Taarifa ya Baraza la watu wenye Ulemavu likiwa na mikakati ya maendeleo kwa jamii hiyo

Mwenyekiti wa Baraza la watu wenye Ulemavu bi Salma Hajji Saadat akitoa tarifa ya jamii hiyo kuelekea maadhimisho ya siku ya watu wenye ulemavu duniani ambayo huadhimishwa kila ifikapo  tarehe 3 Dicember  kila mwaka. Kushotoni kwake ni Mkrugenzi wa Baraza la watu wenye Ulemavu Zanzibar  Ussy Khamis Debe

Ndugu waandishi wa habari; 

 

 

Tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kuwa katika hali ya uzima, afya bora na kutuwezesha kufika hapa leo, katika shamra shamra za shuguli za maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani. Shukrani za pekee ziwaendee wanahabari wote mliopo hapa kwa kuona umuhimu wa shughuli yetu hii katika kuifahamisha jamii juu ya siku ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu.    

Kama inavyoeleweka, ifikapo tarehe 3 Disemba ya kila mwaka Zanzibar inaungana na nchi nyengine ulimwenguni katika kuadhimisha siku ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani. Maadhimisho hayo yanatufanya tuweze kutafakari juu ya maendeleo na changamoto mbalimbali walizonazo Watu wenye Ulemavu ili kufikia Maendeleo Jumuishi kwa wote. 

 

Ndugu waandishi wa habari; 

Historia inaonesha kwamba, harakati za kupigania haki na fursa za Watu wenye Ulemavu zilianza miaka ya 1970 kwa nchi Wanachama katika Umoja wa Mataifa baada ya kupitia na kuangalia masuala yote yanayohusu maisha na maendeleo ya watu wote duniani. Hivyo, wameona kuwa, bado masuala ya Watu wenye Ulemavu hayajatiliwa mkazo wa aina yoyote hasa katika upande wa suala la haki za kibinadamu. 

Hatua mbalimbali zilichukuliwa kwa kipindi cha miaka mingi kuanzia mwaka 1981, hadi mwaka 1992, maamuzi ya mwisho yalitangazwa tarehe 3 Disemba 1992 kuwa kila ifikapo tarehe 3 Disemba ya kila mwaka iwe ni Siku ya Kimataifa ya Maadhimisho ya Haki za Watu wenye Ulemavu Duniani, kwa misingi ya kuhakikisha kwamba, suala la Watu wenye Ulemavu ni moja kati ya masuala mengineyo ya Haki za Binadamu Duniani 

 

Ndugu waandishi wa habari; 

Siku hii imepewa kipaumbele, umuhimu na ulazima wa kuadhimishwa kila mwaka duniani kote, kwa nchi wanachama zilizoridhia Mkataba wa Kimataifa wa haki za Watu wenye Ulemavu, kuendena na kauli mbiu ya mwaka huu”




Ndugu waandishi wa habari; 

Kwa mujibu wa kauli mbiu ya mwaka huu inayosema “Uongozi na Ushirikishwaji wa Watu wenye Ulemavu, kuelekea ujumuishwaji na ufikiwaji endelevu baada ya uviko 19 Duniani”

Uchambuzi na ufafanuzi wa kauli mbiu hii imezingatia masuala mbali mbali yakiwemo: - 

Usawa katika kupata mawasiliano  

Mara nyingi Watu wenye Ulemavu katika suala la mawasiliano wanapata changamoto kubwa ambapo wanakuwa hawawezi kujua katika taifa lao kwa kila kinachotokea, kwani miundombinu ya huduma hii si rafiki kwao na inapelekea kukosa huduma mbali mbali katika jamii kwa wakati muafaka. 

Kuwawezesha katika kupata maendeleo  

Hii inatoa msisitizo wa kauli mbiu ya mwaka huu. Ushirikishwaji wa Watu wenye Ulemavu, tunakusudia kusema kuwa, Watu wenye Ulemavu wanapaswa kushirikishwa katika mipango yote ikiwemo ya kisera kwa masuala yanayohusu kundi hili. Si jambo la busara hata kidogo na haitapendeza iwapo jamii itawatenga na kuwanyanyapaa kwa kutowashirikisha katika masuala tofauti yakiwemo hata yale yanayowahusu.

Chombo kikuu cha utendaji kuhusiana na masuala ya Watu wenye Ulemavu ni Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu ambalo pamoja na majukumu yake, Katika kuhakikisha kuwa Watu wenye Ulemavu wanapata maendeleo, kundi hili liweze kujumuishwa katika nyanja zote zikiwemo za kisiasa, kijamii na kiuchumi. 

 

Ndugu waandishi wa habari;

Umoja wa Mataifa kupitia viongozi wakuu wa Serikali wa nchi mbali mbali walishiriki mkutano uliofanyika makao Makuu ya Umoja wa Mataifa huko Marekani tarehe 24-25 Septemba mwaka huu, katika mkutano huo iliamulika kwamba ni kuwekwa mkazo katika kufanya mapitio makubwa juu ya utekelezaji wa malengo 17 ya maendeleo endelevu ifikapo 2030. Sambamba na hayo; Mkutano huo umepitisha maazimio ya kuboresha zaidi utekelezaji wa agenda iliyoibuliwa mwezi Septemba 2015 kuwa ifikapo 2030 pamoja na kupitisha azimio la kisiasa. 

 

Kwa mujibu wa kaulimbiu ya mwaka huu inavoeleza kuwa “Uongozi na Ushirikishwaji wa Watu wenye Ulemavu, kuelekea ujumuishwaji na ufikiwaji endelevu baada ya uviko 19 Duniani”

Hii ndio kusema kuwa, Watu wenye Ulemavu wana haki ya kushirikishwa katika nyanja zote za kiuchumi kama raia wengine wote wa nchi hii bila ya kujali ulemavu wao Kwani tunachoangalia si ulemavu wao bali taunatizama haki zao na uwezo walionao. 

Ndugu waandishi wa habari; 

Ndugu waandishi wa habari na washiriki wote kwa ujumla, haki hii ya kushiriki katika shughuli za kimaendeleo imeelezwa katika Ibara ya 29 ya Mkataba wa Kimataifa wa Watu wenye Ulemavu ulioridhiwa Tanzania mwaka 2009. 

              

Mkurugenzi wa Baraza la watu wenye Ulemavu Zanzibar Ussy Khamis Debe akifafanua jambo wakati walipotoa taarifa kwa vyombo vya habari kuelekea kuadhimisha  siku ya watu wenye ulemavu Duniiani

Ndugu waandishi wa habari; 

Toka kuundwa kwa Idara ya Watu wenye Ulemavu, yapo yafanikio mengi yaliyopatikana, mafanikio hayo ni pamoja na: - 

• Kuwepo kwa Mfuko wa Maendeleo ya watu wenye ulemavu, Mfuko ambao tayari umeeshanza kuwanufaisha walengwa ikiwa ni pamoja na mikopo, msaada wa kielimu na matibabu. Hali hii imekuwa ni faraja kwa watu wenye ulemavu kwani umewasaidia kutokana na hali ngumu ya kiuchumi na utegemezi, pia kutokana mkopo huu kutokua na riba imekua ni jambo la faraja kwa watu wenye ulemavu kwani zipo taasisi nyingi ambazo zinatoa mikopo lakini ni kikwazo kikubwa kwao kutokana na hali zao

 

• Kuwa na takwimu za Watu wenye Ulemavu kupitia usajili na mfumo wa kielectroniki kwa ajili ya Watu wenye Ulemavu unaojulikana kwa jina la JUMUISHI DATA BASE hili ni suala la kupigiwa mfano, kwani Serikali yetu imeweza kutambua idadi ya Watu wenye Ulemavu na mahitaji yao kupitia mfumo huo ulioanzishwa pamoja na usajili uliofanyika, Aidha taarifa za Watu wenye ulemavu sasa zinakusanywa kwa njia ya simu (Mobile Aplication). Ukusanyaji mwa taarifa kwa njia hii umeipunguzia serikali, Gharama ya kutumia karatasi nyingi kwa ajili ya kukusanyia taarifa vilevile mfumo huu unawezqa kuhesabiwa Mtu mwenye Ulemavu mara tu ya kumaliza kutoa taarifa zake.

 

 

• Kuwepo kwa taarifa ya   upembuzi yakinifu juu ya huduma ya afya ya ya uzazi na uzazi wa mpango kwa vijana wenye ulemavu Unguja na Pemba.  

 

• Kuwepo kwa Mpango mkakati wa Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu (2019 - 2024) ambao utasaidia Baraza kufanyakazi kwa ufanisi zaidi ya kuishauri Serikali kuhusu masuala ya Watu wenye Ulemavu na kutekeleza mambo muhimu kwa maendeleo ya Watu wenye Ulemavu.   

 

• Kuwepo kwa marekebisho ya Sera ya Watu wenye Ulemavu ya mwaka 2018 yatakayoenda sambamba na marekebisho ya Sheria au kutungwa Sheria mpya pamoja na mpango wa utekelezaji wa Sera hiyo ni msingi mzuri utakaowataka wadau wote kutoa haki kutoka ngazi ya Shehia hadi taifa na kufanya wajibu wao kwa Watu wenye Ulemavu hapa Zanzibar, sera hiyo imegusa maeneo 10, yakiwemo;

 

1. Upatikanaji wa huduma kwa Watu wenye Ulemavu,

2. Mifumo ya hifadhi ya jamii,

3. Usimamizi wa majanga,

4. Mazingatio katika ajira,

5. Ufikiaji wa huduma za mawasiliano,

6. Ufikiaji wa huduma za kinga na tiba,

7. Elimu na ushirikishwaji wa watu wenye Ulemavu,

8. Ufikiwaji wa haki za kisheria,

9. Ufikiaji wa Watu wenye Ulemavu katika michezo na burudani na,

10. Elimu, ushirikishwaji na ushiriki wa Watu wenye Ulemavu.

 

• Kuwepo kwa Maafisa Waratibu wa masuala ya Watu wenye Ulemavu katika Wizara za Serikali, kuwepo na maafisa walemavu Mkoa na maafisa walemavu Wilaya wanaosimamia utekelezaji na ushirikishwaji wa Watu wenye Ulemavu katika masuala mbali mbali kwa mujibu wa ngazi zao. 

 

• Kuanzishwa kwa Kamati za Shehia zitakazoshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu katika ngazi za Shehia.

Serikali imeweka muongozo maalum ili maendeleo ya nchi yetu           yasiwaache nyuma Watu wenye Ulemavu kwa kuboresha muundo wa taasisi wa Watu wenye ulemavu kwa kuanzisha Maafisa Walemavu Mkoa, Wilaya na Kamati za Shehia, hii inarahisisha kuibua changamoto mbalimbali za Watu wenye Ulemavu katika ngazi za shehia na serikali kuweza kuzifanyia kazi kwa haraka changamoto hizo.

 

• Kuwepo kwa Muongozo wa viwango vya Miundombinu rafiki kwa Watu wenye Ulemavu.  

• Kuwpo kwa mkakati wa ushawishi na mawasiliano wa Watu wenye Ulemavu

 

Ndugu waandishi wa habari; 

Nitoe shukurani zangu za dhati kwenu waandishi wa habari kwa kukubali kushirikiana nasi katika kufanikisha masuala mbali mbali ya Watu wenye Ulemavu likiwemo hili la leo. Aidha, mashirikiano haya ya karibu tunakuombeni yaweze kudumu zaidi na zaidi. 

Mwisho kabisa, nitoe wito kwenu na kukuombeni nyinyi waandishi wa habari kuwa, muwe mabalozi wazuri katika kuufanyia kazi kwa vitendo kauli mbiu yetu ya mwaka huu kwani tukifanya hivyo tunaweza kufikia sera ya serikali ya awamu ya nane ya Uchumi wa Buluu wenye neema na mafanikio mazuri kwa Watu wenye Ulemavu na Taifa kwa ujumla. 

 

AHSANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA 

 

 

About mmedia

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment