NA BENNY MWAIPAJA, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, ameishukuru Benki ya Dunia kwa
kuwekeza zaidi ya dola za Kimarekani bilioni 5.5, sawa na takriban Sh.trilioni
12.6 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.
Dk. Nchemba ametoa pongezi hizo wakati akizungumza na Makamu wa Rais wa Benki
ya Dunia, anayesimamia nchi za Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Dk.
Hafez Ghanem, wakati wa Mikutano ya Mwaka ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha
la Kimataifa (IMF), iliyofanyika kwa njia ya mtandao, Jijini Dar es Salaam.
“Miongoni mwa fedha hizo ni pamoja na kiasi cha dola za marekani bilioni 1.167
zilizotolewa na Benki hiyo kwa ajili ya kutekeleza miradi mitano ya maendeleo
ikiwemo ya sekta ya elimu, miundombinu, umeme na Tanzania ya Kidijitali kwa
lengo la kuchochea uchumi jumuishi na kupambana na umasikini,” alisema.
Alisema kuwa kiasi hicho cha fedha kinahusisha utekelezaji wa miradi 26 ya
maendeleo inayopata fedha kupitia dirisha la mikopo nafuu (IDA) la Benki ya
Dunia yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 5.502.
Waziri huyo alisema kuwa miradi 21 kati ya hiyo ni ya kitaifa yenye thamani ya
dola za Marekani bilioni 4.804 na miradi 5 ni ya Kikanda yenye thamani ya dola
za Marekani bilioni 0.698 na kwamba mpaka sasa kiasi cha dola za Marekani
bilioni 1.932 kimetolewa na Benki hiyo sawa na asilimia 35 ya fedha zote.
Akizungumzia hatua zinazochukuliwa na Serikali kupambana na athari za kiuchumi
na kijamii zilizosababishwa na ugonjwa wa UVIKO-19, Dkt. Mwigulu Nchemba
alisema, kuwa Serikali imeandaa mpango wa mwaka mmoja wa kukabiliana na athari
za ugonjwa huo utakaogharimu Sh. Trilioni 3.62
“Tayari Serikali imepokea dola za Kimarekani milioni 567.25 sawa na takribani
shilingi za Tanzania trilioni 1.3 kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF)
ukiwa ni mkopo nafuu kwa ajili ya kunusuru maisha ya watu pamoja na uchumi wa
nchi kutokana na athari hizo za UVIKO-19,” alieleza.
Alisema kuwa fedha hizo zimeelekezwa kutatua changamoto za athari za UVIKO-19
kwenye sekta ya utalii, kunusuru kaya masikini, maji, elimu na Afya upande wa
Tanzania Bara na Zanzibar na akatoa wito kwa wadau wengine wa maendeleo kuunga
mkono jitihada hizo za Serikali ili kusisimua uchumi wa nchi.
Dk. Nchemba alisema, kuwa hivi karibuni Serikali inatarajia kukamilisha mazungumzo
na Benki ya Dunia kwa ajili ya kupata fedha za miradi miwili ikiwemo mradi wa
kuboresha masuala ya ardhi na kuongeza msukumo wa kujifunza kupitia elimu ya
msingi.
Kuhusu suala la wanafunzi wanaoacha masomo, Dk. Nchemba alimwambia Makamu huyo
wa Rais wa Benki ya Dunia Dkt. Hafez Ghanem kwamba changamoto ni kubwa ambapo
takwimu zinaonesha kuwa wanafunzi (wasichana na wavulana) 198,620 waliacha
masomo katika shule za msingi wakati wanafunzi 113,484 wa shule za sekondari
waliacha masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo vifo, utoro, utovu wa nidhamu na
ujauzito.
“Serikali inachukua hatua mbalimbali kukabiliana na hali hiyo ikiwemo
kuanzishwa kwa mradi wa kuboresha elimu ya Sekondari (SEQUIP) na mradi wa
kuongeza ubora wa elimu ya msingi unaoombewa fedha kutoka Benki ya Dunia na
wadau wengine wa maendeleo.
Akizungumza katika Mkutano huo, Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayezisimamia
nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika, Dk. Ghanem, aliipongeza Tanzania kwa
hatua mbalimbali inazozichukua katika kusimamia uchumi na maendeleo ya wananchi
wake.
Aliahidi kuwa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Dunia itakutana hivi karibuni
kujadili maombi mbalimbali ya fedha yaliyotolewa na Tanzania kwa ajili ya
kutekeleza miradi ya maendeleo ili fedha hizo zipatikane kwa wakati.
Dk. Ghanem alishauri masuala kadhaa yafanyiwe kazi na Serikali ikiwemo kuongeza
jitihada ya kuyasaidia makundi maalumu yakiwemo ya vijana na wanawake ili
waweze kujengewa uwezo wa kiuchumi pamoja na kukuza ajira.
Alisema pia kuwa suala la wasichana wanaopata ujauzito wakiwa shuleni wajengewe
mazingira ya kuendelea na masomo baada ya kujifungua, suala ambalo Dk. Nchemba
alimweleza kuwa Serikali inalifanyia kazi na kuangalia utaratibu utakaofaa
zaidi kushughulikia suala hilo.
Aidha, Makamu wa Rais huyo wa Benki ya Dunia alipongeza utaratibu mzuri
ulioanzishwa na Serikali wa kuimarisha na kuishirikisha sekta binafsi katika
kutekeleza miradi mikubwa na ya kimkakati ya maendeleo kupitia mpango wa
ushirikiano wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi.
0 Comments:
Post a Comment