matumizi.
“Mchele uliingia bandarini na kuonekana kwamba haufai kwa matumizi na ndipo tulipoanza kufanya ukaguzi katika maduka na maghala mbali mbali na tulifanikiwa kuukamata nan do maana leo tunateketeza”, alisema.
Alieleza kuwa, wafanyabiashara wamekuwa wakifanya udanganyifu kwa kuingiza bidhaa zilizoharibika ama kupitiwa na muda, jambo ambalo ni kosa kisheria na pia ni kuhatarisha afya ya mlaji.
Nae Mfamasia Dhamana kutoka ZFDA Pemba Nassor Ali Nassor alieleza kuwa, ZFDA inafanya kazi kubwa ya kukagua bidhaa ili kuhakikisha wananchi wanakula chakula salama na afya ya jamii inalindwa.
“Tunaelewa kwamba madhara mengi yanaweza kupatikana iwapo wananchi watakula vyakula vipovu, hivyo tutajitahidi kuhakikisha tunadhibiti vyakula vibovu, ili visitumike”, alisema Mfamasia huyo.
Aliwataka wafanyabiasha kuacha udanganyifu katika bidhaa, kwani wanaweza kuhatarisha maisha na usalama wa mwanadamu, hivyo wahakikishe wanaleta biadaa zilizobora.
0 Comments:
Post a Comment