Naibu katibu mkuu Wizara ya Habari Zanzibar Khamis Abdalla Said amesema Serikali imedhamiria ndani ya miezi 9 ijayo tayari wawe wamekamilisha sheria bora ya habari itakayokwendana na matakwa ya pande zote mbili.
Aliyasema hayo wakati alipokua akifungua mkutano wa uwasilishwaji wa ripoti maalumu iliotolewa na TAMWA-ZNZ kwa kushirikiana na Internews TZ iliolenga kuonesha baadhi ya changamoto za sheria ya habari kisiwani hapa.
Alisema wao kama miongoni mwa wahusika wakuu wa kuhakikisha sheria bora zinapitishwa kwa maslahi ya wote wameona changamoto ya sheria hio na ndio maana wamekua wakichukua maoni mbali mbali ya wadau kwa lengo la kuboreha.
Sambamba na hayo Naibu huyo alipongeza jitihada zinazofanywa na wadau wa habari katika kuibua hoja na haja ya jamii juu ya kuwa na sheria na sera ya habari inayokidhi mahitaji ya jamii kulingana na muda na wakati tulionao.
Akiendelea kufafanua zaidi aliwataka wadau hao kuwa na subra wakiamini sheria bora ya habari iliokidhi matakwa ya wote itapatikana siku si nyingi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ustawi wa jamii ya Baraza la wawakilishi Zanzibar Mohamed Ahmada alisema baadhi ya vipengele vya sheria ya habari vilivyowekwa anaamini vilikuja kwa matukio maalumu akitolea mfano sharia ya kudhibiti mitandao ya kijamii.
Sambamba na hayo alizungumzia suala la maslahi duni ya waandishi wa habari ikiwemo kukosa mikataba katika vyombo vyao jambo ambalo alisema linakosesha ueledi kwenye tasnia hio.
Alisema kila mmoja anafahamu kuwa sheria ya habari iliopo sasa inahitaji mabadiliko kwani sharia hio ilipitishwa mwaka 1988 na hadi sasa ndio inayofanya kazi.
Akiwasilisha ripoti inayoonesha baadhi ya changamoto za sheria ya habari Zanzibar,Bi Hawra Shamte alisema baadhi ya vipengele vya sheria vimekua vigumu na havipaswi kutumika kwa wakati tulionao hivi sasa.
Alitolea mfano sheria inayomruhusu Waziri wa habari kufungia au kuvamia chombo cha habari bia ya kupata ushauri au makubaliano ya taasisi nyengine yoyote hile.
Alisema hali hio haiendani na wakati ulipo hivi sasa na inapaswa kuwekwa alau kamati maalumu au bodi ya kutoa maamuzi ya vyombo vya habari na si kupewa mamlaka hayo mtu mmoja tu.
Awali Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa habari Wanawake TAMWA-ZNZ Dkt,Mzuri Issa alisema mchakato huo wa wadau kutaka mabadiliko ya sheria ya habari ni wa muda mrefu na unapaswa kufanyiwa kazi.
Alisema kuwepo kwa sheria bora ya habari kunaweza pia
kuleta uwajibikaji Serikali na kuongeza kasi ya maendeleo kwa Serikali na
wananchi kwa ujumla.
0 Comments:
Post a Comment