Wavuvi Pemba wataka waondolewe ushuru

 

wavuvi wa WeteMkoa wa  kaskazini Pemba 


WAVUVI wa Mkoa wa Kaskazini Pemba wameiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwaondolea ushuru kwenye vifaa vyote vya uvuvi, ili dhana ya uchumi wa buluu iweze kuwanyanyua wao na kuinyanyua Zanzibar kiuchumi.

 

Walisema kuwa, vifaa vya uvuvi vimekuwa na bei kubwa vinapofika Zanzibar kutokana na ushuru uliopo, kiasi ambacho wanashindwa kuvinunua na kusababisha kuvua samaki kidogo ambao hawakidhi mahitaji yao, kwani kipato kinachopatikana hakiwatoshelezi.

 

Walisema kuwa, wanaamini kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inawapenda sana na ndio maana ikaundwa Wizara ya Uchumi wa Buluu, hivyo ipo haja ya kuondolewa kila changamoto zinazowakabili, ili kuwainua kiuchumi kwani asilimia kubwa ya wananchi wa Pemba wanategemea rasilimali ya bahari.

 

"Vifaa tunavyotumianni nyavu, jarife, mishipi, mashine za boti na vifaa vyengine, lakini kwa hapa kwetu havinunuliki mpaka tuagize wenyewe kutoka Dubai inakuwa afadhali na kuagiza ni shida sana", walisema wavuvi hao.

 

Wakizungumza katika mkutano wa mapendekezo ya rasimu ya Sheria ya Uvuvi uliofanyika katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Wete, wavuvi hao walipendekeza Sheria ya kuwekewa mahakama yao maalumu, kwani wao sio wahalifu.

 

"Kwa nini sisi tunapelekwa mahakamani kama wahalifu, tunataka Sheria ituwekee mahakama yetu maalumu kama ilivyo kwa Baraza la Mji na sehemu nyengine, pia leseni za uvuvi zitolewe na Wizara ya Uchumi wa Buluu kwani ndio wanaojua shida zetu na sio SUMATRA", walisema.

 

Mwenyekiti wa Kamati ya Uvuvi Wilaya ya Wete Mohamed Kombo Hamad (Mwinyi mpeku) alifahamisha kuwa, Kamati za uvuvi zinahitaji zitambulike kisheria sambamba na mapato yao kukusanywa na Wizara inayohusika na uchumi wa buluu na sio Baraza la Mji ama Halmashauri, kwani wanapopata matatizo hata hawashughuliki.

 

"Kila siku tunakatwa fedha sio kidogo lakini zinapotokea matatizo baharini kama ya kupotea ama kuzama kwa boti, tunapigania wenyewe Baraza hata halitutambui, hivyo hatutaki wakusanye wao maana hazitunufaishi pesa zetu", alisema Mwinyi Mpeku.

 

Aidha alisema kuwa, muwekezaji wowote atakaekwenda kuekeza katika mkondo wa Pemba lazima Kamati zishirikishwe, ili wapate ajira ambazo zitakuwepo.

 

Kwa upande wake Bidawa Kassim Haji alieleza kuwa, katika Sheria mpya ziwepo kanuni na leseni ambazo zitawalinda ndani na nje ya nchi kama silaha yao, kwani wavuvi wamekuwa wakipata tabu sana juu ya hilo.

 

Nae Kombo Malik Mbwana alisema, wavuvi wamekuwa wakizaraulika kiasi ambacho hata zinapotokea ajali hakuna boti za uokozi zinazokwenda kuwasaidia licha ya fedha ambazo wanakusanya kila siku wanaporudi kuvua.

 

"Kinachotushangaza ni kule tunapookota boti baharini, tukishazifikisha juu Serikali inazichukua na kuziuza bila sisi tulohangaika kutuuliza chochote, hii sio haki kwani tulitakiwa tupewe sisi tuliopata tabu, lakini sasa tutaziacha waje wachukue wenyewe", alisema.

 

Mapema akifungua mkutano huo Afisa Mdhamini Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi dk Salim Mohamed Hamza aliwataka washiriki wa mkutano huo kutoa mapendekezo ya Sheria ambayo yatasaidia kuboresha zaidi, ili uchumi uwe endelevu.

 

"Kama mnavyojua kwamba azma ya Serikali ya awamu ya nane ni kukuza uchumi katika mazingira ya bahari ili uwe endelevu, hivyo ikiwa Sheria zitakuwa nzuri, malengo ya Serikali yetu yataweza kufikiwa na wananchi watafaidika", alifahamisha Mdhamini huyo.

 

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi Salim Sudi Ame alieleza kuwa, lengo la kuboresha Sheria hizo ni kwenda mbele kimaendeleo, hivyo watoe maoni yao ili tume ya irekebishe Sheria hizo, kwani hawataki kuona kwamba Sheria  zinawakwaza wananchi.

 

Nae Mkurugenzi wa Idara ya Hifadhi alisema kuwa, sehemu kubwa ya Uchumi wa Zanzibar inategemea bahari, ni vyema wakaitumia fursa hiyo bila kuharibu rasilimali za bahari, kwani hawatoweza kuzalisha vizuri.

 

Akiwasilisha mada ya rasimu ya Sheria ya Uvuvi mwanasheria Asha Mohamed Kombo aliwataka wavuvi hao wasifanye uvuvi haramu ambao huharibu na badala yake watumie uvuvi wenye tija utawasaidia katika kuwapatia kipato kitakachowakwamua na maisha duni.

 

Mkutano huo wa siku moja ulifanyika katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Wete, ambao uliwashirikisha wavuvi na wakulima wa mwani, kwa lengo la kutoa mapendekezo yao yatakayosaidia kuboresha Sheria mpya.

About mmedia

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment