Idadi ndogo Masheha Wanawake tatizo Pemba


Baadhi ya wanawake kisiwani Pemba wakiwa kwenye moja ya mkutano wa uhamasishaji kiwani humo.Picha na Maktaba.


Pemba


Wanaharakati wanaopigania haki za wanawake kisiwani Pemba, wamesema bado mwanamke, hajapewa kipaumbele ipasavyo kwenye uongozi, kuanzia nafasi za usheha, kwa kuwepo masheha wanawake 28 pekee, ikilinganishwa na masheha 101 wanaume.

Idadi hiyo ya masheha 28 wanawake, ni sawa na kila wilaya moja yenye wastani wa shehia 30, kuwepo masheha saba (7) wanawake, huku idadi ya masheha wanaume kwa wastani huo huo ikionesha 26 wastani wa idadi ya wanaume 25 kwa shehia.

Wakizungumza na mwandishi habari hizi, walisema bado kuna mamlaka hazijatilia maanani uwepo wa kundi la wanawake katika uongozi, na ndio maana kwa mfano mkoa wa kusini Pemba, ulioundwa na wilaya mbili kwa shehia 68 masheha wanawake ni 15.

Wilaya ya Mkoani pekee yenye masheha 36, imebainika kuwepo masheha wanawake 10, huku idadi ya wanaume wakiwa 26, wakati wilaya ya Chake chake yenye masheha 32, wanawake wamejitokeza kwenye shehia tano ‘5’ pekee.

Kwa upande wa Mkoa wa kaskazini Pemba unaongozwa na mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya na katibu tawala wote wanawake, unaoundwa na wilaya za Micheweni na Wete, unao masheha 61, kati yao wanawake wakiwa 13 pekee na masheha wanaume 48.

Akizungumza hivi karibuni Mratibu wa mradi wa kuwawezesha wanawake kudai hazi zao za uongozi, demokrasia na siasa ‘SWIL’ kutoka TAMWA-Zanzibar Salma Amir Lusangi, alisema zipo mamlaka hazijawabika ipasavyo na ndio maana, wanawake masheha kisiwani Pemba wamekuwa kidogo.

Alisema, bado elimu zaidi inahitajika kwa viongozi wenye mamlaka, kuona wanawake wanapewa haki zao za uongozi, kwa vile katiba, sheria, matamko na maazimio mbali mbali hayajapinga wanawake kuwa viongozi.

“Sisi TAMWA – Zanzibar tunaendelea na mradi mkubwa, wa kuwawezesha wanawake kudai haki zao mbali mbali, zikiwemo za uongozi, na moja ya changamoto ambayo tunaiona ni wenye mamlaka kutolipa kipaumbele kundi hili,’’alieleza.

Kwa upande wake Mratibu wa mradi kama huo kutoka Jumuiya ya Utetezi wa Kijinsia na Mazingira Pemba ‘PEGAO’ Dina Juma Makota, alisema wanawake wanahaki zao mbali mbali ikiwemo za uongozi.

Alieleza kuwa, ingawa changamoto kubwa ni jamii ya kundi la wanaume kutowaamini wanawake na kisha kutooneka kwenye uongozi, kuanzia ngazi ya shehia na taifa kwa ujumla.

“Kila mmoja akiwajibika kisheria na kutoa fursa za uongozi kwa wanawakae, basi hata masheha, wakuu wa wilaya, mkoa, mawaziri na makatibu wakuu idadi ya wanawake na wanaume italingana,’’alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tumaini Jipya ‘TUJIPE’ Tatu Abdalla Msellem, alisema bado hali ya kuwaamini wanawake katika safu ya uongozi, inatisa.

Alieleza kuwa, hata idadi ya masheha ukiiona hairidhishi, bado kuna mamlaka wakiwemo wanaopendekeza majina, hawajawajibika ipasavyo, hali inayodhoofisha uwezo wa wanawake.

‘Ukienda kwenye siasa, nafasi za juu zote zimechukuliwa na viongozi wanaume, lakini hata nafasi kama za usheha, bado hali ya wanawake kupewa nafasi hairidhishi,’’alieleza.

Sheha wa shehia ya Madungu wilaya ya Chake chake Mafunda Hamad Rubea, alisema anaendelea kuiongoza shehia yake licha ya changamoto za dhaharu anazozipata.

“Wengine ukiwapelekea wito kama wananchi, wanaoenesha dharau kwa sababu ya uwanauke wangu, lakini nikichimba mkwala wanatii wito na kuniomba radhi kwa utukutu wao,’’alieleza.

Mkuu wa mkoa wa kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib, ambao mkoa wake una masheha 61 wakiwa wanawake ni 13 na wanaume 48, alisema kwa hali alivyoikuta ya wanawake kutoonekana, hatua ya sasa ameipiga.

“Nilikuta mkoa wangu idadi ya masheha wanawake hawafiki hata tisa, leo tunao 13 na wanafanya vizuri, lakini hatujasita tukihisi kuna anaetufaa na kuna ambae ameboronga, tutawapa nafasi,’’alieleza.

Katibu tawala wlaya ya Mkoani Miza Hassan Faki, alisema changamoto ya nafasi ya usheha hasa kwa mfumo wa kisiasa umekuwa ukiwapa hofu na kuzikataa nafasi wenywee.

“Kwa mfano tulipotaka kumpendekeza sheha wa shehia ya Mwambe awe mwanamke, tulilazimika kutumia mbinu za ziada, maana mifumo ya kisiasa na mtazamo wa jamii, ndio unaowatia hofu wanawake,’’alieleza.

Hata hivyo, aliwashauri masheha wanawake kuendelea kufanyakazi kwa bidii na kufuata sheria, kwani ugumu wa uongozi wakati mwengine husindikizwa kwa kufanya kazi kinyume na maelekezo.

Kisiwa cha Pemba chenye mikoa miwili ya kusini na kaskazini, unazo wilaya nne za Chake chake, Mkoani, Wete na Micheweni zikizaliwa shehia 129 sawa na masheha wanawake 28 pekee na wanaume 101.


                                                    Imeandikwa na Haji Nassor

About mmedia

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment