Mradi wa CCTV Camera pasua kichwa Pemba

Muonekano wa kati kati mji wa Chakechake Pemba ambao ni miongoni mwa sehemu ilionufaika na mradi wa uwekaji wa Camera.


Kamati  ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi, imesema haikuridhishwa na taarifa ya mradi wa Zanzibar salama (CCTV Camera) Kisiwani Pemba, kutokana na sababu kadhaa ikiwa ni pamoja na kutoonesha mchanganuo mzuri wa matumizi ya fedha.

Wajumbe wa kamati hiyo, waliyasema hayo mara baada ya upokeaji wa taarifa ya mradi wa uwekaji wa kamera (CCTV) Pemba, katika ukumbi wa Kikosi cha Zimamoto na uwokozi Chanjaani Chake chake Kisiwani humo.

Walisema, hawana tatizo na ufungwaji wa kamera hizo kutokana na uwepo wa mabadiliko ya teknolojia sambamba na kujitokeza kwa matukio mbali mbali ikiwemo la uvunjia wa sheria za usalama barabarani.

Mwenyenkiti wa kamati hiyo Ali Suleiman Ameir, ameitaka ofisi ya Rais, tawala za mikoa serikali za Mitaa na Idara maalum za SMZ kuifanyia marekebisho taarifa hiyo, ili kujuwa matumizi sahihi ya fedha za Serikali sambamba na kuyatekeleza waliyoelekezwa.

“Niiombe Wizara ihakikishe kila kinachostahiki kufanywa kama Serikali hakistahiki kutaka ushauri kwa mshauri elekezi kwa mujibu wa mkataba na vikao ndani ya wiki moja kiwe kimeweza kutekelezwa,” alisema.

Aidha, alimtaka mkandarasi kumaliza haraka jukumu hilo kwa muda mchache uliobakia kwani alisema, wanaelewa kwamba yupo nje ya muda wa kutekelezwa mpango huo wa ufungaji wa CCTV.

Mjumbe wa Kamati hiyo Prof. Omar Fakih Hamad alisema, taarifa hiyo imeonekana kutokuwa na muonesho wa mchanganuo mzuri wa mradi hasa katika matumizi ya fedha.

“Lengo la kufungwa CCTV ni kuongeza usalama katika nchi yetu, hivyo lazima tueke taarifa au mabango yatayowajulisha wananchi eneo hilo limeekwa kamera hatuna nia ya kukamata wahalifu tunachokitaka ni kupunguza matukio hii itasaidia watu wabaya kuwa na hofu ya kufanya matukio,” alisema.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Nchi ofisi ya Rais Tawala za mikoa serikali za mitaa na Idara maalum za SMZ Issa Mahfoudh Haji, aliahidi kuyachukua na kuyatekeleza yote ambayo wameelekezwa ili malengo ya Serikali yaweze kufikiwa.

Mapema, akisoma taarifa hiyo Afisa Mdhamini wa ofisi hiyo Thabit Othman Abdalla alisema, jumla ya kamera 248 zinatarajiwa kufungwa katika maeneo tofauti Kisiwani Pemba ambapo mpaka sasa kamera 227 tayari zimeshafungwa.

Alieleza kuwa, kamera 21 bado hazijafungwa, 139 ndizo zinazoonesha huku 88 zikiwa katika maeneo tofauti hazionyeshi kutokana na ukosefu wa huduma ya nishati ya jua na ukosefu wa sehemu ya kuhifadhia mitambo.

Kamati ya bajeti ya baraza la Wawakilishi ilitembelea maeneo makuu ya mradi huo katika kituo cha Chake chake ndani ya kambi ya Kikosi cha zimamoto na uwokozi (KZU) Chanjaani, kituo cha kikosi cha KMKM Mkoani na kituo cha kambi ya mafunzo (MF) Wete.


 Imeandikwa na  NA Hanifa  Salim, Pemba.

About mmedia

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment