TAARIFA KWA UMMA TAARIFA YA UFANYIKAJI WA MITIHANI YA TAIFA YA SMZ KWA MWAKA 2021


Ndugu wanahabari, wanafunzi, wazazi/walezi na wananchi kwa ujumla mnaotusikiliza. Ndugu wananchi, Mitihani ya Taifa ya Darasa la Nne, Darasa la Sita na Kidato cha Pili ya mwaka 2021 itafanyika tarehe kuanzia tarehe 25 Oktoba,2021 hadi tarehe 12 Novemba, 2021. Kama ifuatavyo:


 Tarehe 25 Oktoba 2021 na tarehe 26 Oktoba, 2021 ni Mitihani ya Darasa Nne. Tarehe 27 Oktoba 2021 hadi tarehe 02 Novemba, 2021 ni Mitihani ya Darasa la Sita. Tarehe 03 Novemba hadi tarehe 12 Novemba ni Mitihani ya Kidato cha Pili. 


 Mitihani hii itafanyika kwa Vituo vyote 465 vya Darasa la Nne, 427 vya Darasa la Sita na 295 vya Kidato cha Pili. Ndugu wananchi, Kwa mwaka huu wa 2021, jumla ya watahiniwa 54,324 kati yao Wanawake ni 26,745 na Wanaume ni 27,579 wameandikishwa kufanya mtihani wa Darasa la Nne, kuna ongezeko la watahiniwa 3,372 sawa na asilimia 7.0 ikilinganishwa walioandikishwa mwaka 2020. 


Kwa Mtihani wa Darasa la Sita watahiniwa 47,471 wameandikishwa kufanya mtihani huo wakiwemo Wanawake 24,755 na Wanaume 22,715 Watahiniwa 13,253 wameongezeka sawa na asilimia 38.7 ikilinganishwa na mwaka 2020.


 Aidha Watahiniwa 32,957 wameandikishwa kufanya mtihani wa Kidato cha Pili kati yao Wanawake ni 17,405 na Wanaume ni 15,552 kunaupungufu wa Watahiniwa 9,165 sawa na asilimia 27.1 ikilinganishwa na idadi ya watahiniwa waliosajiliwa kufanya mtihani huu mwaka 2020. 


Kati ya Watahiniwa walioandikishwa, watahiniwa wenye mahitaji maalumu ni 40 kwa Darasa la Nne, 33 wa Darasa la Sita na 33 wa Kidato cha Pili ambao mitihani yao huandaliwa kwa mujibu wa hali za mahitaji yao ili kuwawezesha kupata haki yao ya elimu. Jumla ya wasimamizi 1,981 kwa Mtihani wa Darasa la Nne, 1,796 kwa Mtihani wa Darasa la Sita na 1,284 kwa Mtihani wa Kidato cha Pili wameteuliwa kusimamia Mitihani hii ya Mwaka 2021 kwa Zanzibar yote. 


Wasimamizi wote hao wamepatiwa mafunzo juu ya taratibu za usimamizi wa mitihani hiyo yaliyofanyika katika Wilaya zote. Ndugu wananchi, Baraza la Mitihani la Zanzibar linachukua nafasi hii kuwapongeza Walimu wote kwa juhudi kubwa wanazochukua katika kuwalea watoto wetu Kitaaluma na Kimaadili mema.


 Pia linawaomba wazazi/walezi na Wananchi wote kwa jumla kuwa karibu zaidi na watoto wao wanaofanya mitihani hii na wahakikishe kuwa wanafika katika vituo vyao vya mitihani kwa wakati kwa ajili ya kutumia haki yao ya msingi ya elimu. 


Aidha, Baraza linawaomba madereva na utingo wa gari za abiria kuzidisha busara na hekima kwa wanafunzi wakati wa kwenda na kurudi kufanya Mitihani yao.


 Ndugu wananchi, Baraza la Mitihani linapenda kuweka wazi kwamba, ufanyaji wa mtihani unahitaji amani na utulivu wa hali ya juu, hivyo linawasihi kwamba mtu yeyote asiyehusika asijaribu kusogelea Kituo cha Mtihani, kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na “Sheria na Kanuni za Mitihani”, na kwa yeyote atakayepatikana na hatia, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.


 Pia linawasisitiza Watahiniwa wote kujiepusha na vitendo vyote vinavyokwenda kinyume na Kanuni za Mitihani ikiwemo kufanya udanganyifu kwani atakayebainika kwenda kinyume na Kanuni na taratibu za mitihani, hatua za Kisheria zitachukuliwa dhidi yake ikiwa ni pamoja na kufutwa kwa matokeo yake yote.


 Kwa taarifa hii, Baraza linasisitiza kusitishwa kwa shughuli zote zisizokuwa za Mitihani hii katika Vituo vyote vya Mitihani. Mwisho Kwa niaba ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, tunawatakia Watahiniwa wote ufanyaji mwema wa Mitihani yao na wenye mafanikio. “Ahsanteni kwa kunisikiliza” Imetolewa na Mkurugenzi Baraza la Mitihani

About mmedia

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment