Na Salum Vuai
MVUA ni neema ambayo kila mja anaihitaji na kama
inapita miezi au miaka bila kunyesha, viumbe tunakuwa mashakani.
Mvua huleta maji yanayohitajika kuhuisha ardhi ili
mazao yanawiri na kujaza vianzio vya maji hayo ambayo kuwepo kwake ndio furaha
ya kila kiumbe.
Si mwanadamu, mnyama, ndege, miti na hata wadudu
warukao na kutambaa, anayeweza kuishi kwa raha bila ya maji.
Lakini pamoja na uzuri wake, mvua inaponyesha katika
nchi au eneo lisilokuwa na miundombinu rafiki, ni wazi madhara yatatokea na
mara nyengine makubwa sana kiasi cha kuporomosha majengo na kuondoka na roho.
Kwa bahati mbaya sana, katika kipindi cha kuanzia
miaka ya 1980 hadi sasa, hapa kwetu Zanzibar kila msimu wa mvua unapowadia
inakuwa karaha badala ya raha, na nakama badala ya neema.
Lakini la kusikitisha zaidi, Serikali hutumia fedha
nyingi kutengeneza miundombinu kwa lengo la kuzuia mafuriko na kutuwama kwa
maji katika maeneo ya makaazi na majengo ya ofisi bali tija
haionekani.
Bila shaka maji ni muhimu lakini katu hayafai
kufungiwa njia ili mvua inaponyesha yaweze kupita kwa urahisi na
kuwaacha viumbe na makaazi yao salama.
Lakini hivyo sivyo ilivyo hapa nchini, kwani pamoja na
watu kuhitaji mvua, inapopatikana inakuwa wasiwasi mtupu wakikumbuka tafrani
iliyowakumba misimu iliyotangulia.
Tayari mfano umeonekana kutokana na mvua zilizoanza
kunyesha siku tatu zilizopita katika maeneo mengi ya Zanzibar hasa mjini ambako
miundombinu haikidhi haja wala kuwahakikishia wananchi usalama wa kutosha.
Katika hali ya kawaida, mvua za awali huonesha
mapungufu yaliyopo juu ya paa la nyumba yetu, kwani kila palipo pabovu patavuja
na hii inayonyesha sasa imefichua udhaifu wa miundombinu yetu.
Lakini tujiulize, kwa nini iwe tunasubiri mvua
zituoneshe matundu badala ya kutumia kipindi cha kiangazi kujiandaaa mapema
kukabili athari zinazoweza kujitokeza?
Je, ni yepi matokeo ya miradi ya ujenzi wa miundombinu
iliyolenga kudhibiti kutuwama kwa maji ambayo imegharimu mapesa mengi mno, tena
mengine ni misaada na mikopo ambayo walipaji ni sisi walipa kodi wanyonge?
Ukiacha udhaifu wa viwango katika misingi na njia za
maji, wananchi nao wanafanya makosa sana kuongeza ukubwa wa tatizo.
Khulka ya wakaazi wa maeneo mengi kuigeuza misingi
kuwa ndio majaa ya kutupia taka, ni ukosefu wa nadhari na isipoachwa inaweza
kutuletaa janga kubwa la mafuriko.
Ifahamike kuwa kutupa taka katika misingi kunaziba
njia ambazo zimejengwa ili kusafirisha maji kwenda baharini au sehemu nyengine
zilizotengwa kwa ajili hiyo.
Hali kama inayoonekana eneo la posta Kijangwani wakati
wa mvua, njia kutuwama maji pamoja na mitaani, ni matokeo ya tabia isiyokuwa ya
kistaarabu kutupa taka kila pahala hata misingini.
Lazima jamii ifahamu kwamba uchafu ukichanganyika na
maji matokeo yake ni mazalia ya nzi ambao ni wadudu waenezao maradhi hasa ya
matumbo na kipindupindu.
Hakuna asiyejua ubaya wa kipindupindu ambacho kikipiga
hodi hakiwaachi watu salama na mara nyingi vifo mfululizo na vya haraka
huchukua nafasi.
Hali hii ikitokea, inakuwa marufuku hata kuwatembelea
wagonjwa wanaotengewa kambi mbali na familia na jamii zao kutokana na tabia ya
maradhi hayo kuambukiza kwa kasi.
Ufike wakati tuiweke nchi yetu Zanzibar katika
mandhari nzuri ya kuhimili hali zote kiangazi na mvua, ili shughuli ziendelee
bila kikwazo chochote.
Serikali ifanye wajibu wake kuhakikisha ujenzi wa
miundombinu unakuwa na kiwango kinachoakisi thamani ya fedha zinazotumika,
lakini na wananchi nao waitunze na kuilinda isiharibiwe kwa kumwagiwa taka.
Wenye dhamana ya kutoa zabuni kwa wakandarasi wasiweke
mbele tamaa binafsi kwa kuchagua washindi kwa upendeleo wakitarajia pasenti
kama bahashishi yao.
Pia wakandarasi nao wasifanye ghushi kwa kutumia vifaa
duni au kupunguza saruji na kuongeza mchanga, kitendo kinachoweza
kutusababishia majuto kwa ubovu wa majengo, misingi na barabara zetu.
Simu: 0777 865050/0714 425556
0 Comments:
Post a Comment